WACHUNGAJI WA KKKT WATISHIA KUJIVUA UCHUNGAJI...

Wakati Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ikikumbwa na migogoro kiasi cha kuutikisa uongozi wa dayosisi hiyo mkoani Arusha, mgogoro mwingine unaonekana kufukuta katika dayosisi ya hapa.
Katika sakata jipya mkoani hapa, baadhi ya wachungaji wa dayosisi hiyo wametishia kukabidhi kola zao za uchungaji kwa Kanisa, endapo uamuzi wa kuwahamisha vituo vyao vya kazi hautatenguliwa.
Uchunguzi wetu kutoka makao makuu ya dayosisi hiyo, Mpwapwa na Kondoa, umebaini, kuwa baadhi ya wachungaji walioguswa na uhamisho wanalalamikia uonevu, wakidai wanakomolewa na pia uongozi mpya wa Dayosisi chini ya Askofu Amon Munyunyu aliyeshika madaraka Novemba mwaka jana, unapanga safu yake.
Habari zaidi zinasema uamuzi huo unalenga kumtafutia nafasi mmoja wa waliokuwa viongozi wakubwa wa kanisa hilo aliyekuwa masomoni, hivyo kufanya panguapangua kwa kuwaondoa baadhi ya wachungaji wanaotajwa kutokuwa katika ‘mtandao’ wa uongozi. Hali hiyo imewafanya wachungaji hao kudai kwamba wako tayari kuacha kazi kuliko kuonewa.
Pamoja na kupinga uhamisho huo kwa maandishi, hakuna mchungaji aliyefanikiwa kuushawishi uongozi kubadili msimamo na hivyo wote kutakiwa kuhamia vituo vyao vipya vya kazi.
Nakala zilizopatikana za barua za baadhi ya wachungaji waliohamishwa, moja ikisomeka: “Kwa niaba ya uongozi wa Dayosisi ninashukuru kwa kupokea na kuukubali uhamisho. Aidha, barua yako ya tarehe 3.12.2012 imethaminiwa sana. Baada ya ofisi kuu kukaa na kutafakari juu ya ombi la kuahirisha uhamisho wako imetoa uamuzi ufutao:
“Sababu ulizotoa hazina nguvu ya kuifanya Halmashauri Kuu itoe uamuzi vinginevyo juu ya uhamisho wako. Hivyo uongozi unakutakia Krismasi njema na Heri ya Mwaka Mpya unapojiandaa kwenda kuripoti kituo chako kipya cha kazi.”
Mmoja wa waliopata barua za kukataliwa kubatilishwa kwa uhamisho wao, aliomba asihame kutokana na sababu za kiafya, akisema ushauri wa madaktari unamtaka asifanye kazi mbali na hospitali. Mbali na maelezo, pia aliambatanisha vyeti vinavyothibitisha sababu za kiafya zinazomtaka kutokuwa mbali na familia yake au hospitali.
Hata hivyo, uongozi huo wa KKKT Dayosisi ya Dodoma ulisema sababu zilizotolewa hazina nguvu ya kubadilisha uhamisho huo.
Mchungaji mwingine ambaye alikataa jina lake lisitajwe gazetini, alidai katika moja ya vikao vya wachungaji, wainjilisti na wafanyakazi wa ofisi (parish workers), mmoja wa viongozi alisema watumishi hao wasithubutu kupuuza ushauri wa madaktari, kwa kuwa uzembe huo unaweza kuwagharimu kama ulivyomgharimu aliyekuwa Askofu mstaafu, Festo Ngowo ambaye anaumwa.
Msaidizi wa Askofu, Mchungaji Mshana Samuel ambaye ndiye aliyesaini barua ya uhamisho kwa wachungaji hao pamoja na kupigiwa mara kwa mara simu yake ya mkononi, iliita bila ya kupokewa.
Mwandishi aliwasiliana na Askofu wa KKKT Jimbo la Dodoma, Kinyunyu, akakanusha kutoa uhamisho kwa mchungaji yeyote na kwamba hana mamlaka ya kufanya hivyo. Kadhalika, alisema hajapokea malalamiko kuhusu jambo hilo. 
“Kama kuna mchungaji amekwenda kwenye vyombo vya habari, basi huyo hatufai na atakapobainika tutamshughulikia kwa kumfukuza, kwani hata naye ana wachunguzi wake. Kama kuna malalamiko, huyo mchungaji ana mwajiri wake, basi angefuata utaratibu ili asikilizwe,” alisema Askofu Kinyunyu.
Alipoulizwa kuwa barua ya uhamisho na ya malalamiko ya uhamisho zimenakiliwa kwake na isitoshe tayari mwajiri kupitia Halmashauri Kuu ameshajibu kuwa maombi ya kuahirisha uhamisho hayana msingi hivyo aende kuripoti kituo kipya, Askofu alikana kuzipokea lakini akasema hata kama uhamisho huo ulifanywa na msaidizi wake, yeye alikuwa anatekeleza uamuzi wa vikao vyenye mamlaka ya kufanya hivyo.
Aliongeza kuwa kila mchungaji amekula kiapo, hivyo hakuna sababu kwa mchungaji kukataa kwenda kuhudumu sehemu nyingine ndani ya jimbo kwa visingizio.
Wakati Dodoma chokochoko zikianzia kwenye uhamisho wa kikazi, katika Dayosisi ya Kaskazini Kati, Arusha, chanzo kikuu kinaelezwa kuwa matumizi mabaya ya rasilimali za kanisa ambapo mali za kanisa hilo, ikiwamo hoteli ya kitalii ya Arusha Corridor Springs na hospitali ya Selian, zinatajwa kuwa hatarini kufilisiwa ili kulipa deni la benki moja nchini linalokadiriwa kufikia Sh bilioni 11.
Ili kukabiliana na deni hilo linalotokana na mkopo, waumini zaidi ya 600,000 wa kanisa hilo walitakiwa kuchangia Sh 20,000 kila mmoja, ili kunusuru mali za kanisa zisipigwe mnada.
Na kuanzia hapo, waumini na wachungaji walicharuka kuhoji juu ya deni hilo, kutokana na ukweli, kwamba vitega uchumi hivyo vya kanisa haviendeshwi kihasara.
Miongoni mwa waliobeba ‘bango’  kupinga michango hiyo, huku wakitaka viongozi wa  Dayosisi waliolitia aibu Kanisa na hata kukaribia kufilisiwa mali zake wawajibike, ni Mchungaji Philemon Mollel wa Usharika wa Ngateu, ambaye alivuliwa cheo na kufukuzwa uchungaji, jambo lililochangia msuguano ndani ya Dayosisi hiyo inayoongozwa na Askofu Dk Thomas Laizer.
Licha ya kumfukuza Mchungaji Mollel, Meneja wa Corridor Springs, John Kiama amefukuzwa kazi, sasa ikidaiwa amefichwa katika moja ya nchi za kiarabu na baadhi ya viongozi wa juu wa dayosisi.
Wakati mambo yakizidi kufukuta ndani ya Dayosisi ya Kaskazini Kati, Askofu Mkuu wa dayosisi hiyo, Dk Laizer amekasimu madaraka yake kwa Askofu Msaidizi Solomoni Massangwa, ikidaiwa kuwa Askofu Mkuu kwa sasa ni mgonjwa. 

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item