ASKOFU THOMAS LAIZER WA KKKT ALAZWA ICU...
https://roztoday.blogspot.com/2013/02/askofu-thomas-laizer-wa-kkkt-alazwa-icu.html
![]() |
| Askofu Thomas Laizer. |
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amemtembelea na kumjulia hali Askofu Thomas Laizer wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Selian jijini hapa.
Pinda alikwenda hospitalini hapo jana saa 9 alasiri na kukaa zaidi ya nusu saa, huku waandishi wa habari wakizuiwa kuingia katika chumba alimolazwa cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
Hata hivyo, baada ya kutoka katika chumba hicho kama ilivyo ada ya viongozi kuzungumzia hali ya mgonjwa, Pinda hakuzungumza na waandishi wa habari na kulikuwa na ulinzi mkali ambapo pia waandishi wa habari walizuiwa kuzungumza naye.
Askofu Laizer amelazwa kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na hakuna daktari wala ndugu aliye tayari kusema ugonjwa unaomsibu.
Awali ilisemekana kuwa Askofu Laizer amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Moshi mkoani Kilimanjaro, baada ya watu wengi kumiminika Selian kutaka kumwona, lakini jana ilidhihirika kuwa, amelazwa hospitalini hapo.
Mwandishi alijaribu kuzungumza na watumishi wa hospitali hiyo, ambao hawakutaka kutajwa majina yao, waliotaka waumini wamwombee Askofu Laizer.
Kabla ya Waziri Mkuu Pinda kufika hospitalini hapo, asubuhi alifungua mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), unaoshughulikia masuala ya gesi na mafuta na mchana alitembelea kituo cha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha SOS, Ngaramtoni, nje kidogo ya hapa.
Akiwa katika kituo hicho, Pinda alitoa Sh milioni 20 kusaidia watoto hao na kuomba wadau wengine, wenye uwezo kujitokeza kuwasaidia.
