LWAKATARE NA WENZAKE WAFUTIWA MASHITAKA, WAKAMATWA TENA...

Wilfred Lwakatare (kushoto) akitoka Mahakama ya Kisutu.
Mkurugenzi wa Mashitika (DPP) amepeleka hati katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ya kuwafutia mashitaka ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa  Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake.

Akiwasilisha hati hiyo jana, Wakili wa Serikali Mkuu, Ponsiano Lukosi, alidai kuwa DPP amewasilisha hati hiyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambacho kinampa mamlaka ya kuondoa kesi yoyote mahakamani.
Alidai kuwa upande wa mashitaka uliona hauna haja ya kuendelea kuwashitaki washitakiwa hao.
Baada ya kupokea hati hiyo, Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, aliwaachia huru Lwakatare na Ludovick Joseph saa tatu asubuhi. 
Kesi hiyo jana ililetwa kutajwa ili kutoa uamuzi wa dhamana, baada ya upande wa utetezi kuomba mahakama itoe dhamana kwa Lwakatare, kwa kuwa ni haki ya kikatiba na kudai kuwa mshitakiwa amebambikiziwa mashitaka kwa lengo la kumnyima dhamana.
Mawakili wa upande wa utetezi, walidai kuwa Mahakama haitakiwi kuangalia hati ya mashitaka pekee, bali kuchunguza kinachoelezwa na upande wa mashitaka, kama kinakwenda sawa na sheria walizoshitakiwa nazo.
Wakili Tundu Lissu aliiomba Mahakama itupilie mbali mashitaka hayo kwa kuwa yaliwasilishwa bila kibali cha DPP, akidai kuwa karatasi ambayo inaonesha ni kibali cha DPP haina mhuri wala nyaraka muhimu zinazoonesha kuwa ni hati halali.
Saa 4.30 asubuhi, washitakiwa walipandishwa tena kizimbani, safari hii wakiwa mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana.
Washitakiwa hao walisomewa upya mashitaka manne ya kula njama na kufanya mkutano na kuhamasisha vitendo vya ugaidi, kinyume na Sheria ya Kuzuia Ugaidi na Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, hawakuruhusiwa kujibu chochote, kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi  haujakamilika na kuomba washitakiwa waendelee kuwa chini ya ulinzi wa Polisi ili kukamilisha upelelezi.
Wakili mwingine wa utetezi, Peter Kibatala, alidai kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa imefunguliwa kwa mashitaka hayo na kufutwa, aliomba kutaka kuwasilisha maombi yake.
Hata hivyo, Hakimu Katemana alitaka upande wa utetezi ulete maombi yao wakati kesi hiyo itakapotajwa tena Aprili 3 na washitakiwa wataendelea kubaki rumande.
Katika mashitaka hayo, washitakiwa wanadaiwa Desemba 28 mwaka jana katika eneo la King’ongo
Kimara Stop Over, wilayani Kinondoni Dar es Salaam, walipanga njama ya kutenda kosa la jinai la kutumia sumu kumdhuru Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
Katika mashitaka mengine, Wakili Lukosi, alidai kuwa  washitakiwa hao walipanga njama za kufanya kitendo cha ugaidi cha kumteka Msacky.
Walidai siku hiyo hiyo, washitakiwa walipanga na kushiriki mkutano wenye lengo la kutenda ugaidi, ambao ni kumteka Msacky.
Katika mashitaka yanayomkabili Lwakatare peke yake, Wakili Lukosi alidai kuwa aliruhusu mkutano kati yake na Joseph, ufanyike nyumbani kwake King’ong’o kwa lengo la kuhamasisha ugaidi.
Washitakiwa hao waliondolewa eneo la Mahakama saa 5 asubuhi, wakisindikizwa na magari matano ya Polisi, likiwamo la maji ya kuwasha na lingine likiwa na askari wenye silaha na mbwa.
Wafuasi wa Chadema walikusanyika nje ya Mahakama wakiwa  na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe wakipiga kelele za “People’s power!”
Mbowe aliwataka wanachama wake kutulia na kuacha Mahakama ifanye kazi, kwa madai kuwa alichofanyiwa Lwakatare, si jambo jipya.
Katika kesi hiyo, Lwakatare anatetewa na jopo la mawakili Lissu, Kibatala, Nyaronyo Kicheere, Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item