ASILIMIA 7 YA WATU WAZIMA TANZANIA WANA KISUKARI...
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi. Aidha, alizungumzia ugonjwa wa shinikizo la damu na kusema theluthi moja ya watu wazima wameathirika na asilimia 10 ndio wenye uelewa wa ugonjwa huo.
Dk Mwinyi alisema hayo jana wakati akizindua gari la Chama cha Kisukari nchini (TDA) la kutoa huduma ya kliniki kwa wenye kisukari, shinikizo la damu pamoja na magonjwa mengine.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TDA, Dk Kaushik Ramaiya, wapo watoto 900 wenye ugonjwa huo wa umri kati ya miaka minne na 21 na kwamba kwa walio na umri chini ya miaka 15 wako wagonjwa 475.
Waziri alisema idadi kubwa ya watanzania wamekuwa hawana utaratibu wa kupima afya zao. Alisema hufika wakati wakiwa katika hali mbaya.
“Ninawahisi wananchi kuacha tabia hiyo ya kutokuwa na utaratibu wa kupima afya zao, pia waangalie utaratibu wao wa kuishi pamoja na vyakula kwa kuongeza mazoezi ya mwili ili kudhibiti kuongezeka kwa uzito,” alisema na kuonya juu ya unywaji vilevi.
Kuhusu gari hilo alisema litaunganisha nguvu zinazofanywa na serikali katika kuboresha huduma za afya vijijini ambapo wananchi watapata fursa ya kupima afya zao pamoja na kukutana na wataalam wa afya ambao walishindwa kuwafikia kwa sababu ya umbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa TDA, Dk Ramaiya alisema gari hilo litafanya kazi Dar es Salaam na baada ya hapo litakwenda Kanda ya Ziwa kwani ndiko linakotarajiwa kuwafikia wananchi walio wengi.