RAIS KIKWETE AMKABIDHI 'RUNGU' MAGUFULI...

John Magufuli.
Wahandishi washauri na makandarasi watakaoshindwa kukamilisha kazi waliyopewa na Serikali katika ujenzi wa barabara kwa kiwango tarajiwa na kwa wakati watafukuzwa kazi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kuagizwa na Rais Jakaya Kikwete kuwachukulia hatua kali makandarasi na wahandisi wa aina hiyo.
Ili kuepuka kuangukiwa ‘nyundo’ makandarasi hao wametakiwa kukamilisha ujenzi wa barabara walizopewa mkoani hapa ifikapo Aprili mwakani vinginevyo wafukuzwe nchini.
Mbali na makandarasi hao, Rais Kikwete pia alimtaka Waziri wa Ujenzi awatimue kazi wahandisi washauri, watakaozembea kusimamia vizuri makandarasi wanaojenga barabara kwa kiwango cha lami nchini kwa kushindwa kutelekeza majukumu yao ipasavyo.
Alitoa agizo hilo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Chipukizi mjini hapa. 
Rais Kikwete alisema kwa kuwa asilimia kubwa ya fedha wanayolipwa makandarasi hao inatokana na kodi za wananchi wakiwamo wa hapa, barabara zinazojengwa ni lazima ziwe za kiwango kizuri cha hali ya juu zenye kukidhi matarajio ya Watanzania.
“Wizara ya Ujenzi kuweni makini, wabaneni makandarasi wazembe na wahandisi washauri, Waziri ongeza ukali kwa kuwa hapa tunachohitaji ni barabara za kiwango,” alisema Kikwete.
Alisema wakati akiomba kura kwa wananchi wa  Tabora, kilio chao kikubwa kilikuwa ukosefu wa miundombinu ya barabara yenye kiwango cha lami inayounganisha  mikoa jirani na Serikali yao imesikiliza kilio chao.
Alisema akiwa katika kampeni za kuomba ridhaa kwa wana Tabora kuwa Rais, aliahidi kuwajengea barabara ya kiwango cha lami itakayounganisha mikoa jirani ya Singida, Shinyanga na Kigoma na kuondoa kero ya ukosefu wa barabara za uhakika kwa mkoa huo tangu nchi ipate uhuru.
Waziri Magufuli alisema, atahakikisha agizo la Rais linatekelezwa kwa nguvu zake zote na hataogopa mkandarasi yeyote bila kujali ni Mchina, Mzungu au Mweusi.
Alisema hatakubali kutimuliwa kazi kwa kuogopa kufukuza mkandarasi na kabla hajafukuzwa uwaziri, atawafukuza kwanza wao.
“Nakuhakikisha tu kwamba mimi kabla hujanitimua kazi, hawa jamaa lazima nile nao sahani moja, wasisingizie mvua wala nini, mbona kule kwao wanajenga hata kama kuna mvua!
“Kule kwao huwa kuna wakati wa baridi sana mpaka barafu na hawaachi kujenga barabara, sasa kwa nini hapa kwetu wanatwambia mvua zimezidi? Nakuhakikishia usiwe na shaka yoyote, hawa nitapambana nao tu,” alisema.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item