AFUNGWA MAISHA JELA KWA KUMNAJISI BINTI YAKE KATAVI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/afungwa-maisha-jela-kwa-kumnajisi-binti.html
Mkazi wa mtaa Kigamboni, Kata ya Shanwe mjini Mpanda, Katavi , Abisai Joseph (40) ametiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Mpanda na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kunajisi mtoto wake mwenye umri wa miaka sita.
Akisoma hukumu hiyo Jumatatu, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Chiganga Tengwa, alisema ameridhika pasipo shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka, Ally Mbwijo.
“Mahakama hii pasipo shaka yoyote hivyo imekutia hatiani mshitakiwa kwa kuvunja sheria , hivyo utatumika maisha yako yote jela ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia na tabia ya kufanya uovu huo ulioufanya mshitakiwa,” alisema Hakimu Tengwa.
Awali, Mwendesha Mashitaka , Mkaguzi wa Polisi Mbwijo, alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Desemba 18, mwaka jana saa tano usiku, akiwa nyumbani kwake mtaa wa Kigamboni.
Akiiambia Mahakama, kuwa usiku wa tukio, mshitakiwa alimnajisi binti yake huyo aliyekuwa amelala na mdogo wake chumbani, baada ya kumvizia akiwa anatoka nje ya nyumba hiyo peke yake kujisaidia.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mzazi huyo alimvamia binti yake na kumtendea unyama huo huku mtoto akilia kwa uchungu lakini mama yake aliyekuwa amelala chumbani hakusikia kelele kwa kuwa ana tatizo la kutosikia vizuri.
Mwendesha Mashitaka huyo aliendelea kuiambia Mahakama, kuwa baada ya mshitakiwa kumtendea unyama mtoto huyo, alimwamuru aingie ndani kulala, lakini aliendelea kulia kutokana na maumivu hata mama yake kumsikia na kumhoji mumewe kulikoni, akamjibu alikuta binti yao huyo akibakwa nje ya nyumba yao.
Ilielezwa mahakamni hapo kuwa baada ya kusikia maelezo ya mumewe aliwaarifu majirani ambao walimshauri na kumsindikiza kwenda kutoa taarifa hiyo Polisi ambako mtoto huyo alikana kubakwa nyumba jirani na kumtaja baba yake kuwa ndiye amemtendea unyama huo.
Mama huyo ambaye alikuwa shahidi muhimu katika shauri hilo, katika ushahidi wake aliiomba Mahakama imsamehe mumewe kwa kumpa adhabu ndogo.
Na baada ya mumewe kuhukumiwa mama huyo aliyefuatana mahakamani hapo na bintiye mdogo alimsihi binti huyo waagane na baba yake lakini alimkatalia kwa alichokieleza ni kutofurahishwa na unyama aliomtendea dada yake.