MACHINGA WANAOINGIZA 40,000/- KWA SIKU SASA KUTOZWA KODI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/machinga-wanaoingiza-40000-kwa-siku.html
Baadhi ya wamachinga wakiwa kazini katika moja ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam. |
Serikali imeanza kuimarisha ukusanyaji mapato yake, kwa kutoza kodi pia wafanyabiashara wadogo wanaotembeza bidhaa zao kwa wateja barabarani, maarufu kama Wamachinga.
Ukusanyaji wa mapato hayo ya Serikali utafanyika kwa wafanyabiashara wakiwamo wa maduka madogo ambao hawajasajiliwa kwenye orodha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), wenye uwezo wa kuuza bidhaa na huduma za Sh 40,000 kwa siku.
Mfumo utakaotumika kukusanya mapato hayo, utahusisha Mashine za Kodi za Kutolea Stakabadhi (EFDs), ambao utaanza na wafanyabishara 200,000 na kuzinduliwa Mei 15 na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya.
Ofisa Mwandamizi Mkuu Elimu wa TRA, Hamisi Lupenja, alisema hayo jana, wakati akitoa mada katika semina ya kodi kwa wafanyabiashara wa hoteli na migahawa, kuhusu mfumo huo mpya.
Kwa mujibu wa Lupenja, wafanyabiashara hao kila mmoja baada ya kuuza bidhaa au huduma, atatakiwa kutoa stakabadhi ya mauzo na taarifa zake zitaonekana TRA.
Lupenja alisema mwisho wa mwezi, mfanyabiashara atakuwa na taarifa za mauzo yake na kodi anayostahili kulipa TRA.
Alisema awali Serikali ilianzisha mfumo wa utoaji stakabadhi kwa kutumia EFDs, Julai mosi 2010, ambao utekelezaji wake ulianza kwa awamu huku awamu ya kwanza ikihusu wafanyabiashara waliosajiliwa VAT.
Alisema katika mfumo huo, hakuna kodi itakayotozwa kwenye ununuzi wa mashine, isipokuwa gharama ya utengenezaji mashine na usafirishaji ndivyo atatozwa mfanyabiashara.
Lupenja alionya, kuwa sheria ya VAT, imeweka wazi kuwa adhabu kwa wasiotumia mashine bila sababu, ni faini ya si chini ya Sh milioni tatu. Aidha, kuna mpango wa kusaka watakaofanya biashara bila vifaa hivyo.
Sheria hiyo pia inaeleza kuwa watakaochezea mashine, ili kukwepa kodi, faini itakuwa mara mbili ya kodi iliyokwepwa au Sh milioni nne pamoja na kodi ambayo haikulipwa.
Kwa watakaojaribu kuchezea mashine na mfumo wake, Ofisa huyo wa TRA alionya kuwa faini itakuwa Sh milioni 10.
Lupenja alitaja aina za mashine hizo kuwa ni Rejesta ya Kodi ya Kielekitroniki, inayotumika kwa wafanyabiashara wa rejareja, wanaotoa stakabadhi kwa maandishi ya mkono na ambao watakuwa wanauza bidhaa kwa kutembeza kwa wateja.
Pili ni Printa ya Kosi ya Kielektroniki ya Kodi, ambayo itatumika kwa wafanyabiashara wa rejareja, ambao wanatumia mtandao wa kompyuta katika utoaji wa stakabadhi na ankara za madai.
Mashine hiyo pia hutumika katika maduka makubwa, vituo vya mafuta na ukataji stakabadhi.
Vituo vya mafuta, vimeandaliwa utaratibu maalumu, wa kufunga kifaa cha kodi ndani ya pampu, ili kuondoa kasoro zilizopo na mahesabu yote yaingie kwenye kifaa hicho.
Aina ya tatu ni Mashine ya Alama za Kodi, ambayo hutumika kwa wafanyabiashara wanaotumia programu maalumu za biashara katika utoaji stakabadhi na ankara za madai.
“Mashine hizi zina uwezo wa kuratibu shughuli za kibiashara katika matandao huo na kuifanya kompyuta kukosa uwezo wa kutunza au kuchapa taarifa yoyote bila idhini ya mashine yenyewe,” alibainisha Lupenja.
Alitaja faida za kutumia mashine hizo, kuwa ni mfanyabiashara kuwa na uhakika wa usalama wa taarifa za biashara ambazo zitatunzwa katika kifaa maalumu.
Taarifa hizo kwa mujibu wa Lupenja, hazifutiki wala haziharibiki kwa kemikali yoyote. Pia zitatumika kutoa haki katika tathmini ya kodi.
Mashine hizo pia haziruhusu kubadili tarehe na stakabadhi zake ni vigumu kughushiwa, hivyo zitapunguza ujanja na wizi, huku ikiwa rahisi kutumia kwa Kiingereza na Kiswahili na nyinginezo.
Lupenja alisema utafiti waliofanya, ulibaini mafanikio katika awamu ya kwanza, ambapo wafanyabiashara walikiri kuwa mfumo huo uko wazi na rahisi kujikadiria wenyewe.
Alisema wafanyabiashara hao, walikiri kuweka kumbukumbu vizuri, kuongeza faida, kupunguza wizi na kuchangia ongezeko la makusanyo ya kodi.
Changamoto walizokabiliana nazo katika awamu ya kwanza, ni pamoja na watumiaji mashine kutotoa stakabadhi na wanunuaji kutodai stakabadhi.
Nyingine ni mafunzo kutofikia wafanyabiashara kwa wingi na kukosekana kwa wasambazaji mikoani. Hata hivyo, Lupenja alisema changamoto hizo walizipatia utatuzi.
Alisema katika kutafuta utatuzi wa changamoto hizo, waliwataka wasambazaji kurekebisha mashine, ili zikidhi mahitaji na wanatarajia kuanzisha bahati nasibu ili kujenga utamaduni wa kudai na kupewa stakabadhi.
Katika bahati nasibu hiyo, kwa mujibu wa Lupenja, takayekusanya stakabadhi nyingi za ununuzi, atapata zawadi mbalimbali kubwa, likiwamo gari ili kujenga utamaduni wa kudai stakabadhi.
Naye, Naibu Kamishna Idara ya Kodi za Ndani wa TRA, Generose Bateyunga, alisema hawana mamlaka ya kupanga bei ya kifaa hicho, lakini waliwaagiza wasambazaji kisizidi Sh 750,000.
Katika awamu ya kwanza ya mfumo huo, Bateyunga alisema walifikia asilimia 93 ya wafanyabiashara hao, ambapo ilisaidia kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali kwa Julai 2010 hadi 2011, ambapo mapato yaliongezeka kwa asilimia 9.6
Bateyunga alisema mwaka 2011 hadi 2012, mapato yaliongezeka kwa asilimia 23, na wanaamini mfumo wa awamu mpya utaongeza zaidi mapato ya Serikali.
Pia alizungumzia utekelezaji wa sheria kwa watakaokiuka matumizi ya mashine hizo na kubainisha kuwa wanaanza kwa kutoa elimu na kuhamasisha.
Alisema watu watakapohamasika, watasaka na kukamata wafanyabiashara watakaokuwa hawana mashine.