CHADEMA SASA YAITENGA RASMI ZANZIBAR...

John Mnyika.
Mbali na kukosa ushawishi katika siasa za Zanzibar ikilinganishwa na Bara ambako imewekeza nguvu kubwa kwa muda mrefu, sasa  Chadema imeamua kuitenga Zanzibar.
Moja ya dalili za hatua hiyo ni sera yake ya majimbo inayokwenda sambamba na kuondoa wakuu wa mikoa, ambayo haiihusu Zanzibar kwa namna yoyote ile.
Chadema katika maoni yake ya Katiba mpya, viongozi wake walitaka Katiba hiyo ianzishe majimbo yasiyozidi 10, ili kuweka ilichodai ni mgawanyo sawa wa rasilimali za nchi.
Mapendekezo ya majimbo yaliyotajwa pamoja na mikoa itakayojumuishwa ni Nyanza Magharibi lenye mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga; Nyanza Mashariki lenye Mwanza, Mara na Simiyu.
Jimbo la Kanda ya Nyanda za Juu litakuwa na mikoa ya Njombe, Mbeya na Ruvuma na la Ziwa Tanganyika lenye mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.
Mengine ni Kati ambalo lina Dodoma, Tabora, Singida na Iringa na la Kaskazini lenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Chadema ilipendekeza majimbo mengine kuwa  ni Pwani ya Kaskazini lenye Tanga, sehemu ya Pwani na sehemu ya Morogoro,  Jimbo la Dar es Salaam na la Pwani Kusini lenye Mtwara, Lindi, Mafia, Rufiji na Ulanga.
Katika mapendekezo ya sera hiyo, Zanzibar haikuguswa wala kuzungumzwa kama itaendelea kuwa na mikoa kama ilivyo sasa au italazimika kuwa na majimbo.
Msemaji wa Chama hicho, John Mnyika alisema Chadema inaitambua Zanzibar kuwa nchi kamili inayoweza kujiamulia mambo yake, kutokana na kuwa na Katiba inayojitegemea, uongozi na mifumo ya kiutawala.
Mnyika ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Sekretarieti ya Chama hicho iliyowasilisha maoni mbele ya Tume, alisema chama hicho kilipendekeza Serikali tatu na kwamba Tanganyika ndiyo itakayokuwa na utawala wa majimbo.
Kwa mujibu wa Mnyika, Serikali nyingine zilizopendekezwa ni ya Shirikisho la Muungano na ya Zanzibar.
“Sera yetu ya majimbo na ya kuondoa wakuu wa mikoa itahusu Tanganyika peke yake kwa sababu Zanzibar ni nchi inayoweza kujiamulia mifumo yake ya utawala na ina Katiba inayojitegemea na uongozi uliokamilika,” alifafanua Mnyika.
Alisema endapo Zanzibar itataka kufuata mfumo huo wa utawala wa majimbo, itakuwa huru kufanya hivyo kulingana na matakwa ya Katiba inayoiongoza ambayo hata hivyo, haitaihusu Tanganyika.
“Hiyo ndiyo sera ya chama chetu sasa, Zanzibar wakitaka kuifuata itakuwa ni juu yao,” aliongeza kwa kauli iliyoonesha kama vile chama hicho hakipo Zanzibar.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item