MAMA MTAALAMU WA MAABARA AUA BINTI ZAKE WAWILI KWA KEMIKALI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/mama-mtaalamu-wa-maabara-aua-binti-zake.html
Heena akiwa na binti zake wawili, Jasmine (kushoto) na Prisha. |
Mtaalamu wa maabara anadaiwa kuwaua mabinti zake wawili wadogo kwa kutumia mchanganyiko wa sumu kabla ya kujiua katika msiba wa vifo vitatu.
Mama huyo, aliyefahamika eneo hilo kama Heena Solanki, imefahamika kuwa kwanza aliwaua mabinti zake wawili Jasmine, mwenye miaka tisa, na Prisha, mwenye miaka minne, na kisha yeye mwenyewe katika nyumba yao nadhifu.
Baba wa watoto hao anaaminika kuwa ndiye aliyegundua miili hiyo mitatu.
Muda mfupi baada ya madaktari na polisi kuwasili, majirani walisema walifunga milango yao yote na madirisha, wakisema kwamba kulikuwa na 'kadhia ya kemikali' kwenye nyumba hiyo.
Jana wapelelezi kutoka Kikosi cha kushughulikia Mauaji na Uhalifu Mkubwa cha Makao Makuu ya Polisi walikuwa wakichunguza nyumba hiyo yenye vyumba vitano vya kulala.
Msemaji wa polisi alisema wapelelezi hawakuwa wakimtafuta yeyote mwingine kuhusiana na vifo hivyo, ambavyo walisema vilikuwa vikichukuliwa kama 'visivyoelezeka.'
Jana madirisha mengi ya nyumba yalikuwa wazi kwa ajili ya kuruhusu hewa kuingia licha ya mvua na joto dogo. Nyumba hiyo ya thamani ya Pauni za Uingereza 600,000 imebaki ikiwa imewekewa vizuizi.
Turubai la polisi limewekwa kwenye njia ya kuingilia na maeneo ya uhalifu maofisa walionekana wakiwa wamebeba mifuko iliyojaa ushahidi kutoka kwenye jengo hilo.
Majirani walisema Heena alikuwa akifanya kazi kama mtaalamu wa maabara na alikuwa ameolewa na Kalpesh, mwenye miaka 42.
Kwenye ukurasa wake wa Facebook, alieleza kwamba alisoma katika Chuo Kikuu cha Gujarat ya Kusini hadi mwaka 2002.
Jirani mmoja mzee ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema: "Usiku wa jana polisi hao walikuwa wakigonga milangoni wakimweleza kila mmoja kuingia ndani na kufunga madirisha yao sababu kulikuwa na kadhia ya kemikali.
"Kulikuwa na magari ya zimamoto na magari ya wagonjwa na hata polisi.
"Walikuwa hapo hadi saa za mapema," alisema.
"Walikuwa familia yenye upendo. Watoto hao walikuwa wakikimbia huku na kule na kucheza nje, wakati wote wakiwa na furaha mno.
"Mke wangu amesikitishwa mno. Inauma sana. Walikuwa watoto wenye upendo. Mama huyo alikuwa akifanya kazi katika maabara."
Mwanamke mmoja anayeishi jirani na hapo, ambaye hakutaka kuandikwa jina, alisema: "Walikuwa familia yenye upendo na watoto walilelewa vizuri mno. Kila mara walifanya jitihada za kukusalimu. Hakika ni huzuni kubwa."
Miili hiyo ya mwanamke na watoto hao wawili ilichukuliwa mapema jana kwenye gari binafsi la wagonjwa.
Msemaji wa polisi alisema kwamba uchunguzi wa miili hiyo kubaini sababu za vifo unatarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Msemaji huyo wa polisi alisema kwamba jamaa wa karibu wa familia hiyo wameshataarifiwa kuhusu msiba huo.