HUKUMU YA OFISA WA TAKUKURU ALIYEUA POLISI YATENGULIWA...

Mahakama ya Rufaa Tanzania.
Mahakama ya Rufaa Tanzania inayoendelea na vikao vyake mjini hapa imetengua hukumu dhidi ya Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Egidius Rugemalila aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia askari Polisi aliyetaka kumkamata kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.
Hata hivyo, tayari Rugemalila amemaliza kutumikia kifungo hicho cha kuua bila kukusudia katika tukio hilo lililotokea mkoani Singida.
Rufaa hiyo ilikuwa ikisikilizwa na jopo la majaji watatu Angella Kileo, Benard Luanda na Catherine Oriyo.
Ilidaiwa kuwa Koplo Laban alikuwa ni askari Polisi mwenye namba D.4322 na mshtakiwa alikuwa ameajiriwa na Takukuru kama Ofisa Uchunguzi na siku ya tukio alipewa kazi ya  kumfuatilia na kumkamata Laban ambaye alikuwa akituhumiwa kuomba rushwa.
Mahakama hiyo iliambiwa kuwa muomba rufaa (Rugemalila) alifika hotelini akiwa na mtu mwingine  ambapo baada ya muda askari huyo alipewa fedha kwa lengo la kukamatishwa rushwa.
Lakini hata hivyo Laban hakukubali kukamatwa na hapo mtafaruku ulitokea hali ambayo ilisababisha askari huyo kupiga teke sufuria la chai ambapo chai hiyo iliyokuwa ya moto ilimjeruhi mtu aliyekuwa na mshtakiwa ambaye alikuwa shahidi wa tatu upande wa utetezi.
Baada ya kitendo hicho ilidaiwa kuwa askari huyo akatoka nje na kuanza kukimbia kwenda Kituo cha Polisi lakini kabla hajafika alipigwa risasi na kuanguka chini.
Katika kesi hiyo Rugemalila kupitia kwa Wakili wake, Njulumi  aliwasilisha sababu tano ikiwemo Jaji aliyesikiliza kesi hiyo alikosea kisheria na kimaelezo na kumuelewa vibaya shahidi namba nne na kusababisha kutotendewa haki.
Pia ushahidi wa shahidi namba 4 haukuangaliwa kwa makini kwani upo uwezekano kulikuwa na patashika na bastola ilipigwa kwa mkono na risasi kufyatuka.
Pia upande wa mashtaka haukuleta mahakamani ramani ya tukio ili kulinganisha maelezo ya shahidi namba nne na hata Jaji alishindwa kutatua tatizo la ushahidi uliokuwa ukigongana kwani shahidi namba nne aliona tukio na shahidi namba tatu alifika Kituo cha Polisi na akaona Laban akipigwa risasi na kuanguka.
Wakili wa muomba rufaa alidai kuwa Jaji alitakiwa kuangalia kama Laban alipigwa risasi wakati akikimbilia Kituo cha Polisi.
Akitoa uamuzi huo wa jopo la majaji, Jaji Kileo alisema kuwa, ushahidi uliomtia hatiani mshtakiwa ulikuwa na maswali mengi hasa mgongano wa shahidi namba tatu na shahidi namba nne.
“Kama marehemu alipigwa risasi na muomba rufaa basi jeraha lilitakiwa kuwa mgongoni na si tumboni jambo ambalo limethibitishwa na mashahidi na ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu. Pia ushahidi unaonesha kuwa kabla ya tukio hilo kulikuwa na mapambano, Laban akikataa kukamatwa na mapambano hayo yalipelekea askari huyo kujeruhiwa,” ilisema sehemu ya hukumu hiyo.
Pia upande wa mashtaka ulitakiwa kuthibitisha shtaka hilo bila kuacha mashaka yoyote kwani mashtaka yaliyoonekana yamekuwa faida kwa mleta rufaa.
Alidai kuwa kutokana na hali hiyo, licha ya mshtakiwa kumalizia kutumikia kifungo chake cha miaka mitatu hukumu aliyohukumiwa inatenguliwa. Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na wakili wa Serikali, Angaza Mwipopo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item