SHERIA INAYOMSHITAKI WILFRED LWAKATARE HAIELEZI MAANA YA UGAIDI...

Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA Wilfred Lwakatare akitoka mahakama Kuu Dar es Salaam jana, kuelekea rumande baada kusikilizwa tena kesi yake ya kutuhumiwa kwa kukabiliwa na kesi ya ugaidi dhidi ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Uhariri Abslom Kibanda lilitokea mwezi uliopita.
Wakili wa Serikali katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, amedai kwamba sheria haijaeleza maana ya ugaidi ambao kada huyo wa Chadema anashitakiwa. 

Prudensi Rweyongeza, hata hivyo alifafanua jana kwamba, kuteka nyara ni kosa la ugaidi, hivyo wataangalia ushahidi watakaopata kama utathibitisha kosa hilo kwa Lwakatare, basi ataendelea kushitakiwa kwa sheria hiyo.
Rweyongeza alitoa maelezo hayo mahakamani, mbele ya Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakati akijibu hoja iliyotolewa na Wakili wa Lwakatare, Tundu Lissu, aliyeomba Mahakama ifute mashitaka dhidi ya mteja wake.
Lissu katika maombi yake alidai kuwa Sheria ya Ugaidi inaeleza kuwa mkutano wa kigaidi unahusisha watu zaidi ya watatu ilhali washitakiwa walikuwa wawili. Pia Lissu alidai kuwa kosa la kuteka nyara lipo katika Kanuni ya Adhabu.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Rweyongeza alidai kuwa ombi hilo la Lissu, liliwasilishwa katika muda usio mwafaka, kwa kuwa kesi hiyo iko katika hatua ya upelelezi.
Alidai kuwa kesi ikiwa katika hatua hiyo, mashitaka hayo yanaweza kufanyiwa mabadiliko yoyote, kama kuwashitaki chini ya Kanuni ya Adhabu au kuwaachia huru.
Hivyo, Rweyongeza aliiomba Mahakama, kufuta ombi la  Lwakatare, akitaka Mahakama ifanye marejeo katika mwenendo wa majalada ya kesi mbili za ugaidi, zilizofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kuwa halina msingi kisheria. 
Ombi la Lwakatare, liliwasilishwa na mawakili wake Machi 22, siku chache baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwafutia mashitaka yeye na mshitakiwa mwenzake Ludovick Joseph, kisha kuwakamata na kusomewa upya mashitaka hayo.
Jaji Kaduri aliahirisha kesi hiyo hadi atakapopanga siku nyingine na kuzifahamisha pande zote ili kutoa uamuzi kuhusu utata huo.
Wakitoa hoja, mawakili wa Lwakatare walidai kuwa kitendo cha DPP kufuta mashitaka na kuyafungua upya ni kinyume cha misingi ya sheria inayomwongoza.
Wakili Peter Kibatala alidai kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo, DPP alitakiwa kufuta mashitaka kwa haja ya kulinda haki, kuzuia matumizi mabaya ya mfumo wa Mahakama, maslahi ya umma na kudhibiti mashitaka lakini aliwasilisha hati hiyo kwa nia mbaya.
Akijibu hoja hizo, Wakili Rweyongeza, alidai kuwa DPP aliwasilisha hati ya kufuta mashitaka dhidi ya washitakiwa kwa kufuata sheria na kulinda haki.
Alidai kuwa DPP alifuta mashitaka ya awali, kwa kuwa kesi hiyo namba 37 ya mwaka huu, ilisajiliwa katika kitabu cha kesi zinazosikilizwa na mahakama za chini hivyo waliifuta na kuisajili upya katika kitabu cha kesi zinazosikilizwa na Mahakama Kuu.
Aidha, alidai kuwa DPP alifuta kesi hiyo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikosea kuruhusu washitakiwa kujibu mashitaka katika kesi ambayo haina mamlaka ya kusikiliza, hivyo kuruhusu kesi hiyo isikilizwe upya itakuwa ni kuendelea kuwa katika makosa hayo.
Washitakiwa wanadaiwa kuwa Desemba 28 mwaka jana katika eneo la King’ong'o, Kimara Stop Over, Kinondoni, Dar es Salaam, walipanga njama za kutenda kosa la kigaidi la kutumia sumu kumdhuru Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky, kumteka nyara na kufanya mkutano wa kuhamasisha vitendo vya ugaidi.
Lwakatare alisomewa mashitaka ya ugaidi na kukana na mawakili wake wakawasilisha ombi la dhamana, uhalali wa mashitaka na upungufu wa kuruhusu washitakiwa kujibu mashitaka; hata hivyo kabla ya uamuzi kutolewa Machi 22 DPP alifuta mashitaka dhidi yao na kuwafungulia upya.
Katika ombi lao, wanataka Mahakama Kuu ifanye marejeo na kuchunguza ili iweze kujiridhisha juu ya usahihi na uhalali wa mwenendo katika kesi namba 37 ya 2013, iliyofutwa na namba sita iliyofunguliwa upya, ifanye marejeo au kutengua hati ya DPP iliyowafutia mashitaka, kabla ya kuwafungulia tena.
Wanaomba Mahakama iamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itoe uamuzi wa ombi la dhamana uliotakiwa kutolewa Machi 20 katika kesi iliyofutwa, pia ifanye marejeo na au kutengua mwenendo wa kesi namba sita, iamuru kuwa utaratibu uliotumika kutoa hati ya kufuta mashitaka dhidi ya washitakiwa, ulikuwa kinyume cha sheria au haukuwa sahihi.
Wakati kesi ya Lwakatare ikiendelea, wilayani Igunga, Tabora, mkazi wa wilaya hiyo, Evodius Justian (30), alipandishwa kizimbani, akidaiwa kummwagia tindikali aliyekuwa mfuasi wa CCM katika uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011, Mussa Tesha. 
Justian alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ajali Milanzi.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Cosmas Mboya, alidai kwamba Justian alimmwagia tindikali  Tesha na kumjeruhi Septemba 9, 2011,  saa tano usiku katika kitongoji cha Mwayunge mjini Igunga. Justian alikana mashitaka hayo. 
Upande wa mashitaka uliomba mshitakiwa asipewe dhamana kwa sababu washitakiwa wengine bado hawajakamatwa, kwa hofu kwamba akipewa dhamana, anaweza kusababisha washitakiwa wengine kujificha. 
Pia ilielezwa mahakamani hapo, kuwa ndugu wa aliyemwagiwa tindikali wapo karibu na wanaweza kusababisha madhara kwa mshitakiwa.  
Mahakama ilikubaliana na maombi hayo, ambapo mshitakiwa alirudishwa rumande na shauri hilo liliahirishwa hadi Aprili 29 litakapotajwa.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item