NYUMBA ZA VIONGOZI WA CCM ZATEKETEZWA MOTO...

Mbunge wa Liwale, Faith Mitambo.
Nyumba zaidi ya saba za kuishi na nane za maduka pamoja na mifugo; vyote vikimilikiwa na viongozi wa CCM, akiwamo mbunge na madiwani wilayani Liwale, vimeteketezwa kwa moto na kuharibiwa na wahalifu.

Mali hizo zikiwamo za viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ilulu, Liwale, vimeteketezwa kwa kilichdaiwa kuwa ni kupinga kulipwa malipo kidogo ya korosho, msimu wa mwaka jana.
Taarifa ya Polisi, ilisema jana kuwa watu wanaodhaniwa kuwa wakulima wa korosho, walijaribu kuzuia gari lililokuwa na malipo ya korosho, wakipinga malipo ya pili ya zao hilo na kufanya vurugu na uharibifu wa mali.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, alionesha wasiwasi bungeni  akisema huenda kuna baadhi ya watu, wakiwamo wanasiasa walio nyuma ya matukio hayo ili kuficha uovu wao na wengine kujinufaisha kwa maslahi binafsi.
Waliochomewa nyumba katika vurugu hizo, ni Mbunge wa Liwale, Faith Mitambo, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Liwale, Mohammed Mngomambo,  Katibu Mwenezi wa CCM wa Wilaya, Abdallah Chande na Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ilulu, Hamza Mkunguru.
Wengine walioathiriwa na vurugu hizo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Diwani wa CCM, Abas Mtalilo ‘Chigogola’ na madiwani wenzake,  Hassan Myao, Musa Mkoyage, Mzee Salehe na Amina Mnoche.
 Akizungumza na mwandishi jana, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Hemed Ndimane alisema duka lake la vyakula lilivamiwa na mali zote kuporwa. Ng’ombe watano waliouawa kwa kukatwa mapanga, ni mali ya  Mkunguru.
Naye Mitambo alisema nyumba zake mbili zilichomwa moto huku moja ikiteketezwa kabisa, nyingine ikibomolewa paa na kunyofolewa milango na madirisha.
Mbunge huyo alisema Chigogola alichomewa nyumba ya vyumba 11, pikipiki mbili, trekta dogo ‘power tiller’ na ng’ombe wake 12 waliuawa.
Alisema Mngomambo alichomewa nyumba kama alivyofanyiwa Chande; sawa na madiwani wote wa kata za mjini Lindi.
Ingawa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alisema atatoa taarifa baadaye, lakini taarifa ya makao makuu ya Polisi, Dar es Salaam, ilisema mpaka jana watuhumiwa 19 walikuwa wamekamatwa kwa mahojiano. Vurugu hizo zilizoanza juzi asubuhi, eneo la Liwale ‘B’.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Abdallah Ulenga, Kamati ya Ulinzi na Usalama ilikutana jana baada ya tukio hilo huku Kamanda akisisitiza kuwa hadi jana mchana walikuwa wakiendelea na vikao, kabla ya kutoa taarifa kamili kwa vyombo vya habari.
Ulenga alisema wananchi hao walivamia maduka na nyumba za viongozi hao na kuziteketeza kwa moto, kutokana na madai kwamba walipata malipo ya pili ya Sh 200 badala ya Sh 600 kwa kilo.
“Lazima tufahamu ni kwa nini, kama mauzo yalikuwa Sh 1,100 kwa kilo, wataalamu wanatakiwa watoe maelezo juu ya malipo hayo yaliyofanywa Liwale,” alisema Ulenga.
Bei ya korosho kwa kilo ilikubaliwa kuwa Sh 1,200 kwa kilo, lakini baada ya kushuka kwa bei katika soko la dunia, ilishuka na kuwa kati ya Sh 1,000, Sh 1,070 na 1,100.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Lindi, Killian Kapamba alisema hajui kama vurugu hizo ni za ununuzi wa korosho au za kisiasa, kwa kuwa mali za viongozi wa kisiasa ndizo zilizoharibiwa.
Alisema inakuwa vigumu kubaini sababu za vurugu hizo kwa kuwa pia Chama cha Msingi cha Ushirika cha Umoja, ambacho ndicho chenye jukumu la kutoa malipo hayo, kilikuwa hakijaanza kutoa malipo ya pili kwa wakulima na wanachama.
Hata hivyo, taarifa kutoka Polisi zilisema baadhi ya viongozi waliodaiwa kuhusika na uchochezi huo, wamekamatwa.
Akizungumza bungeni jana, Malima alieleza kusikitishwa na vitendo vya wananchi kuchukua hatua mkononi na kuharibu mali bila kutoa fursa ya matatizo yao kushughulikiwa.
Malima ambaye alionesha wasiwasi wa wanasiasa kuwa nyuma ya vurugu hizo, alisema hayo baada ya Mbunge wa Viti Maalumu,  Zainabu Kawawa (CCM), kuliwasilisha suala hilo bungeni.
Zainabu wakati akitoa hoja hiyo, aliitaka Serikali kutengeneza  utaratibu utakaowezesha wakulima hao kulipwa fedha wanazodai, ambazo ni Sh 400 walizopunjwa katika malipo ya korosho.
“Naomba nieleze masikitiko yangu juu ya tukio la jana (juzi) usiku katika wilaya ya Liwale…wakulima wa korosho wameghadhabika na kuamsha mapambano  kati yao na polisi, hadi kusababisha uharibifu wa mali zikiwamo nyumba za viongozi,” alisema Kawawa.
Alisema wakulima hao walichukua hatua hiyo, baada ya kutotimiziwa malipo ya korosho ya Sh 1,200 kwa kilo. Alisema awali walilipwa Sh 600 tu, baadaye wakapewa Sh 200 na hadi sasa hawajamaliziwa Sh 400 zilizobaki.
“Kwa maana hiyo wakulima hao walilipwa Sh 800 tu, wanachodai ni tofauti ya Sh 400, nimezungumza na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika amenieleza kuwa bei ya korosho imekuwa ikibadilikabadilika,” alisema Zainabu.
Aliiomba Serikali iingilie kati mgogoro huo kwa kuahidi kama inaweza kufidia Sh 400, ili mkulima wa korosho alipwe Sh 1,200.
Akijibu hoja hiyo, Malima alisema: “Hii lazima tukubaliane kuwa kuna vitu vimejificha humu, sehemu zote ambazo zinalimwa korosho ikiwamo Mkuranga, kuna matatizo ambayo yanasababisha korosho kutouzwa na matatizo haya hayalingani kote, yanatofautiana,” alisema.
Alisema kwingine matatizo ya wakulima wa korosho yanatokana na vyama vya ushirika wakati kwingine kuna matatizo ya wanunuzi.
“Sasa mimi nashangaa kwa nini vurugu za namna hii zinaibuka? Kuna sababu nyingi, pengine hata hawa viongozi wa ushirika wanahusika ili kuficha maovu yao au hata tu masuala ya kisiasa,” alisema Malima.
Kutokana na vurugu hizo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, ametuma timu maalumu ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Issaya Mngulu, kwenda kuongeza nguvu mkoani humo kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa.
Timu hiyo imetakiwa kuhakikisha hali ya amani na utulivu inarejea haraka na waliohusika na uhalifu, wanakamatwa na kufikishwa mahakamani, ili sheria ichukue mkondo wake.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item