RUSHWA, UZEMBE VYAITAFUNA TANESCO...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/rushwa-uzembe-vyaitafuna-tanesco.html
Moja ya miundombinu ya umeme inayomilikiwa na Tanesco. |
Wakati watendaji wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), wakilalamika kuwa shirika lina hali mbaya ya kifedha, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameonesha rushwa na uzembe, ndio chanzo cha kulikosesha shirika hilo mapato.
CAG katika ripoti yake maalumu, katika eneo la wizi wa umeme, ameonesha kuwa Tanesco haina mifumo inayoaminika na kuthibitika, kwa ufasaha na ufanisi wa kuhakikisha uhalisia na usahihi wa ukusanyaji mapato yake yote kwa mwaka.
Ripoti hiyo ya ukaguzi maalumu wa awamu ya pili iliyotolewa hivi karibuni, inaeleza kuwa bado Tanesco haiwezi kudhibiti mapato yake, yatokanayo na mauzo ya umeme kupitia vituo vya mawakala wa Luku, ambao wametapakaa sehemu mbalimbali nchini.
Pia, Tanesco imetajwa kufanya usuluhishi na uoanishi wa mauzo ya wakala wa mauzo ya Luku na kumbukumbu za Tanesco, bila kutumia mifumo ya kompyuta, jambo ambalo CAG ameeleza kuwa huwa na makosa mengi na urahisi wa kughushi.
Alitoa mfano kuwa Tanesco, haina kumbukumbu inayoonesha ni idadi gani ya umeme uliotolewa kwa wauzaji wa umeme na kiasi kilichokusanywa na shirika.
Uzembe mwingine ulioneshwa na CAG kuhusu Tanesco, ni shirika kutokuwa na kumbukumbu za kuaminika na taarifa sahihi za mita za umeme zinazotumika, na mashine za kuuzia umeme zilizowekwa nchi nzima.
Hali hiyo imetajwa na CAG kuwa imedhihirisha kuwepo kwa ukiukwaji wa usimamizi wa mifumo ya fedha, kanuni na mifumo ya udhibiti wa ndani.
Katika eneo la rushwa, CAG katika ripoti hiyo ameonesha kuwa shirika hilo limegubikwa na ukiukwaji uliokithiri wa kutozingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005, uliosababishwa na viongozi wa juu na kati wa shirika.
“Mkurugenzi Mkuu akiwa mwenye uamuzi wa juu wa ununuzi, alishindwa kuzuia ukiukwaji wa utaratibu wa Sheria ya Manunuzi na mara nyingi Mkurugenzi Mkuu aliidhinisha ununuzi kutoka chanzo kimoja au ununuzi uliozuia ushindani,” inaeleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imeeleza Tanesco imeingia mikataba na kampuni mbili za uwakili, zikiiwakilisha kwenye kesi kubwa za kimataifa na kesi nyingine, ambazo kwa ujumla zinaigharimu Tanesco zaidi ya Sh bilioni 10 kila mwaka.
Kampuni hizo za uwakili ambazo CAG hakuzitaja, zilipewa kazi na Tanesco bila kufuata utaratibu wa Sheria ya Manunuzi. Pia, inaonekana wazi kwamba malipo ya ada za huduma hiyo ya kisheria ni makubwa na hayana uhalisia.
Lakini kibaya zaidi ni kwamba, Menejimenti ya Shirika imeelezwa kwamba haikuweza kubainisha thamani ya fedha, iliyopatikana kutokana na huduma hiyo ya uwakili.
Awamu ya pili ya ukaguzi maalumu ndani ya Tanesco, ilikuwa kwa ajili ya kuangalia ununuzi usiofuata utaratibu wa ununuzi wa umma, uchunguzi wa rushwa, wizi wa umeme, maswala yanayohusu ajira, ununuzi na uuzaji wa mali za shirika, mgawo wa umeme na malipo yaliyofanyika kwa mawakili.
Katika awamu ya kwanza ya ukaguzi maalumu ndani ya shirika hilo, CAG alionesha madudu yaliyokuwa yanafanywa na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, William Mhando ikiwemo namna alivyoipatia zabuni Kampuni ya Santa Clara Supplies Ltd ya thamani ya mabilioni ya Shilingi, ambayo inamilikiwa na mke wake.