HUKUMU YA KESI YA SHEKHE PONDA YAAHIRISHWA HADI MEI 9...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/hukumu-ya-kesi-ya-shekhe-ponda.html
Askari Magereza akimfungua pingu Shekhe Ponda Issa Ponda mahakamani. |
Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aloyce Katemana, aliahirisha hukumu hiyo kwa kuwa Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo.
Akiahirisha kesi hiyo jana, Hakimu Katemana, alisema amepata taarifa kutoka kwa Hakimu Victoria, kuwa hukumu hiyo itakuwa tayari Mei 9 na kesi hiyo itatajwa Mei 2 mwaka huu.
Aidha alitoa hati ya kukamatwa kwa washitakiwa, Salum Mkwasu na Ally Salehe, pamoja na wadhamini wao, kwa kosa la kutofika mahakamani hapo bila taarifa.
Shekhe Ponda na wenzake wanakabiliwa na mashitaka ya uchochezi, kuingia kwa jinai na kujimilikisha isivyo halali kiwanja cha Chang’ombe Markazi, kinachomilikiwa na Kampuni ya Agritanza na wizi wa mali zenye thamani hiyo.
Jana Shekhe Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa 1:00 asubuhi na kuingia katika chumba cha Mahakama saa 2:45 huku baadhi ya wafuasi waliokuja kusikiliza kesi hiyo, wakizuiwa kuingia mahakamani.
Ulinzi uliimarishwa na askari wakiwa kwenye farasi walizunguka nje ya Mahakama, huku wengine waliovaa mavazi ya kujikinga na vurugu, wakiwa na mbwa wanne walizunguka katika eneo la ndani na kila aliyeingia alikaguliwa kwa mashine maalumu.
Aliondoka mahakamani hapo saa 3:15 akisindikizwa na msafara wa magari saba, likiwemo la maji ya kuwasha, umati wa wafuasi wake waliozuiwa kuingia mahakamani ulianza kupiga kelele wakati Shekhe Ponda akirudishwa rumande.
Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka walikuwa na mashahidi 16 ambao walidai kuwa kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na Bakwata ambao waliamua kubadilishana eneo la ekari 40 za Kampuni ya Agritanza lililopo Kisarawe mkoani Pwani kwa lengo la kujenga Chuo Kikuu cha Waislamu.
Machi 4 mwaka huu, washitakiwa walipatikana na kesi ya kujibu na kuanza kujitetea ambapo walikuwa na mashahidi zaidi ya 50, wakiwemo washitakiwa wenyewe, ambao walikiri kukutwa eneo la tukio na kudai kuwa walikwenda kwa ajili ya ibada ya Itikafu ambayo hufanyika saa 9 usiku.