LWAKATARE AANGUKIA MIKONONI MWA MWANASHERIA WA POLISI...

Wilfred Lwakatare.
Hatima ya kufikishwa au kutofikishwa mahakamani kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare ipo mikononi mwa
Mwanasheria wa Polisi wa Kanda.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema jana kwamba ingawa upo uwezekano wa kufikishwa leo mahakamani, lakini wanasubiria uamuzi wa Mwanasheria huyo wa Kanda.
 “Lengo ni kufikishwa mahakamani kesho (leo), uwezekano huo upo, lakini unasubiria uamuzi wa Mwanasheria wa Kanda, yeye ndio anajua kwa kina kuhusu hatma hiyo,” alisema Kova wakati akizungumza na mwandishi.
Lwakatare anashikiliwa na Polisi tangu Jamatano iliyopita, akituhumiwa kuonekana kwenye video iliyowekwa kwenye mitandao, akizungumzia mipango ya kukamata waandishi wa habari.
Kova alipotakiwa kufafanua kuhusu kuendelea kukaa rumande kwa kiongozi huyo wa Chadema zaidi ya saa 24 tangu kukamatwa, alisema hana jibu kuhusu swali hilo,  litajulikana mahakamani.
Katika kufuatilia kwa baadhi ya wanasheria, wanasema muda anaopaswa kushikiliwa mtuhumiwa ni saa 48.
Hata hivyo, mmoja wa wanasheria na Wakili wa Kujitegemea, Emmanuel Makene alifafanua “kama anaweza kuhatarisha upatikanaji wa ushahidi au usalama, sheria hiyo hiyo ambayo hata  Uingereza wanaitumia utaambiwa inabidi akae ndani.”
Wakati huo huo taarifa zilizotufikia jana kuhusu sakata hilo, inadaiwa polisi walikwenda kufanya ukaguzi tena katika ofisi ya Lwakatare iliyopo  Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Kova na Wakili wa Lwakatare, Nyaronyo Kicheere, walikanusha kwa nyakati tofauti na kutoa ufafanuzi wa kilichojiri jana.
“Hakuna upekuzi wowote uliofanyika leo (jana), tulienda tu na polisi ofisini kuchukua nyaraka moja ambayo ilikuwa inahitajika na wala si kwamba walienda kupekua, nani huyo anazusha mambo ya ajabu ajabu hivyo?” Alionya Kicheere.
Akielezea hali ya mteja wake, Kicheere alisema afya ya Lwakatare ambaye inadaiwa anasumbuliwa na kisukari, bado si nzuri na jana alipelekewa dawa na kaka yake ambaye ni Daktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini Polisi hawakumpa.
Wakili huyo alidai ratiba yake ya chakula, inapaswa kuwa mara nne kwa siku, lakini haizingatiwi.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene akizungumza na gazeti hili jana, aliomba Polisi iharakishe kumfikisha kiongozi huyo mahakamani ili apate haki yake ya msingi ya dhamana na kumuondolea mateso anayoyapata kutokana na afya yake.
Lwakatare mbali na kuwa Kiongozi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, pia ni mwanasiasa mwenye historia nchini, aliyewahi kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini kupitia CUF kuanzia mwaka 2000 hadi 2005 kabla ya kuhamia Chadema.
Mwanasiasa huyo ambaye yumo katika video iliyowekwa kwenye mitandao, akizungumza maneno yanayodaiwa ni ya uchochezi, kukamatwa kwake kumekuja siku chache baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) na Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006, Absalom Kibanda.
Katika hatua nyingine, Mkoa Maalumu wa Vyuo Vikuu wa Kanda ya Dar es Salaam wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM)  umetaka wanaharakati na wanasiasa kuacha kuingilia au kuvuruga taratibu za kisheria na kiusalama katika uchunguzi wa watu waliohusika kumvamia Kibanda.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Wilaya ya Dar es Salaam ya kanda hiyo, Daniel Zenda wamelaani uvamizi uliofanyika siyo tu kwa Kibanda, bali pia kwa viongozi wa dini.
“Tumevitaka vyombo vya Dola kuwakamata, kuwashikilia na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliothibitika kuhusika na matukio ya namna hiyo bila kuangalia itikadi za kivyama.
“Pia tunayataka makundi ya kijamii, wanaharakati na wanasiasa kuacha kuingilia au kuvuruga kwa namna yoyote taratibu za kisheria na kiusalama,” ilisema sehemu ya taarifa.
Tamko hilo walilitoa jana kwenye kikao cha kujadili mipango na mikakati mbalimbali ya kuimarisha mkoa huo na chama.
Kibanda ambaye amelazwa hospitalini Afrika Kusini, alishambuliwa hivi karibuni na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam, usiku.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item