MAELFU WAJITOKEZA KUMZIKA BI KIDUDE LICHA YA MVUA KUBWA...

Waumini wa dini ya Kiislamu wakibeba Jeneza lenye mwili wa Marehemu Fatma Baraka 'Bi Kidude', wakati wakiingiza jeneza hilo Msikiti wa Mwembeshauri, kwa ajili ya kuswaliwa kabla ya kuelekea kijijini kwa marehemu, Kitumba Wilaya ya Kati kwa maziko, mchana huu.
Sehemu ya umatiwa waliohudhuria wakinyeshewa na mvua wakati wa mazishi hayo.
Maelfu wamzika Bi Kidude licha ya mvua kubwa
Maelfu ya wananchi wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, walihudhuria katika maziko ya msanii gwiji na mkongwe nchini, Fatuma Binti Baraka Hamis ‘Bi Kidude’ yaliyofanyika nyumbani kwao Kitumba Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja jana.

Mvua kubwa iliyonyesha wakati wa maziko ya marehemu Bi Kidude, haikuzuia umati mkubwa wa wananchi kushiriki katika safari ya mwisho ya msanii huyo aliyefariki dunia juzi mchana.
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alimuelezea Kidude kuwa msanii mkongwe aliyefanya kazi kubwa kuitangaza sanaa ya muziki wa taarab na utamaduni wa Mzanzibari ulimwenguni kote.
“Tumepata msiba mkubwa wa kuondokewa na mtu ambaye alikuwa kipenzi cha watu wengi,” alisema Shein na kuongeza kuwa kila nafsi itaonja mauti kwa hivyo watu wanatakiwa kuyakumbuka yale mema yaliyofanywa na msanii huo pamoja na mchango wake kwa jamii na taifa.
Dk Shein alisema hayo wakati alipoitembelea familia ya marehemu na kutoa mkono wa pole eneo la Rahaleo mjini Unguja mapema jana asubuhi.
Ibada ya kuswalia mwili wa marehemu ilifanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa, Mwembe Shauri na kuongozwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Khamis Haji, ambapo msafara mkubwa wa gari ulielekea katika Kijiji cha Kitumba Wilaya ya Kati Unguja kwa maziko.
Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alisema ni msanii mahiri aliyetembea nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kutangaza sanaa ya muziki wa taarab na utamaduni wa Mzanzibari.
“Kwa niaba ya Serikali, natoa mkono wa pole na Serikali itagharimia shughuli zote za mazishi,” alisema.
Viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Rais wa Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal, Balozi Iddi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki.
Aidha, watu mbalimbali wakiwemo wasanii wa muziki wa taarabu walihudhuria mazikoni hapo. Baadhi ya wasanii waliokuwapo katika maziko hayo ni pamoja na Isha Ramadhan ‘Mashauzi’, Nassib Abdul ‘Diamond’, Fatma Issa, Rukia Ramadhan, Fauzia Abdalla na Sada Nassor.
Mmoja ya wawakilishi wa familia ya marehemu Bi Kidude, Haji Ramadhan Suwedi aliipongeza Serikali kwa kushiriki kikamilifu katika maziko hayo huku Serikali ikitambua mchango wa marehemu.
“Tumefurahishwa sana na uamuzi wa Serikali wa kushiriki kikamilifu katika maziko ya mzee wetu kuanzia Rais wa Muungano pamoja na Rais wa Zanzibar,” alisema Suwedi.
Mwishoni mwaka jana, Bi Kidude alikabidhiwa Nishani ya Ushujaa na Rais Kikwete ikiwa ni ishara ya kutambuliwa kwa mchango wake kwa Taifa.
Katika hatua nyingine, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), limepokea kwa masikitiko taarifa za msiba wa msanii nguli wa tasnia ya muziki wa taarab nchini, Fatma Binti Baraka Hamisi ‘Bi Kidude.’
Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza alisema kifo cha msanii huyo ni pigo kubwa katika tasnia ya muziki nchini.
“Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya kifo hiki cha Bi Kidude ambaye mchango wake katika muziki wa taraab ni mkubwa mno na unahitajika sana. Pengo aliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wake bado unahitajika katika tasnia hii,” ilieleza taarifa ya Mngereza.
“Baraza linatoa pole kwa familia ya marehemu na wasanii wote nchini. Tunawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wetu.”

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item