MORANI WAINGILIA KATI MGOGORO KANISA LA KKKT...

Baadhi ya Morani wa Kimasai wakiwa katika shughuli zao za kijadi.
Vijana wa kimasai maarufu kama Morani, wameingilia kati mgogoro wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati na kutoa masharti kwa uongozi kumrudisha kazini Mchungaji Philemoni Mollel wa Usharika wa Ngateu.
Taarifa zilizotufikia jana, zilieleza kuwa morani zaidi ya 300 tayari wameandaliwa na wametoa muda wa siku tatu kuanzia leo kwa uongozi wa Dayosisi hiyo, kumrudisha kazini Mollel.
Mchungaji Mollel alisimamishwa kazi na kuzuiwa kufanya kazi za kichungaji katika Kanisa hilo kuanzia Desemba 24, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni makosa yasiyovumilika ndani ya Kanisa.
Kabla ya kusimamishwa kazi Mchungaji huyo, kuliibuka mgogoro katika Kanisa hilo baada ya moja ya benki za biashara (jina tunalo) kuipa Dayosisi hiyo muda hadi Desemba 31 mwaka jana iwe imelipa deni la Sh bilioni 11, vinginevyo mali zake zingepigwa mnada.
Kutokana na taarifa hiyo ya benki, Kanisa lilitoa waraka wa Askofu ambapo waumini zaidi ya 600,000 walitakiwa kila mmoja achangie Sh 20,000 ili kunusuru mali za Kanisa zilizo hatarini kufilisiwa baada ya hoteli ya Corridor Springs, mali ya Kanisa hilo kudaiwa fedha hizo.
Baada ya waraka huo, baadhi ya waumini akiwamo Mollel walitaka waliohusika na uzembe uliosababisha deni hilo, wawajibike kabla ya waumini kutoa mchango huo.
Kutokana na msimamo huo, Mollel alitakiwa kuomba radhi na alipokataa, alisimamishwa kazi na kuvuliwa madaraka ya kuhudumia Usharika wa Ngateu aliokuwa akihudumia.
Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili jana, zilieleza kuwa morani hao walipanga kumrudisha madarakani Mchungaji huyo kwa nguvu.
Kabla ya uamuzi huo wa Morani, mtoa habari wetu alieleza kuwa vikao vya mchana na usiku vilifanyika vikihusisha wachungaji, wainjilisti na washarika kutoka Jimbo la Arusha Magharibi ambalo linasimamia Usharika huo.
Katika vikao hivyo, ilielezwa kuwa uamuzi huo ulifikiwa kwa maelezo kuwa Mchungaji Mollel hana kosa, kwani alikuwa akitimiza wajibu wake wa kusema ukweli juu ya hali ilivyo ndani ya Kanisa hilo.
Chanzo kingine cha habari kilieleza kuwa iwapo uongozi wa Dayosisi hautatekeleza maazimio ya vikao hivyo ndani ya siku hizo tatu kuanzia leo, morani kutoka Jimbo la Arusha Magharibi, watachukua hatua za makusudi za kumrudisha kwa nguvu Mchungaji huyo.
Hatua hizo zimepangwa kuchukuliwa Jumapili na vikao hivyo vimepanga morani hao waandamane kwa amani wakiwa na mavazi ya kimasai ya lubega kwenda nyumbani kwake Ngaramtoni, Arumeru mkoani hapa.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item