MSICHANA ALIYETEKWA KIBAHA KUREJEA TENA DARASANI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/03/msichana-aliyetekwa-kibaha-kurejea-tena.html
Binti huyo akitoka sehemu alimokuwa amefichwa kwa takribani miezi minne. |
Wakati kesi ya kuteka na kubaka binti mwenye umri wa miaka 16, inayokabili vijana watatu mkoani Pwani ikiendelea, binti huyo hatimaye ameruhusiwa kurejea shuleni.
Kabla ya kukumbwa na kadhia hiyo, binti huyo alikuwa akisoma kidato cha kwanza katika Sekondari ya Pangani.
Hata hivyo, hakufanikiwa kufanya mtihani wa mwisho wa darasa hilo, baada ya kutekwa na vijana watatu waliomfungia ndani kuanzia Novemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu.
Akizungumza na mwandishi hivi karibuni, babu wa binti huyo, Daudi Zakayo, alisema Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, alimwita na kumtaarifu kuwa wameridhika na sababu za binti huyo za kutofika shuleni kwa kipindi hicho na sasa anaruhusiwa kuendelea na masomo.
“Tayari amesharuhusiwa kuendelea na masomo shuleni kwao, lakini mimi na baba yake, bado tunatafakari kumruhusu aendelee pale na masomo yake au la,” alisema Zakayo.
Alisema baba ya binti huyo, kwa sasa anatafuta shule nyingine ili kuona uwezekano wa kumhamisha ili asome kwa utulivu kutokana na mazingira ya shule hiyo ambayo huenda yamsipe utulivu hasa kutokana na matukio yaliyompata.
“Unajua tukio lile, limetokea jirani kabisa na shuleni pale, ni wazi kuwa walimu na wanafunzi wote wanalifahamu na kujua kuwa (anamtaja) ndiye aliyetendwa, sasa tuna wasiwasi kuwa mazingira ya aina hii hayatamfaa kusoma, ni bora aende shule nyingine ambayo haina taarifa zozote za tukio hili,” alisema.
Binti huyo alifaulu darasa la saba katika shule ya msingi Kidimu wilayani Kibaha, Pwani na kuchaguliwa kujiunga na sekondari ya Pangani, lakini alishindwa kuendelea na masomo ya kidato cha pili baada ya kukumbwa na tukio la kutekwa na kubakwa.
Tayari watuhumiwa wa kitendo hicho, Faida Kazigwa, Isaka Kazigwa na Jovian Oswald, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa wa Pwani, kujibu tuhuma nne ikiwamo ya kula njama ya kutenda kosa.
Mashitaka mengine matatu ni pamoja na kudaiwa kubaka, kubaka kwa pamoja na kumweka kizuizini binti huyo na kufanya naye mapenzi bila ridhaa yake.
Hata hivyo, baada ya kusomewa mashitaka, vijana hao walikana mashitaka na shauri lao linatarajiwa kuendelea kusikilizwa katika Mahakama hiyo.
Katika tukio lenyewe, binti huyo alidai nje ya Mahakama, kwamba mmoja wa vijana hao alimwingilia kimwili mara kwa mara mpaka akapata ujauzito, lakini wakafanikiwa kuutoa kwa kuchemsha majani ya chai na kumnywesha kwa nguvu.
Alidai kuwa kipindi chote hicho aliwekewa mlinzi huku akizuiwa kutoka ndani na hata wakati polisi walipofika kwenye kibanda kilichokuwa maskani yao, hawakubaini chochote.
Lakini Februari 23, vijana hao waliondoka kwenye chumba hicho alfajiri na mmoja wao kusahau kufunga mlango, ndipo akapata upenyo na kukimbilia porini ambako alikutana na msamaria mwema aliyemsaidia.
Binti huyo alidai kuwa mtu huyo, mchoma mkaa alimsaidia kupitia porini hadi nyumbani kwao, ili asikutane na vijana hao ambapo alimpigia simu babu yake na akisaidiana na wakazi wa kijiji hicho na serikali za mitaa, walisaka vijana hao na kuwakamata.
Babu wa binti huyo, Zakayo, alidai kuwa mjukuu wake huyo alipotea Novemba 3 na walifanya juhudi zote za kumtafuta ikiwa ni pamoja na kuripoti Polisi, lakini bila mafanikio.
Aliongeza kuwa kutokana na binti huyo kutoonekana kwa muda mrefu, baba yake alikwenda kwa waganga na mmojawao akadai kuwa yuko maeneo hayo, lakini amefichwa kwenye mti na mganga huyo kufanya ‘mambo yake’ lakini hakuonekana.