SITTA AWASHAMBULIA WABUNGE WA AFRIKA MASHARIKI...

Samwel Sitta.

Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepinga malalamiko ya wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuwa hawashirikishwi ikisema malalamiko ya baadhi ya wabunge hao ni ya ajabu na si ya kweli.
Aidha, wizara hiyo imesema baadhi ya wabunge wamekuwa na mambo yao mengi nje ya ubunge huo na vinapotokea vikao hawahudhurii na orodha ya mahudhurio inaonesha ukweli huo.
Akitoa ufafanuzi katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dar es Salaam jana, Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Samwel Sitta alisema katika kuwashirikisha ni pamoja na safari ya Mwenyekiti kualikwa katika uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya Wizara na uzinduzi wa shughuli za kiwizara.
“Wabunge hawa wana shughuli zao nyingi sana na hilo liko wazi, hao hao ni wafanyabiashara, hivyo namna ya kupanga vikao nao kuhudhuria ni tatizo, watambue kuwa kama wamegombea wahakikishe wanatekeleza,” alisema Sitta.
Alisema wabunge wa EALA wamekuwa wakishirikishwa katika shughuli za wizara ambayo hata hiyo haijawahi kupokea ombi lolote kutoka kwa mbunge na isilishughulikie.
Sitta alisema Wizara haina fungu la kuhudumia wabunge hao na hilo limekwishajadiliwa katika vikao vya kamati vilivyopita na ikabainika kuwa ofisi ya Bunge itaangalia uwezekano wa kuwapa ofisi na vitendea kazi vingine.
Juzi mbunge wa EALA Shy-Rose Bhanji alitoa malalamiko mbele ya Kamati hiyo akisema wabunge hao wamekuwa sawa na yatima.
Alisema wamekuwa wakitengwa katika masuala yanayohusu jumuiya hiyo nchini na kuiomba Kamati kuhakikisha sera ya utangamano ya Tanzania inaundwa rasmi, alidai kuwa hawana ofisi na hawajui wako chini ya chombo gani.
Sitta alisema malalamiko kuwa wizara imewatenga na imeshindwa kuwapa mwongozo wanapokwenda katika vikao vya Bunge, ni ya ajabu  yasiyo na ukweli wowote.
Alitaja mambo ambayo wizara imeyafanya kuwa ni kwa kushirikiana na ofisi ya Bunge imefanya uchambuzi na kuandaa mwongozo ambao utawezesha ushirikiano na uwajibikaji baina ya Bunge la Tanzania na wabunge wa Tanzania katika EALA.
“Mwongozo huu umewezesha kuundwa kwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inayotoa nafasi ya kutoa taarifa za utekelezaji na kupata mwongozo,” alisema Sitta.
Aidha, alisema kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge, iliandaliwa semina kwa wabunge hao baada ya kuteuliwa kwao, ili kujenga uelewa wao kuhusu jumuiya kabla hawajaanza kazi zao semina iliyofanyika Mei mwaka jana ambapo mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwamo changamoto na mafanikio ya Bunge hilo.
Alisema wajumbe walipewa katika semina hiyo vitabu kuhusu mfumo, taratibu, maeneo ya kuzingatia na vipaumbele vya Tanzania.
“Wizara iliandaa utaratibu wa kukutana na wabunge wa EALA kila kabla ya kikao cha Bunge la EALA mkutano ambao hufanyika sehemu ambako Bunge hufanyika na panapokuwa na suala nyeti Wizara huhakikisha inapata wadau kutoka sekta husika na kushirikiana nao ili kutoa uelewa sahihi kwa wabunge,” alisema Sitta.
Alisema wabunge wa EALA ni wawakilishi wa Bunge la Tanzania kwenye Bunge hilo na ndilo jimbo lao la uchaguzi, hivyo wana wajibu wa moja kwa moja katika Bunge la Tanzania na hivyo wanatarajiwa kutoa taarifa mara kwa mara za yanayojiri katika Jumuiya ikiwa ni pamoja na uamuzi unaofanyika na miswada iliyopitishwa ili kupata miongozo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item