WATU 40 BADO WAHOFIWA KUFUNIKWA NA JENGO DAR...
https://roztoday.blogspot.com/2013/03/watu-40-bado-wahofiwa-kufunikwa-na.html
Jengo hilo baada ya kuporomoka ambapo inahofiwa bado kuna watu 40 chini ya kifusi hiki. |
Ni tukio la kusikitisha na kuhuzunisha baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa likijengwa katika makutano ya barabara za Indira Gandhi na Morogoro jijini Dar es Salaam kuporomoka saa 2.30 asubuhi huku watu zaidi ya 40 wakihofiwa kufunikwa na kifusi.
Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Mohammed Gharib Bilal, mawaziri na viongozi wengine wa kitaifa ni miongoni mwa viongozi waliofika kushuhudia tukio hilo na kushindwa kuzuia kuonesha nyuso za majonzi.
Wakati watu zaidi ya 60 wanadaiwa kuwepo ndani ya jengo hilo wakati maafa hayo yalipotokea, wengi wao wakiwa vibarua, hadi jioni jana ni watu 20 tu ndio waliofanikiwa kuokolewa, 17 wakiwa hai na wengine watatu wakiwa wamepoteza maisha, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kova alisema inakadiriwa kuwa kati ya vibarua 50 na 60 walikuwa ndani ya jengo hilo lililoporomoka na jitihada za kuwaokoa zilikuwa zinaendelea kwa kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama, vikiwemo vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Kikosi cha Kukabiliana na Majanga ya Moto, Shirika la Msalaba Mwekundu na vinginevyo.
Kamanda Kova alimtaja mmiliki wa jengo hilo kuwa ni Ally Radha ambaye tayari amekamatwa na polisi, lakini mkandarasi aliyekuwa akilijenga hajapatikana na polisi inaendelea kumtafuta.
Kamanda Kova pia alieleza polisi inawashikilia maofisa watatu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ili kusaidia katika uchunguzi wa tukio hilo.
Wanaoshikiliwa ili kuisaidia Polisi kwa mujibu wa Kamanda Kova ni Mhandisi Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Ojare Salu, Mhandisi Majengo, Goodluck Mbanga na Mkaguzi Majengo Wilbroad Mbuliyaso. Alisema mmiliki na mjenzi wa jengo hilo wanasakwa.
Iddi Baka Pandisha mfanyabiashara wa Dar es Salaam akielezea tukio hilo, anasema saa 4 asubuhi alipigiwa simu na rafiki yake Andrew Juma mkazi wa Mwanza, akimweleza kuwa alikuwa ndani ya gari na mkewe akiwa amefukiwa na kifusi baada ya jengo hilo kuanguka akiwa ameegesha chini kununua tambuu katika duka la jirani.
“Rafiki yangu aliweza kunielekeza hadi jengo lilipo na niliweza kufika hapa tukiendelea kuwasiliana na rafiki yangu, lakini baadaye nilipompigia tena simu yake ilikuwa haipatikani,” alisema Pandisha.
Alisema pamoja na waokoaji kuokoa magari matatu, lakini matumaini ya kuonana na rafiki yake yalififia baada ya magari hayo kuwa si lile lililokuwa linatumiwa na rafiki yake aliyekuwa Dar es Salaam kwa shughuli zake binafsi.
Mtoto Ajiridha Virany (12) mwenye asilia ya Kiasia, alisema yeye na watoto wenzake 14 walikuwa wakicheza kwenye uwanja ulio jirani na jengo hilo ambao wamekuwa wakiutumia siku zote kwa michezo mbalimbali.
Alisema tofauti na siku zote, jana ilikuwa siku mbaya kwani ghafla waliliona jengo hilo likititia na kutoa vumbi zito katika eneo la jirani. Wakati walipotahamaki ili kujiokoa, watoto wengine 7 walifukiwa na kifusi ambapo alisema watatu waliweza kuokolewa wakiwa hai lakini wengine wanne walikuwa wamesalia kifusini.
Mtoto Ajiridha anawatambua kwa majina marafiki zake hao aliosema anatamani kuwaona rafiki zake Yusuph Khaki, Suhail Kharim, Zahidi Abbas na Tariman Damji, wakiokolewa wakiwa hai matumaini ambayo hata hivyo yalikuwa yakififia usoni mwa mtoto huyo kadri muda ulivyokuwa ukisonga mbele.
Kutokana na tukio hilo kwa watoto hao, mwandishi wa gazeti hili alishuhudia kuwepo kwa akina mama wenye asili ya kiasia wakiwa wametundukiwa dripu za maji kutokana na mshtuko walioupata huku wanaume wakilia kwa uchungu.
