BABA MTAKATIFU APONGEZA MUUNGANO TANGANYIKA NA ZANZIBAR...

Papa Francis I.
Viongozi wa mataifa mbalimbali akiwamo Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, wametuma salamu za pongezi kwa Rais Jakaya Kikwete kwa niaba ya Watanzania, kwa kuadhimisha miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. 

Muungano huo uliasisiwa na marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na marehemu Abeid Amaan Karume.  
Katika ujumbe huo uliotumwa jana kwa Rais Kikwete kupitia Ubalozi wa Vatican nchini, Papa Francis alisema: "Natuma salamu za furaha kwako na wananchi wako katika siku hii ya furaha ya Muungano.
“Nikiwa mwanzoni mwa utawala wangu, nafurahi kuipongeza Jamhuri (ya Muungano wa Tanzania) kwa uwezo wa Mungu na kuomba wananchi wawe na amani na ustawi,” alisema Papa Francis katika ujumbe wake.
Rais wa Marekani, Barack Obama, katika salamu zake alisisitiza kwamba nchi yake itaendelea kuwa rafiki na mbia wa Tanzania, ikizingatiwa kwamba nchi hizo zina maono sawa ya kidemokrasia, uchumi na amani.
Malkia wa Uholanzi, Beatrix pia alimtakia Rais Kikwete na wananchi amani na ustawi. 
Wengine waliotuma salamu wakisisitiza kuimarisha ushirikiano na Tanzania, ni Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Dk Nkosazana Zuma,  aliyeahidi kuendelea kufanya kazi na Rais Kikwete, ili kufanikisha malengo ya umoja huo.
Marais wengine waliotuma salamu na nchi zao kwenye mabano ni  Xi Jinping (China), Raul Castro (Cuba),  Pranab Mukherjee (India), Asif Ali Zardari (Pakistan), Mahinda Rajapaksa (Srilanka) na Ukraine kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje,  Leonid Kozhara.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Makame Mzee, alisema wananchi wa Zanzibar walishirikishwa kikamilifu kabla ya kuanza kwa Muungano, ikiwamo kuulizwa na  Mzee Karume, kama wanaukubali mfumo wa Serikali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mzee alisema hayo alipozungumza na gazeti hili katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa jana, kuhusu   maadhimisho ya Muungano, ambayo kilele chake kinafanyika leo katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Akifafanua, Mzee alisema baada ya wazo la kuwapo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais wa kwanza hayati Karume, alipita katika vijiji vya Unguja na Pemba   kuuliza wananchi kama wanautaka Muungano huo.
“Nakumbuka Mzee Karume alikuja kijijini kwetu Mgenihaji, na kuitisha mkutano wa wananchi ambapo waliulizwa kama wanautaka Muungano,” alisema.
Kwa mujibu wa Mzee, Mzee Karume alitumia muda mrefu kuzielezea na kufafanua faida za Muungano ambazo Zanzibar itanufaika nazo, kama itakuwa na Serikali ya Muungano.
Kwa mfano, alisema wananchi wa Zanzibar watakuwa na fursa ya kuishi Tanzania Bara na kufanya biashara zao katika eneo moja lenye idadi kubwa ya watu, na kubwa la ardhi.
“Karume alizieleza faida hizo za kujiunga na Tanzania Bara na kufanya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambazo wananchi walikubaliana nazo moja kwa moja,” alisema.
Alitaja faida zingine, yakiwamo masuala ya ulinzi na kuwa na Jeshi la pamoja la ukombozi, litakalofanya kazi ya kulinda mipaka na bahari ya eneo lote.
Muasisi huyo alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulifikiwa baada ya wananchi wa pande mbili hizo kuwa na uhusiano wa damu, yakiwamo makabila   kutoka Bara kufika Zanzibar kwa muda mrefu.
Mzee alisema hata kabla ya harakati za kupigania uhuru, wananchi wa Bara tayari walikuwa Zanzibar kwa muda mrefu.
Aliwataja kuwa ni Wazaramo, Wandengereko, Wachole kutoka Mafia, Wanyamwezi na Wamakonde.
“Hizo ndizo sababu zilizochangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni wa damu,” alisema Mzee.
Mzee alisema pamoja na Muungano huo kuwa wa damu, bado kuna changamoto zinazoukabili kwa miaka 49 na kusema zinatakiwa kutatuliwa kwa kutumia hekima na busara katika vikao halali.
Hata hivyo, alionya kuwa kero za Muungano kamwe isiwe sababu na kisingizio cha kuwepo kwa chokochoko za kuvunja Muungano, yakiwamo madai ya Serikali ya Mkataba.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Samia Suluhu Hassan, alitoa mwito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi leo katika maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. 
“Kesho (leo)  ni siku muhimu kwa Watanzania kuuenzi na kuudumisha Muungano kwa kuwa umesababisha Tanzania kupata heshima kubwa Afrika na duniani kote,” alisema Samia. 
Alisema pamoja na changamoto zilizopo, Muungano umeendelea kuimarika kwa kuwa wananchi wana imani kubwa nao na Serikali imeendelea kushughulikia kero zake.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item