WAJUKUU WA BIBI ALIYEUAWA WATAKA IUNDWE TUME...

Kamanda Charles Kenyela.
Wajukuu wa mwanamke aliyetekwa na kuuawa siku ya kusikiliza kesi yake ya kudhulumiwa nyumba,  Anastazia Kambanyuma wameiomba Serikali kuunda tume ya kuchunguza mauaji  hayo.
Wakizungumza jana jijini hapa walisema kifo cha bibi yao kilitokea katika mazingira ya kutatanisha na hata waliporipoti katika Kituo cha Polisi hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa.
Mmoja wa wajukuu ambaye ni msimamizi wa mirathi, David Kambanyuma alisema bibi yao alifariki Septemba 12 mwaka jana.
Alisema siku hiyo alitakiwa kwenda mahakamani kusikiliza kesi ya kudhulumiwa nyumba zake zilizopo Kariakoo, Magomeni, Kigogo na Kimara Stop Over .
Alisema waliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Mbezi kwa Yusuph na kupewa  taarifa ya Polisi yenye kumbukumbu namba RB/KMR/IR/7531/2012 na RB/KMR/2B/12234/2012 wakiwatuhumu baadhi ya watu waliotajwa kwa majina.
Alisema utata wa kifo unatokana na taarifa ya watuhumiwa ambao wanadai kuwa bibi yao alifariki kwa ugonjwa wa tumbo huku ripoti ya Daktari wa Hospitali ya Mwananyamala ikisema kuwa alikufa kwa kukosa pumzi.
“Sisi hatugombanii mali, bali tunataka haki itendeke kwa kuwa siku hizi vikongwe wengi wanauawa na kunyang’anywa mali zao na matapeli wachache ambao wanajipatia mali kwa njia ya udanganyifu,” alisema. 
Naye Elizabeth Kambanyuka alisema siku moja kabla ya kufa, bibi yao alitoweka nyumbani na kudaiwa alichukuliwa na watuhumiwa hao, na cha kushangaza watuhumiwa wanasema wana wosia na wamerithishwa mali zote.
Mwandishi alimtafuta mmoja wa watuhumiwa aliyekiri kuitwa  Kituo cha Polisi na kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo na kuwa madai yanayotolewa dhidi yao si ya kweli kwa kuwa yeye na bosi wake (aliyemtaja jina) walikuwa wanamlea bibi huyo aliyekuwa ametelekezwa na wajukuu zake.
Aliongeza kuwa wajukuu hao walimtelekeza bibi yao kwa miaka saba na kwa sasa wanajitokeza kwa sababu wanataka mali. “Kama ni hivyo wangefuata taratibu kujua wanazipataje na siyo kukimbilia katika vyombo vya habari,” alisema.
Akizungumzia kesi ya madai ya kudhulumiwa nyumba iliyofunguliwa na bibi huyo alisema ilikuwa kati ya Bibi Anastazia na mdogo wake anayeitwa Alexia ambao walikuwa wanagombania mali za marehemu baba yao hata hivyo walizungumza na kumaliza mgogoro huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela aliwataka wajukuu hao kupeleka malalamiko kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi  Kimara kuhoji sababu za watuhumiwa kutokamatwa. Alisema wasiporidhika na majibu waende kwake atashughulikia suala hilo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item