Kibarua Mwinyimvua Sheni anashangaa ni vipi ameweza kuepukana na janga hilo kwani ni miongoni mwa wafanyakazi ndani ya jengo hilo akiwa mfagizi, lakini baada ya kuingia kazini asubuhi, alitoka baadaye kidogo kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuata dawa na akiwa huko alipata taarifa za jengo kuporomoka.
“Nilipopata hizi taarifa sikujua kama ni jengo letu, niliporudi nilishangaa kuona watu wamejaa na nilipokaribia nililiona jengo likiwa limeporomoka. Namshukuru Mungu kwa kuweza kuniepusha maana sifahamu kama ningeweza kusalimika,” alisema.
Yeye pia alisema anatamani kuwaona marafiki zake wanne aliowataja kwa jina moja moja la Shukuru, Mustapha, Daudi na Issa aliowaacha ndani ya jengo hilo wakiokolewa wakiwa hai.
Shuhuda Mohammed Ally alisema wakiwa nje ya Msikiti ulio jirani na jengo hilo walishtuka kuona jengo hilo likiporomoka huku mafundi wakionekana kuwa juu yake waliokuwa wakimwaga zege.
“Tulianza kukimbia lakini baadhi yetu walikwenda kuwaokoa watoto wa kihindi waliokuwa wanacheza kwenye uwanja pembeni ya jengo lakini matokeo ndio kama unavyoona,” alisema.
Hata hivyo mashuhuda hao wote walikuwa na kauli zinazofanana juu ya kile wanachodhani kuwa chanzo cha tukio, wakisema ni kutokana na kujengwa kwa malighafi hafifu.
“Nadhani mnaweza kuona namna mahala hapa palivyojaa kifusi cha udongo badala ya mawe mawe, hii inadhihirisha wazi kwamba wajenzi walitumia saruji kidogo sana na hata nondo zilizotumika zilikuwa ni za milimita nane ambazo hazifai, “ alisema Sheni.
Rais Kikwete, Mke wa Rais, Salma Kikwete, Makamu wa Rais, Gharib Bilal, Waziri wa Mambo ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, wabunge na viongozi mbalimbali walifika kujionea janga hilo na kuonesha dhahiri kusikitishwa nalo.
Mkuu wa Mkoa alisema serikali itatumia wataalamu mbalimbali kuangalia chanzo cha kuanguka kwa jengo hilo, alisema pia wataangalia uimara wa jengo la jirani linalodaiwa kumilikiwa pia na Radha alilosema linadaiwa pia kujengwa chini ya kiwango.
NHC yatoa tamko
Wakizungumzia tukio hilo, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wanaomiliki asilimia 25 ya hisa za umiliki wa jengo hilo, wamemtupia lawama Ladha anayemiliki asilimia 75 kuwa ndiye anayepaswa kutoa majibu ya tukio hilo.
“Mradi huu wa ubia kati ya NHC na M/s Ladha Construction Limited ya Jijini Dar es Salaam ulianza kutekelezwa tarehe 4 Februari 2008 ambapo Shirika la Nyumba litakuwa na hisa asilimia 25 na mbia ana asilimia 75 mara baada ya mradi kukamilika.
“Kwa mujibu wa sera ya ubia iliyoanza kutumika mwaka 1993 na kuhuishwa mwaka 1995 na 2005, Shirika la Nyumba la Taifa lilikuwa likitoa ardhi ambayo ilikuwa ikihesabika kama asilimia 25 ya mtaji wake kwenye jengo husika na mbia alikuwa akipata asilimia 75.
“Kwa mujibu wa mkataba huo, mbia mwendelezaji M/s Ladha Construction Limited kama walivyo wabia wengine, anapaswa kabla ya kuanza ujenzi kupata vibali kutoka kwenye mamlaka husika na kuwa na wataalamu wa ujenzi na washauri waliokubalika na kuthibitishwa na mamlaka husika.
“Aidha, mbia huyu akishapata wataalamu hao ndiye anayehusika kuingia nao mikataba ya kazi ya kujenga na kusimamia ubora wa jengo husika kwa mujibu wa sheria. Katika mradi huu, mbia mwendelezaji aliajiri wataalamu wote waliosajiliwa na Mamlaka husika ambazo ni CRB, ERB, AQRB na Manispaa husika na mamlaka nyinginezo.
“Kwa kuwa ujenzi ulikuwa haujakamilika, Shirika lilikuwa bado halijapata asilimia 25 ya umiliki wake,” walisema NHC katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma.