SERIKALI YAANDAA BEI ELEKEZI YA VIWANJA...

Goodluck ole Medeye
Wananchi wa kipato cha chini nchini wataanza kupata nafuu watakapotaka kununua viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.
Hali hiyo itatokana na kuanza kutangazwa kwa bei elekezi ya ununuzi wa ardhi kwa ajili ya kujenga makazi bora nchini kote.
Hiyo inatokana na kuendekea kupanda kwa bei ya ardhi nchini na hata kuifanya watu wa kipato cha chini kushindwa kununua maeneo ya ujenzi wa nyumba bora.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye alisema jana katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa ,Jijini hapa kwamba wananchi wengi wanashindwa kununua viwanja hasa vinavyouzwa na halmashauri.
Kutokana na hali hiyo, alisema Rais Jakaya Kikwete aliagiza Serikali itoe bei elekezi kwa nchi nzima ili kuondoa kero na malalamiko ya wananchi wengi kushindwa kumudu bei ya viwanja ambavyo vimekuwa vikiuzwa na halmashauri hizo.
"Hivi karibuni tutatoa bei elekezi kwa nchi nzima tunatarajia bei za viwanja kushuka," alisema.
Alitoa mfano wa Arusha na halmashauri za mkoa huo kwamba zinaongoza kwa upangaji bei kubwa za viwanja hasa katika uanzishaji wa miji mipya na kusababisha masikini washindwe kununua ardhi.
"Kwa mfano bei za viwanja hapa Arusha ni kubwa kuliko hata Dar es Salaam … karibuni tutatoa bei elekezi," alisema Medeye.
Utaratibu wa kutangazwa bei elekezi ulianzia kwenye mafuta jamii ya petroli ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) kila mwisho wa mwezi imekuwa ikitoa bei hiyo.
Hatua hiyo ilitokana na soko huria kupanga bei na hivyo kusababisha baadhi ya wafanyabiashara ya mafuta kujipangia bei kubwa na kuumiza walaji.
Katika kikao hicho cha madiwani, Medeye alisema pia Serikali imetoa utaratibu wa malipo ya fidia ya ardhi inayochukuliwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Katika utaratibu huo kwa wageni kutoka nje ambao maeneo yao yatapitiwa na miradi ya maendeleo kama barabara, alisema hawatalipwa fidia na badala yale watalipwa gharama za kuendeleza ardhi hiyo.
Awali Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Arusha, Deusdedit Kakoko ililalamikia gharama kubwa za fidia za ujenzi wa barabara mpya ambazo zimepangwa kujengwa hapa.
Kakoko alisema Tanroads inatarajiwa kutumia zaidi ya Sh bilioni 200 katika ujenzi wa awamu ya kwanza wa barabara ya njia nne kutoa eneo la Usa River hadi mjini hapa.
Ujenzi wa barabara hiyo kwa mujibu wa Kakoko, utakuwa kwa awamu ambapo ya kwanza itakuwa ya kilometa 15 kati ya 22.3 ambazo zimepangwa kukamilisha ujenzi huo kutokana na gharama kubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo akizungumza katika kikao hicho alisema haridhishwi na kasi ya ujenzi wa barabara katika halmashauri za Arusha na kuagiza kasi iongezwe ili kutoa huduma za mawasiliano ya uhakika kwa wananchi.
Alisema yapo maeneo barabara zimetengenezwa chini ya viwango na cha kushangaza wapo wataalamu wamezipitia na kuziidhinisha wakati zikiwa chini ya viwango na hazilingani na thamani ya fedha halisi zilizotumika.
Alitumia fursa hiyo kupongeza wabunge wa mkoa huo kwa mara ya kwanza kuhudhuria kwa wingi kikao hicho na kuwakumbusha kuwa wajibu wao ni kusaidia upatikanaji wa fedha za barabara.
Pia aliwakumbusha kuwa wanapaswa kutembelea barabara zote kabla ya kufanya vikao kama hicho.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item