WIZI WA MABILIONI MAMBO YA NJE WAKOSA USHAHIDI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/03/wizi-wa-mabilioni-mambo-ya-nje-wakosa.html
Mahadhi Juma Maalim. |
Wizi wa zaidi ya Sh bilioni 3.5 za kitengo cha Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, umethibitishwa, lakini ushahidi wa kupeleka mahakamani wahusika, umekosekana.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim, alisema hayo jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimaitafa.
Akijibu hoja ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimaitafa, Edward Lowassa, kuhusu sakata hilo, Mahadhi alisema fedha hizo, zilichukuliwa Hazina kinyemela na kitengo hicho kwa ajili ya safari za viongozi, ambazo hata hivyo hazikuwapo.
Kwa mujibu wa Mahadhi, baada ya Wizara kubaini kuna fedha zimezochotwa Hazina huku Waziri, Naibu wake na makatibu wakuu wakiwa hawapo, ikiwa pia haikuidhinisha utolewaji wake, iliomba msaada wa Takukuru ili kuchunguza zaidi tukio hilo.
“Uchunguzi wa Takukuru ulibaini kuwa fedha hizo kweli zilichotwa Hazina kwa uzembe ama nia ya kuiba,” alisema Mahadhi lakini zilikamatwa.
Baada ya kukiri hali hiyo, Lowassa na wajumbe wengine wa Kamati hiyo, walihoji sababu ya mpaka sasa wahusika kutofikishwa mahakamani, wakati Takukuru ikibaini fedha hizo kuchukuliwa kwa uzembe au nia ya kuiba.
Akijibu hoja hizo, Mahadhi alisema kutokana na ushauri wa Takukuru, wahusika wote licha ya kubainika kuhusika katika tukio hilo, ilikuwa ni vigumu kuwashitaki.
Kwa mujibu wa ushauri huo, hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja kwamba wahusika walitaka kuiba fedha hizo, na hivyo kuishia kuchukuliwa hatua za kiutawala pekee.
Wahusika ni maofisa zaidi ya watano kwa mujibu wa Mahadhi na hatua zilichukuliwa, ikiwamo Mkurugenzi wa Kitengo hicho, Anthony Itatiro, kusimamishwa kazi.
“Wizara imewachukulia hatua za kiutawala watumishi wote walio chini yake na aliye chini ya mamlaka ya Rais, anasubiri hatua zaidi kutoka mamlaka hiyo,” alisisitiza Mahadhi.
Kwa sasa Itatiro anasubiri hatua zaidi kutoka kwa Rais, kutokana na cheo chake kuwa chini ya mamlaka hiyo.
Pamoja na Itatiro, watumishi wengine wanaodaiwa kuhusishwa na sakata hilo, ni Ofisa wa Idara ya Itifaki, Shamim Khalfa; Kaimu Mhasibu Mkuu, Kasim Laizer; Mhasibu Deltha Mafie na Karani wa Fedha, Shabani Kesi.
Kutokana na sakata hilo, pia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliunda tume ya kuchunguza tukio hilo.
Katika hatua nyingine, Lowassa aligiza Wizara hiyo, kukusanya taarifa za kila ubalozi wa Tanzania nje ya nchi, zinazohusu sera ya Diplomasia ya Uchumi na masuala mbalimbali ya utalii.
Aidha wajumbe wa Kamati, waliitaka iunde kitengo rasmi cha diplomasia ya uchumi katika kila ubalozi wa Tanzania, lakini pia kuhakikisha ushirikiano baina ya wizara na wizara unaimarika, ili kutekeleza masuala muhimu ya maendeleo kwa ufanisi.
Akizungumza wakati wa kujadili sera hiyo ya diplomasia ya uchumi na namna itakavyonufaisha Tanzania, Lowassa alisema pamoja na kuwapo kwa sera hiyo, bado ushiriki wa balozi za Tanzania katika masuala ya uchumi wa nchi hauridhishi, huku kukiwa hakuna mfumo thabiti wa kushirikisha kiuchumi Watanzania waishio nje.