PROFESA MWANDOSYA AIBUKA NA KUMTETEA KIKWETE KUHUSU UDINI...

Prof. Mark Mwandosya.
Kauli ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), bungeni kwamba Rais Jakaya Kikwete ni mdini, imemlazimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, kuchambua safu ya uongozi Ikulu.

Akizungumza bungeni jana, Profesa Mwandosya alisema baada ya kusikia kauli za udini, tena dhidi ya Rais Kikwete binafsi, alianza kuangalia Ikulu, aliko Rais.
Profesa Mwandosya, aliyetangulia kujibu hoja za wabunge kabla ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, alisema kwa haraka haraka alibaini kuwa mawaziri wote wanne wa nchi, wanaomsaidia Rais Ikulu ni Wakristo wakati Rais ni Mwislamu.  
Mawaziri hao ni pamoja na Mwandosya mwenyewe, , Steven Wasira anayeshughulikia Uhusiano na Uratibu na Celina Kombani wa Utumishi wa Umma na George Mkuchika mwenye dhamana na Utawala Bora.
“Makatibu wakuu wote wanaomsaidia Rais ni Wakristo, Katibu wake na wakurugenzi wote akiwamo wa Mawasiliano ni wakristo, sasa hapo udini uko wapi? Sisi Watanzania ni jambo la ajabu kwetu na geni kuzungumzia udini…hili ni shetani anapita tu, nchi itakuwa imara, hakuna udini,” alisisitiza.
Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Rungwe Mashariki (CCM), pia alishangazwa na wabunge kuhoji kazi za Idara ya Usalama wa Taifa na kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama bungeni, wakati masuala hayo duniani kote yanazungumzwa kwenye vikao vya siri.
“Mambo ya ulinzi na usalama ni siri, haiwezekani kuyazungumzia hapa, hata Israel na Marekani mambo hayo yanazungumzwa katika vikao vya ndani,” alisema. 
Katika mchango wake huo wa dakika 15 zikiwamo tano alizopewa na Waziri mwenzake wa Utumishi, aliruhusiwa na Spika Anne Makinda kushukuru kutokana na kuugua kwa miaka miwili.
“Kama mtu aliyekuwa akichungulia kaburi, siwezi kuacha kutoa shukrani zangu kwa wabunge, Serikali na watu wote na jimboni. Sikuwepo miaka miwili lakini wamenivumilia na leo naweza kuzungumza, nawashukuru sana na pia kwa sala zenu Watanzania,” alisema.
Wakati akishambuliwa kwa udini na Lema, huku akiungwa mkono na wabunge wenzake wa Chadema, historia ya tangu kuibuka kwa mivutano ya kidini nchini, inaonesha Rais Kikwete ndiye kiongozi aliyelazimika mara kwa mara kuonya kuhusu mivutano hiyo, huku Upinzani ukizungumzia hatari hiyo mara chache au kwa kuchochea.
Mbali na kurudia kuzungumzia hali hiyo juzi wakati akizungumza na Watanzania wanaoishi Uholanzi, ambako alisisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kuzungumza, Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita, alizungumzia kwa kirefu mivutano hiyo. 
“Napenda kuzungumza nanyi leo kuhusu uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini.  Jambo hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali ilivyo sasa.
“Tumefikia mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali kubadili mwelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya.  Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo, ushirikiano na kuvumiliana itatoweka,” alisisitiza Rais Kikwete.  
Katika hotuba hiyo, Rais alisema nyaraka na kauli kali  zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu, zinamshawishi aamini kwamba kama viongozi hao hawatabadilisha mwelekeo, amani itatoweka.
“Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili makuu.  Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine, kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake. 
“Kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini, ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano,” alisema.
Alisema pia kila upande unailaumu Serikali kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo inaendeshwa huku Serikali haichukui hatua. 
Katika malalamiko hayo, pia Wakristo wanadai kuteswa na viongozi wao kuuawa na Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua.  “Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake. Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu,” alisema Rais Kikwete. 
Alisema Waislamu pia wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui hatua yoyote ya maana.
“Waislamu wanalalamika wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba Serikali inawapendelea Wakristo. Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo.
“Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea na hushiriki zaidi kwenye shughuli za Wakristo, kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga makanisa na shule za makanisa.  Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya maaskofu kuliko mashekhe wanapofariki,” alisema Rais Kikwete.
Alikumbusha kuwa ipo misikiti mitatu ya Dar es Salaam, ambayo ilimsomea itikafu afe. “Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Suleiman Kova.”
Rais Kikwete alisisitiza dhamira na msimamo wa Serikali anayoongoza kwa kuhakikishia Watanzania kuwa yeye na Serikali, hawapendelei upande wo wote. 
“Hatufurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake, ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa nyakati mbalimbali.
“ Vyombo vya usalama vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki, ni ulegevu wa mtu tu katika kutimiza wajibu wao, na si kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya Serikali,” alisema Rais Kiwete.  
Rais Kikwete alisema yeye binafsi habagui, na ameshiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila alipoalikwa, labda akose nafasi kwa sababu nyinginezo. 
Alikumbusha kuwa ameshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume Muhamad (S.A.W.), safari za Hija, ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo mengi.
Alisema pia ameshiriki mazishi ya mashekhe kama alivyofanya kwa maaskofu na watu mbalimbali, Waislamu na Wakristo. 
“Pale ambapo sikushiriki mazishi ya Shekhe au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi. 
“Kwa upande wa Waislamu, desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki dunia huwa kikwazo kwangu kushiriki, hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam, kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine, si nyepesi.
Wakristo hawana utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri, hivyo huniwia rahisi kushiriki,” alifafanua.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item