DEREVA ALIYEACHA BASI NA KWENDA KUSHUHUDIA KUZALIWA MWANAE ATIMULIWA KAZI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/dereva-aliyeacha-basi-na-kwenda.html
KUSHOTO: Shaun Hooley akiwa amembeba mwanae, Jacob Thomas. KULIA: Basi la kampuni ya Tates Travel alilokuwa akiendesha. |
Dereva mmoja wa basi amefukuzwa kazi baada ya kuwa barabarani kwa miaka 17 sababu alitaka kushuhudia mtoto wake wa kwanza wa kiume alipokuwa akizaliwa.
Shaun Hooley, mwenye miaka 38, kutoka Barnsley, South Yorkshire, tayari alikuwa kazini kwa masaa manne ndipo alipopokea simu inayomtaarifu kuwa mpenzi wake Rebecca Asquith amepelekwa leba.
Bila kuchelewa akawapigia simu waajiri wake katika kampuni ya Tates Travel na kuomba watafute dereva wa kumshikia ili aweze kumaliza kazi mapema aende Hospitali ya Barnsley.
Shaun, ambaye alikuwa ameitumikia kampuni hiyo kwa wiki 10, aliendesha basi lake kurudi depo na kuelezwa alikuwa ametimuliwa.
"Ni dhahiri nilitaka kuwepo pale kwa ajili ya kuzaliwa kwa mtoto wangu wa kwanza wa kiume, baba gani asingependa hilo?
"Nilipiga simu kadhaa ofisini kujaribu kupata ufumbuzi wa tatizo hilo. Sikusema nilitaka kuondoka papo hapo. Sikusimamisha basi hilo na kutimka.
"Nilifanya kile nilichofikiri ni wajibu wangu. Nilipiga simu ofisini hapo na kuuliza kama wangeweza kufanya utaratibu wa dereva wa akiba kuchukua njia yangu. Nilisema ningewapigia simu baadaye kuona mipango gani iliyofanyika na kwa wakati huo nikaendelea kuendesha basi hilo.
"Nilipiga simu zaidi lakini sikujibiwa hivyo nikaendesha basi kurejea depo. Nilisubiri hadi niliposhusha abiria wangu na basi lilikuwa tupu kabla ya kurejea depo.
"Sababu ya hilo hakuna sheria yoyote iliyotekelezwa."
"Nilielezwa na bosi wa kampuni hiyo nimejifukuzisha mwenyewe sababu ya uamuzi wangu. Nilikuwa nikitafuta maelewano kidogo, ilikuwa katika dharura na nilitaka kuwa na Rebecca.
"Nimefanya kazi katika kampuni hiyo kwa kipindi kirefu na nimekuwa mchapakazi na sikuwahi kuwaangusha. Nilidhani wangekuwa wenye huruma.
"Nimechukizwa na kufadhaika, unaweza kufikiri kwamba kila mwajiri siku hizi angeweza kutambua kwamba baba wanataka kuwapo pale kushuhudia kuzaliwa kwa watoto wao.
"Nimepoteza kazi yangu lakini niliweza kufika hospitalini kwa wakati na nilikuwapo kushuhudia kuzaliwa kwa mtoto wangu wa kiume Jacob Thomas."
Graham Mallinson, mkurugenzi mkuu wa Tates Travel alisema: "Alikuwa maili 14 kutoka Depo ndipo aliponipigia kusema anataka muda wa mapumziko kuhudhuria kuzaliwa kwa mtoto wake.
"Hiyo ilikuwa takribani masaa manne baada ya kuwa ameanza zamu yake. Tulimweleza tungejaribu kupata dereva wa kumshikia zamu na Saa 3:40 tulimpata mmoja.
"Tulimpigia simu lakini hakujibu. Alirejea depo muda mfupi baada ya Saa 4 asubuhi akiwa na basi tupu na alielezwa kwamba alikuwa amevunja mkataba wake na alikuwa amefukuzwa.
"Alikuwa katika majaribio ya miezi mitatu na endapo angekuwa ametupatia taarifa muafaka kwamba mpenzi wake alikuwa akitarajia kujifungua na alitaka kuwapo wakati wa kujifungua angeweza kuwa alichukua muda wa mapumziko."