MFUKO WA PENSHENI PSPF WACHUNGULIA KABURI...

Mkurugenzi Mkuu, Adam Mayingu.
Baada ya kukanusha kwa matangazo katika vyombo vya habari kuhusu hali mbaya ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mkurugenzi wake, Adam Mayingu, sasa amekiri kuwa na hali mbaya.

Amesema Mfuko huo una hali mbaya kifedha na huenda ukafa baada ya miaka mitatu ijayo, endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuunusuru.
Mayingu alisema hayo mjini hapa jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambayo baada ya kuona hali hiyo, iliitisha mkutano wa dharura wa viongozi wa PSPF na Wizara ya Fedha, ili kuona namna ya kuunusuru.
Serikali ilikiri kuhusika kuudhoofisha  Mfuko huo, na kuahidi mbele ya Kamati hiyo, kuwa itachukua hatua za haraka wiki hii, kwa kuanza kulipa madeni inayodaiwa na PSPF ikiwa ni hatua ya mwanzo ya kuukomboa.
Akitoa maelezo kuhusu hali ya Mfuko, Mkurugenzi huyo alisema unakabiliwa na uhaba wa fedha, kutokana na madeni makubwa yaliyoko nje  yanayosababisha uwezo wa kifedha kufikia asilimia 10 tu.
“PSPF kwa sasa uwezo wake kifedha, umeshuka na kufikia asilimia 10 kiwango ambacho ni cha chini, ikilinganishwa na kiwango kilichowekwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA), ambapo kila Mfuko wa hifadhi hutakiwa angalau kuwa na uwezo wa kifedha wa asilimia 40,” alisema Mayingu.
Alisema iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa za kuuokoa, ikiwa ni pamoja na Serikali kupitia taasisi zilizo chini yake kulipa madeni yao yanayodaiwa na Mfuko huo, baada ya miaka mitatu utakuwa umekufa kwa kushindwa kujiendesha.
Mayingu alisema hadi sasa Mfuko umefanya tathmini takribani tatu, za namna ya kupandisha kiwango chake kifedha na matokeo yalionesha kuwa tatizo kubwa la PSPF ni mlundikano wa madeni inayodai nje.
“Pia Serikali ilifanya uchunguzi kwa upande wake kwa Mfuko na kubaini kuwa mwaka 1997, Serikali ilitakiwa kuuchangia kutoka michango ya watumishi wake wastaafu kiasi cha Sh bilioni 250.
“Ripoti hiyo ilitabiri kuwa kiwango hicho kingeweza
kupanda na kufikia Sh bilioni 658.23 mwaka 2006, na hivyo Serikali ilitakiwa kuongeza michango,” alisisitiza.
Mayingu alisema Mfuko ulianzishwa bila fedha za kuuwezesha kufikia kiwango kinachotakiwa kuuendesha, na katika tathmini ya kwanza mwaka 2003, kabla ya Mfuko kulipa mafao, ilionekana Serikali inadaiwa fedha za wastaafu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, PSPF ilibeba mzigo wa Serikali baada ya kuanzishwa ambao sasa ni deni lililofikia Sh bilioni 933.4.
Alisema deni hilo, linatokana na malipo yaliyofanywa na Mfuko kwa wastaafu waliokuwapo kabla ya kuanzishwa, ambapo PSPF kwa wakati huo ilikuwa na uwezo wa kulipa mafao hayo kwa asilimia 93.3 lakini tangu ilipe fedha hizo hadi jana Serikali haikuwa imefidia deni hilo.
Katika tathmini ya pili mwaka 2007 baada ya Mfuko kuanza kulipa mafao, ilionesha kuwa hali inazidi kuwa mbaya, kwa kuwa deni ambalo Serikali inadaiwa, lilikua na kufikia Sh trilioni 3.3 huku uwezo wa fedha wa Mfuko ukishuka hadi asilimia 40.
Katika tathmini ya tatu mwaka 2010, ilionesha hali ya mfuko kuzidi kuwa mbaya, kwani uwezo wake kifedha ulishuka hadi asilimia 10 huku deni la nje likikua hadi Sh trilioni 6.4.
“Kitendo cha Serikali kushindwa kulipa angalau robo ya madeni haya, kinarudisha nyuma juhudi za Mfuko za kuboresha huduma zake kwa wateja,” alisema.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Kawawa (CCM), alisema ni wakati wa Serikali sasa kuanza kulipa madeni kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko mara moja ili kuuokoa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alionesha kusikitishwa na kitendo cha Serikali kuchelewa kulipa madeni hayo, na kuuweka Mfuko katika hali mbaya.
“Hali ingekuwa tofauti kama Mfuko ungelipwa Sh bilioni 250 tangu mwanzo kabla ya kuanzishwa,” alisema.
Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene, alikiri kuwa Serikali haikuutendea haki Mfuko huo na kuahidi kushirikiana na wenzake kutafuta suluhu ya tatizo hilo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item