LWAKATARE APANDISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA UGAIDI...

Wilfred Lwakatare akiongozwa kutoka mahakamani jana.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam,
akikabiliwa na mashitaka ya ugaidi.
Lwakatare ambaye ameshitakiwa pamoja na Ludovick Joseph, alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka manne ya kula njama, kufanya mkutano na kuhamasisha vitendo vya ugaidi chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi na Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Katika mashitaka hayo, washitakiwa wanadaiwa Desemba 28 eneo la King’ong’o Kimara Stop Over,  Kinondoni Dar es Salaam, walipanga njama ya kutenda kosa la jinai la kutumia sumu, kumdhuru Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
Wakili wa Serikali Mkuu, Prudence Rweyongeza, alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, kuwa  washitakiwa hao walipanga njama za kigaidi za kumteka Msacky kinyume cha sheria ya kuzuia ugaidi.
Aliendelea kudai, kuwa siku hiyo hiyo, washitakiwa walipanga na kushiriki katika mkutano wenye lengo la  kigaidi  la kumteka Msacky.
Katika mashitaka yanayomkabili Lwakatare,  Wakili Rweyongeza alidai kuwa aliruhusu mkutano kati yake na Joseph, ufanyike nyumbani kwake King’ong’o, ili kuhamasisha vitendo vya ugaidi.
Washitakiwa walikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi kesho, Hakimu atakapotoa uamuzi kama wapate dhamana au la.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba washitakiwa wanyimwe dhamana kwa kuwa wameshitakiwa chini ya sheria ya ugaidi.
Mashitaka hayo kwa mujibu wa sheria hiyo, yanapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu na hayana dhamana. Upande huo wa mashitaka, pia uliomba Joseph aendelee kuwa chini ya ulinzi wa Polisi, kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.
Hata hivyo, upande wa utetezi, uliiomba Mahakama itoe dhamana kwa kuwa ni haki ya kikatiba na kudai kuwa Mahakama haitakiwi kuangalia hati ya mashitaka pekee.
Mawakili wa utetezi walidai kuwa Mahakama, inapaswa kuchunguza kinachoelezwa na upande wa mashitaka kama kinakwenda sawa na sheria walizoshitakiwa nazo washitakiwa.
Wakili Tundu Lissu, aliiomba Mahakama itupilie mbali mashitaka hayo kwa madai kuwa yalifikishwa hapo bila kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), akidai kuwa karatasi ambayo inaonesha ni kibali cha DPP, haina mhuri wala nyaraka muhimu zinazoonesha kuwa ni hati halali.
Wakili Profesa Abdallah Safari, aliiomba Mahakama kuchunguza kwa makini mashitaka, kwa kuwa kuna matumizi mabaya ya kisheria, ambayo ni kumbambikizia mashitaka Lwakatare kwa lengo la kumnyima dhamana.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa sheria iko wazi, kuwa mashitaka yanayowakabili washitakiwa, hayana dhamana na kuhusu kubambikiwa kesi,  itajulikana wakati ikianza kusikilizwa na kuomba suala la siasa lisiingizwe katika kesi hiyo.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Mchauru alisema kesho atatoa uamuzi wa kama
mashitaka hayo yaondolewe au la, pamoja na suala la dhamana.
Wakili Peter Kibatala, aliiomba Mahakama iruhusu Lwakatare apewe daktari maalumu kwa kuwa anaumwa kisukari.
Hata hivyo, Hakimu Mchauru alisema ni mapema kuamua jambo hilo, kwa kuwa bado Magereza haijashindwa kumhudumia.
Lwakatare na Joseph walifikishwa mahakamani hapo jana saa 2.00 asubuhi wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser namba T140BLA na kukaa kwenye gari hilo hadi saa 7.00 mchana walipopandishwa kizimbani.
Kesi hiyo ilisikilizwa kwa saa mbili, ambapo washitakiwa waliondoka eneo la Mahakama saa 9:30 mchana huku wakisindikizwa na magari matano ya Polisi, likiwamo la maji ya kuwasha na lingine likiwa na askari wenye silaha na mbwa.
Wafuasi wa Chadema waliokuwa eneo la Mahakama, walisimama kumshangilia kiongozi huyo, alipokuwa akirudishwa rumande huku wakitoa salamu ya chama chao ya “People’s Power (Nguvu ya Umma).”
Katika kesi hiyo, Lwakatare anatetewa na jopo la mawakili Lissu, Kibatala, Nyaronyo Kicheere, Profesa Safari na Mabere Marando.
Wakati huo huo, Polisi inaendelea na uchunguzi ili kubaini watu wengine watakaounganishwa katika kesi ya ugaidi inayowakabili Lwakatare na Joseph.
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Msaidizi wa Polisi, Isaya Mngulu, alisema wanaendelea na upelelezi ili kubaini wahusika wengine katika mkasa huo.
Alipoulizwa Polisi imebaini nini katika mahojiano na Lwakatare, Mngulu alisema hawezi kuzungumza kwa undani kwani atavuruga ushahidi.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Saidi Mwema, alisema lengo ni kukomesha uhalifu nchini, ikiwa ni pamoja na wimbi la utekaji na utesaji wananchi, ambalo linaonekana kushika kasi.
Alisema Polisi inaweza kufanikisha hilo, ikiwa itapata ushirikiano wa wananchi ambao watafichua uhalifu kutokana na wahusika kuwa ndani ya jamii.
“Siku za nyuma tulikuwa na tatizo la uvamizi wa benki ambalo sasa limetoweka, hili tulifanikiwa kutokana na kushirikiana na wananchi na kutambua mtandano mzima wa uhalifu huo, vivyo hivyo kwa mauaji ya albino, ingawa sasa inaonekana kujirudia,” alisema.
Akizungumzia ucheleweshwaji wa upelelezi katika matukio mbalimbali, likiwamo la Mwenyekiti wa Madaktari, Steven Ulimboka, Mwema alisema upelelezi siku zote unachukua muda mrefu ili kujiridhisha na kupata wahusika.
“Si upelelezi wa tukio la Ulimboka, lakini kuna la (Absalom) Kibanda, Padri Mushi, kuna Shekhe Zanzibar na Arusha na pia mtu aliyemwagiwa tindikali Igunga, bado tuko katika kazi kubwa ya kuendelea na upelelezi wa matukio haya.
“Haya yote tutafanikiwa kwa ushirikiano wa raia wema, kwani hata suala la kutafutwa Osama bin Laden, lilitangazwa dunia nzima lakini je, ni muda gani ulitumika kumpata? Simaanishi kuwa ni lazima upelelezi wetu uchukue muda kama wa Osama,” alisema.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item