WAISLAMU, WAKRISTO WAVUTANA KUHUSU MAHAKAMA YA KADHI...

Wasichana kuolewa wakiwa na umri wa miaka 16 ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa jana mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba jijini Dar es Salaam.
Katika kuendelea kusikiliza maoni ya makundi mbalimbali Tume hiyo jana ilizungumza na makundi mbalimbali ya kidini na kupokea mapendekezo hayo kutoka Jumuiya ya Khoje Shia.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mohammed Dhilan alipendekeza Katiba iruhusu msichana mwenye umri wa miaka 16 aolewe kwa maelezo kuwa mwanamke anakomaa haraka kuliko mwanamume.
Pia Jumuiya hiyo ilipendekeza Katiba itamke kuwa kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 16 anaruhusiwa kupiga kura.
Pia ilitaka Mahakama ya Kadhi iingizwe kwenye Katiba kwa maelezo kuwa Mahakama hiyo ni bora kuliko mahakama zingine nchini.
Kwa upande wa ubunge, walipendekeza Katiba itamke kuwa mtu anaruhusiwa kugombea ubunge kwa vipindi viwili tu: "Wakikaa sana bungeni wanazoea na wanajisahau waliyotumwa na wananchi."
Pia walipendekeza adhabu ya kifo iendelee, kwa maelezo kuwa hukumu ya muuaji ni kifo. Walipendekeza pia Tume ya Uchaguzi ili iwe huru, ni vyema iundwe na wajumbe kutoka asasi za kiraia.
Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT) na Waadventista Wasabato (SDA) ni taasisi ambazo zilifika mbele ya Tume hiyo kutoa maoni yao wakipinga Mahakama ya Kadhi, lakini Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu pamoja na Muungano wa Jumuiya ya Khoje Shia Ithina-Sheri Jamaat ya Afrika wakitaka suala hilo liwekwe kwenye Katiba.
Makamu Rais wa Baraza la Maaskofu Severine Niwemugizi alisema Baraza lake linapinga Mahakama hiyo kuanzishwa na Serikali na kusisitiza kuwa Waislamu  ni lazima walichukue suala hilo kwa kuianzisha na kuigharimia kwa fedha za waumini wao.
Alisema mambo yanayohusu dini si vizuri yaingizwe kwenye gharama za Serikali na  kuwa makanisa yana vyombo ambavyo vinashughulika na masuala ya waumini wao yakiwamo masuala ya ndoa.
"Dini imekuwapo kabla ya Serikali; hivyo inaweza kuendesha mambo yake bila Serikali," alisema.
Alisisitiza kuwa katika maoni yao walisisitiza kuwa TEC haikubaliani na suala hilo kuingizwa kwenye Katiba, kwani jamii ambazo si waumini wa dini ya Kiislamu hawajui misingi ya Mahakama hiyo.
"Sisi tunachofahamu, Kadhi ni mtawala na hakimu, tukiidhinisha suala hili liingizwe kwenye Katiba, kesho Rais wa nchi ataambiwa ni lazima awe Kadhi ili awe na sifa za kuwa mtawala," alisema.
Alifafanua kuwa mambo yaliyojificha ndani ya Mahakama hiyo ni kuwa mtu hawezi kuwa Kadhi kama si Mwislamu, hivyo kuna hatari ya Katiba kulazimisha kuwa Rais lazima awe Mwislamu ili kukidhi matakwa ya Kadhi.
Askofu Niwemugizi ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo la Lulenge wilayani Ngara,  alisema kuna nchi kadhaa ulimwenguni ambako kuna Mahakama ya Kadhi na akaitaja Canada kuwa ni mfano mzuri, ambao Mahakama hiyo inaendeshwa na wataalamu wa masuala ya dini ya Kiislamu bila kuingiliwa na Serikali.
Kuhusu Ubalozi wa Vatican, Askofu Niwemugizi alisema Vatican tangu mwaka 1929 ilitengwa kama nchi licha ya kuwa ndani ya Italia na inatambulika kimataifa; hivyo iwapo Tanzania itavunja ubalozi wake nchini ni sawa na kuvunja Ubalozi wa Iran.
Alisema suala hilo wameliweka sawa kutokana na kelele zinazoendelea nchini kuwa Serikali inaendeshwa kwa mfumo wa Kanisa Katoliki na shinikizo za Waislamu kuwa Serikali sasa iruhusu Tanzania ijiunge na OIC kama ina ubalozi huo nchini.
