MEJA JENERALI MAKAME RASHID KUSOMEWA DUA KARIMJEE LEO...

Maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakiweka jeneza lenye mwili wa Meja Jenerali mstaafu Makame Rashid, katika eneo maalumu lililotengenezwa kwa ajili ya kumuaga jana katika viwanja vya makao makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mlalakua Dar es Salaam. (Picha ya Ofisi ya Makamu wa Rais).
Baada ya kuagwa rasmi kijeshi jana, leo marehemu Meja Jenerali mstaafu Makame Rashid anatarajiwa kusomewa dua na familia yake katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.

Shughuli ya kumuaga kijeshi iliongozwa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal katika viwanja vya makao makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlalakua, Dar es Salaam.
Pamoja na Makamu wa Rais, pia marais wastaafu wa Awamu za Pili na Tatu, Shehe Ali Hassan Mwinyi  na Benjamin Mkapa walihudhuria sambamba na Mkuu wa zamani wa JWTZ, Jenerali Robert Mboma na Mkuu wa sasa Jenerali Davis Mwamunyange na maofisa waandamizi wa Jeshi hilo.
Wengine walioshiriki ni Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Saidi Mwema na Kamishna Mkuu wa Magereza, John Minja.
Jenerali Makame, aliyejiunga na JKT mwaka 1963 na hatimaye kuwa Mkuu wa JKT wa tano tangu Januari 1989, hadi Oktoba 2001. Alifariki dunia juzi saa 12:30 asubuhi, katika Hospitali ya TMJ Dar es Salaam.
Mwili wa Makame uliwasili katika viwanja vya makao makuu ya JKT saa 7:20 mchana, ukitokea Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, ulikohifadhiwa.
Baada ya kuwasili, ulibebwa kwa heshima na maofisa wa Jeshi walioandaliwa kutoka gari maalumu hadi eneo lililotengwa kwa ajili ya kuagwa.
Akisoma ratiba ya shughuli za maziko, Meja Emmanuel Mluga, alisema Jenerali mstaafu Makame atazikwa kesho katika kijiji cha Mnyawa, Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.
Makame alijiunga na JWTZ Oktoba mosi 1964 na kustaafu Oktoba 22, 2001 akiwa amelitumikia Jeshi kwa miaka 37 na siku 22.
Kuhusu madaraka aliyopata kushika, Meja Mluga alisema ni pamoja na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, mwaka 1983 hadi 1989 na  Mkuu wa JKT, 1989 hadi 2001, alipata pia kuwa Mkuu wa Kambi ya JKT Ruvu.
Pia Balozi wa Tanzania  nchini Malawi kati ya mwaka 2004 na mwaka 2008 na kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, hadi mauti yalipomfika.
Mtoto wa kwanza wa marehemu, Mshamu Makame, alisema leo marehemu Makame ataagwa katika Viwanja vya Karimjee, ili kutoa fursa kwa jamaa na marafiki wengine kumuaga kabla ya kusafirishwa kwenda  Tandahimba kwa maziko.
Jenerali mstaafu Makame ameacha mjane, watoto tisa na wajukuu wanane.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item