"HAKUNA WANAJESHI WAVAMIZI KISIWA CHA UKEREWE"
https://roztoday.blogspot.com/2013/02/wanajeshi-wavamizi-kisiwa-cha-ukerewe.html
![]() |
| Mandhari ya Kisiwa cha Ukerewe. |
Baada ya Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli (Chadema), kuliambia Bunge kuwapo kwa askari wa Kenya na Uganda kinyemela kisiwani Ukerewe na kuhatarisha amani zipo taarifa kuwa hao ni maofisa uvuvi wa Afrika Mashariki.
Imeelezwa kuwa maofisa hao wako kisiwani humo wakishirikiana na polisi wa nchini kukamata nyavu zilizopigwa marufuku kutumiwa ziwani kuvua samaki.
Machemli, ambaye jana aliomba Mwongozo wa Spika na kupewa nafasi, aliliambia Bunge kuwa askari hao wa nchi jirani, wamekuwa wakipiga wananchi na kuwadhalilisha kwa kisingizio cha kudhibiti uvuvi haramu.
Mbunge huyo alisema askari hao wamekuwa wakidai kutafuta nyavu ndogo, ambazo wanadai ni haramu kwa shughuli za uvuvi.
Kutokana na kauli hiyo, Spika Anne Makinda, aliagiza Serikali kutafuta uhakika wa habari za askari hao wa Kenya na Uganda kuingia kinyemela kisiwani Ukerewe na kutoa taarifa.
Kauli hiyo ya Spika ilikuja bungeni jana baada ya Machemli (Chadema), kutoa hoja bungeni akitaka Bunge lijadili kuhusu kitendo cha askari wa nchi hizo kuingia nchini kinyemela.
Spika Makinda alisema Bunge haliwezi kujadili hoja hiyo wakati Serikali haijafanya uchunguzi wa kutosha kuhusu kuingia kwa askari hao na kuagiza ifanye uchunguzi kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa Mwandishi Jovither Kaijage, aliye Ukerewe, zilieleza kuwa hakuna uvamizi wa aina hiyo, isipokuwa ni operesheni dhidi ya uvuvi haramu, inayotekelezwa na maofisa uvuvi wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Inadaiwa maofisa hao wakisaidiwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), wamevunja nyumba na kupiga wananchi kwa kisingizio cha kutafuta zana haramu za uvuvi.
Habari kutoka kata za Ngoma, Bwiru na Ilangala zilisema kabla ya uperesheni hiyo kufanyika katika maeneo hayo, polisi walipiga risasi angani na kufyatua mabomu ya kutoa machozi.
Hali hiyo ilizua taharuki na kusababisha watu wakimbie ovyo huku wengine wakikamatwa na kupigwa, wakati huo baadhi ya milango ya nyumba zao ikivunjwa na maofisa hao kutafuta zana haramu za uvuvi.
Mmoja wa wafanyabiashara wa maduka katika mwalo wa Bukimwi, katika kata ya Ngoma, Ruigi Ghatawa, alidai katika ghasia hizo juzi mchana, duka lake lilivunjwa na fedha Sh 270,000 kuibwa na watu hao.
Ofisa Uvuvi wa Mkoa wa Mwanza, Lameck Mongo, anayeongoza operesheni hiyo ya siku sita iliyoanza Januari 31, alikanusha tuhuma hizo za kuvunja nyumba na kupiga watu.
Hata hivyo, alikiri kuwa polisi walitumia mabomu kutawanya wananchi ili wasidhuru maofisa hao wa doria na kuongeza kuwa wavuvi wanaonyang’anywa zana hizo haramu, ndio wanatoa taarifa hizo za uzushi ili waonekane wanaonewa.
Alisema wao hawakwenda Ukerewe kuonea watu, ila wanatafuta wahalifu na kuongeza kuwa ni lazima zana hizo zitafutwe na kuharibiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, mbali ya kuahidi kufuatilia ili kupata ukweli wa suala hilo, pia alisema hajapata taarifa hizo na kuongeza kuwa operesheni hiyo inatekelezwa chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya na ndiye anatakiwa kuulizwa suala hilo.
Mkuu wa Wilaya, Mary Tesha alipoulizwa , alipuuza madai hayo ya wananchi na kuongeza kuwa
hivyo ni visingizio baada ya zana haramu walizokuwa wakimiliki kukamatwa na kuharibiwa.