Alitetea kuwa Ubalozi wa Vatican hauwakilishi mfumo wa Kikatoliki, bali makubaliano ya Vatican na Italia kama nchi yanakubalika katika nchi zote ulimwenguni. "Hata ukienda nchi ambazo zinaongozwa na Uislamu, Vatican ina ofisi za ubalozi, hivyo suala hilo si hapa nchini tu."
Askofu alisema katika maoni yao walisema malengo ya OIC ni kueneza Uislamu na kufuta Ukristo katika nchi wanachama, hivyo TEC pia hawakubali suala hili liingizwe kwenye Katiba. Pia walipendekeza   Katiba itamke kuwa rasilimali za asili lazima kwanza zinufaishe Watanzania kabla ya wageni.
Wasabato wanapinga viongozi wa dini kuingilia mambo ya siasa na kupendekeza suala hilo lisisitizwe kwenye Katiba, ili viongozi wa dini waendelee ‘kuchunga wanakondoo’ wa Mungu na viongozi wa Serikali waendelee kuendesha mambo yaliyo ya Kaisari.
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo jimbo la Mashariki mwa Tanzania (ETC), Mark Malekana alisema mambo mengine waliyopendekeza ni  Katiba kutamka wazi kuwa ni marufuku madhehebu ya dini kukashifiana na badala yake wavumiliane kwa jinsi ya imani zao.
Pia walipendekeza kuwa Katiba ya nchi iseme kuwa kiongozi wa nchi asipatikane kwa udini wake na badala yake achaguliwe kwa uwezo wake wa kazi bila kujali ametoka dini gani.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mwenza wa Kanisa hilo nchini, Mchungaji James Machage alisema katika Katiba mpya walipendekeza Serikali kama inataka kutoa ruzuku kwa madhehebu ya dini ambayo yanatoa huduma za jamii kama elimu na afya, itoe kwa taasisi zote za kidini.
“Mara nyingi makundi haya madogo yanasahauliwa na Serikali, sisi tumeomba Katiba mpya iilazimishe Serikali kusaidia kwenye shule na hospitali zinazomilikiwa na madhehebu mengine, badala ya kuangalia CCT na TEC tu," alisema  Machage.
Kanisa hilo lilisisitiza kuwa uhuru wa kuabudu usisitizwe kwenye Katiba mpya na asiwepo mtu wa kumlazimisha mtu kufanya kazi siku anayokwenda kuabudu au mwanafunzi  kulazimishwa kwenda shule siku yake ya kuabudu.
"Hili tumelisisitiza, kwa vile shuleni watoto wetu wananyanyaswa kutokana na usabato wao, wanalazimishwa kwenda shule siku ya Sabato na kufanya mitihani  shuleni na vyuoni."
Amir Mkuu wa Baraza la Jumuiya na taasisi za Kiislamu nchini, Musa Kundecha, alisema waliitaka Tume isilifanyie mzaha suala la Mahakama ya Kadhi na kupendekeza suala hilo litambuliwe kikatiba ili ligharimiwe na Serikali.
Alisema wanachotaka wao si kuwa na Kadhi mwenye ndevu, badala yake Mahakama yenye nguvu na itakayoongozwa na wasomi wa sheria za Kiislamu ambao watatoa hukumu kwa mambo ya ndoa, mirathi na talaka.
"Sijawahi kuona ulimwenguni Serikali iiachie wananchi waanzishe Mahakama yao, kuna hatari kubwa, suala hilo kuliacha mikononi mwa Waislamu, kwani wanaweza kuendesha sharia kinyume na sheria za nchi.
Maalim Ally Basalehe alisema Mahakama ya Kadhi ni kilio kikubwa cha Waislamu na sasa wamepata fursa ya suala hilo kuingizwa kwenye Katiba. Alisema iwapo Mahakama hiyo itakuwa na mamlaka kamili ya kiserikali, kutakuwa na nidhamu badala ya kuachiwa Waislamu wenyewe suala hilo.
Basalehe pia alisema walitaka Ijumaa iwe siku ya mapumziko kwa Waislamu wote na wanafunzi inapofika saa sita mchana, waruhusiwe kwenda msikitini. Haki ambayo wanaikosa tofauti na wenzao wanaokwenda kusali Jumamosi na Jumapili.
Baraza hilo pia lilizungumzia suala la OIC na kutaka Serikali isitumie fedha za walipa kodi kupamba ofisi zake kwa sikukuu ya Krismasi wakati wafanyakazi wa ofisi hizo ni wa dini tofauti.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item