SHY-ROSE BHANJI AZIDI KUMKALIA KOONI SAMUEL SITTA...

Shy-Rose Bhanji.

Mmoja wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Shy-Rose Bhanji amesema walishafanyiwa semina moja tu, iliyoandaliwa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na hivyo kulalamikiwa kuwa ni watoro, ni uonevu.

Mbunge huyo juzi alikuwa akijibu tuhuma walizotupiwa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo, Samuel Sitta kuwa wamekuwa wakikwepa vikao na kufanya mambo yao kwa maslahi binafsi.
“Semina pekee iliyowahi kufanyika kwa wabunge wa EALA ilikuwa ni baada ya kuchaguliwa takribani miezi 10 iliyopita. Katika semina hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Wizara, tuliambiwa Wizara itatupa mwongozo kabla ya vikao vya Bunge kuanza ili kuweka maslahi ya Taifa mbele, baada ya hapo hatujawahi kuitwa tena na Wizara,” alibainisha katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Alisema kikao pekee kilichoitishwa na Wizara ni cha Januari, Bujumbura, Burundi, wakati yeye akiwa India kwa matibabu.
Shy-Rose aliiomba Wizara ya Afrika Mashariki kuacha kile alichokiita ubabaishaji kwa kutoa kauli za uongo kwa Watanzania na badala yake iongeze kasi ya uwajibikaji. 
“Kama nilivyosema kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara imejitenga sana katika kutoa mwongozo na katika kufikia Watanzania wengi kwa kigezo kwamba Wizara haina fedha,” alisema Shy-Rose. 
Alimwomba Waziri Sitta kukaa na viongozi wa Wizara yake ili apate ukweli wa mambo. “Kwa vile amenitaja mimi moja kwa moja kuwa ni kinara wa kutoa udhuru…nasema si kweli hata kidogo … ninamheshimu Waziri Sitta kama kiongozi na mzazi wangu, lakini kauli yake imenisikitisha sana, kwani amenifedhehesha kwenye jamii, kwa kutoa kauli za kunichafulia jina kwa vile nimesema ukweli,” alilalamika Mbunge huyo.
Alishangaa kwamba katika mkutano wa Bajeti mwaka jana Dodoma, Waziri Sitta alimpongeza Shy-Rose miongoni mwa wabunge wengine wa EALA waliofanya kazi nzuri.
“Leo iweje abadili kauli yake? Au ni kwa vile nimesema ukweli?” alihoji na kuongeza kuwa penye ukweli hatasita kuumbua viongozi wasiowajibika.
Kuhusu suala la posho, alidai kuwa walialikwa mara moja tu bungeni, lakini wakaambiwa kila mtu ajigharimie malazi na usafiri. 
“Hivi inaingia akilini, ualikwe kwenda safari halafu ujigharimie? Yeye Sitta na Naibu Waziri kwa vile wanatumia magari ya Wizara na kuwekewa mafuta na kupewa posho kufika bungeni ndiyo maana inamwia rahisi kuzungumza” alisema.
Hata hivyo pamoja na masharti ya kujigharimia, Shy-Rose alidai alikuwa miongoni mwa wabunge waliohudhuria mkutano huo. “Suala la posho kwangu  halijawahi kuwa ajenda kuu hata siku moja,” alisema.
Aliitaka Wizara kushirikiana na wabunge wa EALA kuwafikia Watanzania wengi na kuwapa elimu juu ya  ushirikiano huu.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item