SPIKA MAKINDA ABARIKI WABUNGE 6 KUSIMAMISHWA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/spika-makinda-abariki-wabunge-6.html
Spika wa Bunge Anne Makinda amebariki uamuzi wa kuwasimamisha wabunge sita wa Chadema kwa maelezo kuwa kitendo walichofanya ni kudhalilisha Kiti cha Spika.
Ametoa uamuzi huo baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuomba Mwongozo wa Spika kwa maelezo kuwa Naibu Spika, Job Ndugai alikiuka kanuni za Bunge kusimamisha wabunge hao kuhudhuria vikao kwa siku tano.
Kwa uamuzi huo wa Spika, wabunge Tundu Lissu (Singida Magharibi), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Peter Msigwa (Iringa Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiah Wenje (Nyamagana) wataripoti bungeni Alhamisi.
Baada ya uamuzi huo, Mbowe alitoa msimamo wa chama chake, akisema hawatakubali kuongozwa bungeni kidikteta na kwamba uamuzi huo wataukatia rufaa.
Hatua ya wabunge hao kufungiwa ilitokana na Lissu kugoma kukaa chini baada ya kusimama kuomba Mwongozo wa Spika wakati Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora na Mahusiano.
Kile alichokuwa anachangia Nchemba kwa mujibu wa Lissu, ulikuwa ni uongo, hivyo akataka Mwongozo wa Spika, lakini Ndugai alimkatalia kwa maelezo kuwa alikuwa amesimama mara nyingi zaidi kuliko mbunge mwingine yeyote.
Kutokana na uamuzi huo, juzi Mbowe aliomba Mwongozo kwa Spika Makinda, akitaka kufahamu ni lini wabunge hao sita waliopewa adhabu ya kutohudhuria vikao vitano vya Bunge wataruhusiwa kwa sababu kanuni iliyotumika kuwaadhibu haikuwa
sahihi.
Katika Mwongozo wake, Makinda alisema adhabu hiyo ilitokana na Lissu kukaidi agizo la Kiti la kumtaka kukaa chini wakati alipompa nafasi Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga (Chadema) kuzungumza.
Spika alisema wabunge wengine watano walipewa adhabu hiyo kwa kosa la kuzuia wapambe wa Bunge wakati wanatekeleza agizo la Naibu Spika la kutaka kumtoa nje Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani na kusababisha fujo.
“Kanuni zetu na hasa ya 2 (2), na kanuni ya 5(1) ya kanuni za Bunge, imempa mamlaka Spika kufanya uamuzi pasipo na utaratibu wa kanuni.
“Aidha, uamuzi unaofanywa na Spika ambao unaruhusu uendeshaji bora wa shughuli za Bunge ambao unaleta amani na utulivu bungeni, utakaofanywa unaingizwa kwenye kitabu cha uamuzi ili kuongoza mwenendo wa baadaye wa uendeshaji Bunge,” alisema Spika.
Makinda alisema kitendo kilichofanywa na wabunge hao hakiwezi kupuuzwa, kwani dhahiri ni cha kudhalilisha mamlaka ya Spika na cha utovu wa nidhamu wa hali ya juu hali iliyofanya Watanzania walioshuhudia walaani tukio lililokuwa likiendelea ukumbini.
Alisema hata angekuwa mbunge yeyote anaongoza Bunge wakati huo, angetoa uamuzi huo. “Ninatumia kanuni ya 5(1) na ya 2 (2) ya Bunge inayompa mamlaka Spika kufanya uamuzi ambapo jambo ama shughuli yoyote haikuwekewa masharti katika kanuni hizi, uamuzi uliofanywa na Naibu Spika (Ndugai) wa kuwatoa nje wabunge na kubaki nje ya vikao vya Bunge kwa siku tano ni halali.”
Alisema uamuzi huo kuanzia sasa utaingizwa katika kitabu cha uamuzi wa Spika na mbunge yeyote atakayefanya vitendo kama hivyo atapewa adhabu kama hiyo.
Kwa upande wake, Mbowe akizungumza na waandishi wa habari, Mbowe alisema: “Sisi hatutakubali kuishi maisha ya kidikteta ndani na nje ya Bunge.”
Alisema hata siku nyingine ikitolewa hoja ya uongo na wabunge wa CCM, ni lazima Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Lissu ataendelea kusimama hata mara 100 kuomba Mwongozo wa Spika. “Wasipofanya uovu bungeni, Bunge likaendeshwa kwa haki bila upendeleo sisi hatutasimama na kuomba Mwongozo wa Spika.
Alisema kutokana na uamuzi wa Spika kuhalalisha uamuzi wa Ndugai, watakutana Kamati ya Uongozi ya Chadema na kutoa uamuzi kuhusu mambo hayo.
“Tutakutana mara baada ya waliosimamishwa kurejea bungeni, kuzungumza maana tutapenda kusikia pia maelezo ya Lissu,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema watakata rufaa dhidi ya Makinda na Naibu wake, licha ya kutambua kuwa haki haitatendeka dhidi ya rufaa watakayokata. “Lakini ni vema tukaweka kumbukumbu kuwa jambo hili liliwahi kufanyika na tukachukua hatua hizi,” aliongeza.
Alidai kuwa uamuzi wa Spika haukuzingatia kumpa nafasi ya kujitetea Lissu na wenzake, jambo ambalo ni kosa kwa Makinda kuridhia adhabu hiyo. Aliongeza kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 74(3), adhabu hiyo ingepaswa kutolewa na Kamati ya Haki, Kinga na Maadili baada ya kuridhika kuwa mbunge husika alitenda kosa.
Alisema uamuzi wa Makinda ni wa kumlinda Ndugai na kuwa kama wangetumia vifungu vya 74 katika kuamua suala hilo na kama Lissu angepatikana na kosa wangempa adhabu kubwa zaidi ya hiyo.
Kwa mujibu wa kifungu cha 74 (3A na B) “ikiwa ni kosa lake la kwanza, Kamati inaweza kushauri mbunge huyo asihudhurie vikao vya Bunge visivyozidi 10 au ikiwa ni kosa lake la pili au zaidi mbunge atatakiwa asihudhurie vikao vya Bunge visivyozidi 20.”