BILIONEA MWINGINE WA ARUSHA ADAIWA KUJIUA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/03/bilionea-mwingine-wa-arusha-adaiwa.html
KUSHOTO: Hospitali anayodaiwa Nyaga kujitupa ghorofani. KULIA: Nyaga Mawalla. |
Siku mbili baada ya kifo cha mfanyabishara maarufu wa madini wa jijini Arusha, Henry Nyiti, mfanyabiashara mwingine bilionea wa Jiji hilo, Nyaga Mawalla ameripotiwa kujiua usiku wa kuamkia jana.
Kifo cha Nyiti kilichotokea usiku wa kuamkia Alhamisi, kimeelezwa kimetokana na ugonjwa wa malaria uliompata akiwa katika migodi yake katika kijiji cha Ipanko, wilayani Ulanga, Morogoro.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu zilisema Mawalla mmoja wa mabilionea wenye umri mdogo akiwa hajafikisha miaka 40, alijirusha kutoka ghorofa la Hospitali ya Nairobi, Kenya alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki mbili.
Tukio hilo, habari zilisema, lilitokea wakati akiwa tayari ameruhusiwa kutoka hospitalini na alishamwita dereva wake tayari kwa safari ya kurudi nchini.
Juhudi za mwandishi kupata taarifa za kina kutoka kwa ndugu au washirika wake kikazi katika kampuni aliyokuwa akimiliki ya Mawalla Group hazikuzaa matunda, kwani simu zao ziliita bila kupokewa.
Hata hivyo, mmoja wa watu wa karibu na marehemu ambaye hakuwa tayari kutajwa jina gazetini kwa kuwa si msemaji wa familia, alithibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa, ingekuwa vigumu kupata wasemaji kwa kuwa karibu wote wako Nairobi kutokana na kifo hicho.
“Ni kweli hilo limetokea, lakini linatuchanganya, kwa sababu amechukua uamuzi wa kujiua wakati alisharuhusiwa kutoka hospitalini…sijui ni nini hasa kimemkumba,” alisema mmoja wa watoa habari wetu.
Alidokeza kuwa mwili wa marehemu ulitarajiwa kuwasili jana jioni kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), tayari kwa taratibu za mazishi nyumbani kwao Marangu, Kilimanjaro.
Licha ya kuwa wakili na mfanyabiashara maarufu, alikuwa pia mwalimu wa sheria, akifundisha kwa muda wa ziada katika Chuo Kikuu cha Makumira.
Taarifa za misiba ya wafanyabiashara hao maarufu zimeshitua wengi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, ambako walijijengea mitandao mikubwa ya kibiashara.
Katika mitaa ya Arusha, taarifa za wafanyabiashara hao zilionekana kugusa makundi mengi, kutokana na mikusanyiko isiyo rasmi iliyokuwa inajadili vifo hivyo.
Mjadala uliibuka pia kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakichangia juu ya kifo cha bilionea huyo kijana.
Mmoja wa wachangiaji hao kupitia mtandao wa jamiiforums.com, ameandika; "Marehemu Nyaga Mawalla alikuwa ana matatizo ya pumu siku nyingi, na alikuwa anakwenda Nairobi kwa matibabu, inashangaza kiasi fulani...maana alikwenda kikazi mpaka mauti yalipomkuta ambapo inasemekana kajiua… hii ni kwa mujibu wa Mwanandugu wa marehemu.”
Mwingine ameandika; “Nimeweza kuongea na ndugu wa karibu na ame confirm kwamba jamaa alifariki jana Nairobi Hospital ambapo alikuwa amelazwa kwa takribani wiki mbili.
“Alikuwa amekwenda Nairobi kwa sababu dawa zake alizokuwa anatumia zilikuwa hazifanyi kazi, kwa hiyo madaktari wakawa wamebadilisha dawa. Akiwa Nairobi alikuwa amekataa kuonana na watu. Alikuwa anaonana na mdogo wake, Casmir na dereva wake ambaye walikwenda wote.
“Jana (juzi) alikuwa na dereva wake siku nzima, ilipofika mchana akamwambia aondoke chumbani ili apumzike. Huku nyuma aliruka kutoka ghorofani kwa nia ya kujiua. Hatuwezi kujua pengine hizo dawa zilimfanya achanganyikiwe akili au kuna lingine kubwa.”
Wakati haijafahamika siku ambayo Mawalla atazikwa, habari kutoka kwa familia ya Nyiti aliyekuwa pia kada wa CCM, zilieleza kuwa mwili wa mpendwa wao unatarajiwa kuzikwa kesho Tengeru, Arumeru, Arusha.