DEREVA ALIYEGONGA NA KUUA TRAFIKI AKAMATWA, MAZISHI KESHO...

Watu wakishuhudia tukio hilo eneo la Bamaga, Dar es Salaam.
Askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Koplo Elikiza Nko aliyekufa kwa  kugongwa na gari akiwa kazini eneo la Bamaga, Kinondoni juzi, anatarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwake Bunju, Dar es salaam.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mmoja wa maofisa wa Polisi ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji, kuzikwa kwa Nko kunatokana na kukamilika kwa uchunguzi wa kifo chake kilichosababishwa na mwendo kasi na uzembe wa dereva aliyemgonga ambaye hata hivyo alikimbia baada ya tukio hilo.
Nko alikutwa na mauti saa 7 mchana baada ya kugongwa na gari namba T 328 BML aina ya Land Rover Discovery  eneo la Bamaga baada ya kupita kwa msafara wa Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa  katika ziara jijini humo.
Juhudi za kuwapata Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela kuzungumzia hilo jana hazikuzaa matunda baada ya Mpinga kuwa eneo la msiba na Kenyela kwenye msafara wa Rais Kikwete.
Gari lililomgonga askari huyo kwa mujibu wa Kenyela ni mali ya Kanisa la Tanganyika Assemblies of God (TAG) na lilikuwa likiendeshwa na mtuhumiwa aliyetambulika kama Jackson Steven ambaye kwa sasa anashikiliwa katika kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam kwa mahojiano.
Wakati huo huo, Rais Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu Jeshi la Polisi Tanzania, Saidi Mwema, kwa kifo cha Koplo Elikiza.
 “Nimepokea kwa mshituko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Koplo Elikiza, ambaye nimejulishwa kwamba aligongwa na gari akiwa kazini eneo la Bamaga, wakati akiongoza msafara rasmi,” alisema Rais Kikwete
Alisema ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha, kwamba Koplo Elikiza amepoteza maisha akiwa kazini, kwenye utumishi wa Jeshi na nchi yake, na wakati Taifa bado linaendelea kuhitaji nguvu kazi yake.
Rais Kikwete alisema ataendelea kumkumbuka Koplo Elikiza kwa uaminifu wake kwa Polisi na kwa Taifa lake la Tanzania na kuongeza kuwa kifo chake si tu pigo kwa nchi, bali kwa Polisi na hasa kwa familia yake ambayo bado ilikuwa inahitaji mapenzi, uangalizi na usimamizi wa mama.
 “Nakutumia wewe IGP salamu zangu za rambirambi kuomboleza kifo hiki. Aidha, kupitia kwako nawatumia makamanda na askari wote wa Polisi Tanzania kwa kuondokewa na mwenzao.
“Naomba kupitia kwako, unifikishie salamu za pole ya dhati ya moyo wangu kwa familia ya marehemu. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa na naelewa machungu yao.
“Napenda wajue kuwa naungana nao kumwombea marehemu, na pia kumwomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, ailaze pema peponi roho ya Marehemu Koplo Elikiza. Amina,” alisema Rais Kikwete.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item