BANGO LA MATANGAZO LAANGUKA UWANJA WA NDEGE NA KUUA MTOTO WA MIAKA 1O...
https://roztoday.blogspot.com/2013/03/bango-la-matangazo-laanguka-uwanja-wa.html
KUSHOTO: Luke Bresette enzi za uhai wake. KULIA: Wafanyakazi wa uokoaji wakipakia kwenye gari mwili wa Luke. |
Polisi wa Alabama wamesema Heather Bresette na watoto wake, wenye umri wa kati ya miaka 6 na 10, walikuwa wamesimama sambamba na bango hilo linaloonesha ratiba za ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Birmingham-Shuttlesworth ndipo lilipoanguka bila taarifa.
Luke Bresette, mwenye miaka 10, alitangazwa kuwa amekufa katika Hospitali ya Watoto ya Alabama, alisema Derrick Perryma. Heather Bresette amelazwa katika kitengo cha mahututi cha Hospitali ya UAB akiwa kavunjika vifundo vyake viwili vya miguu na kuteguka nyonga. Alifanyiwa upasuaji juzi.
Wavulana wengine wawili Sam, miaka 8, na Tyler, miaka 5, wanatibiwa kwenye Hospitali ya Watoto ya Alabama ambako hali zao inasemekana zinaendelea vizuri. Sam amevunjika mguu na pua, Tyler ana jeraha kwenye ubongo.
Mjomba wa mvulana aliyefariki amemwelezea mpwa wake kama baadhi ya wenye upendo mkubwa maishani.
"Alikuwa mvulana mzuri sana," alisema mjomba wake, Alex Bresette. "Alikuwa akifanya vema shuleni. Alikuwa mwenye akili na mdadisi."
Ajali hiyo mbaya ilitokea majira ya Saa 7:30 mchana wa Ijumaa wakati familia hiyo ikiwa inarejea Overland Park, mjini Kansas baada ya kutumia wiki nzima huko Destin kwa mapumziko ya majira ya bamvua.
Bango lenye uzito unaokadiriwa kuwa na uzito wa kati ya ratili 300-400 lilichunuka kutoka kwenye ukuta wa uwanja wa ndege huo mpya uliokarabatiwa, na kumwangukia Luke, mama yake na ndugu zake.
Mume na baba Ryan Bresette hakujeruhiwa, wala dada Anna na kaka mwingine, Joe.
Luke alikuwa wa tatu kati ya watoto watano na alikuwa darasa la tano katika Shule ya St. Thomas More.
Mjomba wake alisema alikuwa akicheza mpira wa magongo, mpira wa miguu, mpira wa kikapu na kuimba kwaya. Pia alikuwa shabiki mkubwa wa timu ya soka ya Notre Dame, na Kansas Jayhawks.
Mashuhuda walisema familia hiyo ilikuwa ikipita mbele ya bango hilo kubwa ndipo likawaangukia juu yao. Iliwalazimu wanaume sita kuweza kuliondoa bango hilo kutoka juu ya familia hiyo, na baadaye wanaume takribani 12 kuliinua wakati wafanyakazi wa uokoaji walipokuwa wakiihudumia familia hiyo.
Kipande hicho cha Uwanja wa Ndege kilifungwa kwa muda, na uchunguzi umeamza kujua sababu za kuanguka kwa bango hilo.
Alex Bresette ameelezea ajali hiyo kama ya kuogofya. "Tumehuzunishwa sana," alisema, "lakini tunashukuru kwa msaada tuliopata."
Bango hilo lenye uzito wa kati ya ratili 300 na 400 liliwalazimu watu 10 waliokuwa kando kuliinua kutoka kwa familia hiyo, alisema Mkuu wa Kikosi cha Moto na Uokoaji cha Birmingham, Donald Jones.
Baba wa watoto hao alisemekana kuwa alikuwa akiwatafuta katika dawati la karibu la Kusini-magharibi, kwa mujibu wa shuhuda, ndipo tukio hilo la kutisha lilipotokea majira ya Saa 7:30 mchana.
Safari za ndege kwenye uwanja huo zilisemekana kuwa hazikuathirika kutokana na tukio hilo la Ijumaa.