NAIBU SPIKA ATETEA MAWAZIRI KUHUSU UTORO BUNGENI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/naibu-spika-atetea-mawaziri-kuhusu.html
Job Ndugai. |
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema mawaziri wanapokosekana ndani ya Bunge, haimaanishi hawako Dodoma, ila hawaonekani kwa kuwa kila mmoja anajitahidi kuweka mambo yake sawa katika mkutano huo wa Bajeti.
Ndugai alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akijibu Mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM) ambaye aliomba mjadala wa Bajeti ya Kilimo, Chakula na Ushirika, usitishwe.
Lugora alitoa ombi hilo, kutokana na idadi ndogo ya mawaziri na naibu mawaziri waliokuwa bungeni, wakati sekta hiyo ilipokuwa ikijadiliwa akisema ni mtambuka na imeajiri Watanzania wengi.
Kwa mujibu wa Lugora, wakati mjadala huo ukiendelea ndani ya kikao hicho cha 11 katika Mkutano wa Bunge la 11 unaoendelea, kulikuwa na mawaziri watano na manaibu watano pia.
Mbunge huyo, alisema bajeti inayojadiliwa ya kilimo ni muhimu na inahusu maendeleo ya Watanzania hasa ikizingatiwa kuwa ajira kubwa nchini ni kilimo, lakini cha kushangaza idadi ya mawaziri na manaibu waliokuwa bungeni wakati huo haikuwa inaridhisha.
“Leo tunajadili hapa bajeti muhimu kabisa … naomba Mwongozo wako pamoja na umuhimu wa bajeti hii, mawaziri ninaowaona humu ndani ni watano na naibu mawaziri watano tu. Katika mazingira ya namna hii tunapeleka ujumbe gani kwa Watanzania?” Alihoji Lugora.
Alisema sekta ya kilimo ni muhimu kutokana na ukweli kuwa Watanzania wengi ndio ajira yao kuu. “Je ni sahihi kuendelea kujadili kwa hali kama hii? Naomba Mwongozo wako,” alisema.
Kwa mujibu wa mtandao wa Serikali wa www.tanzania.go.tz kwa takwimu za mwaka 1999, Watanzania milioni 16,006,178, ndio wenye uwezo wa kufanya kazi.
Aidha, asilimia 82 ya watu hao wenye uwezo wa kufanya kazi, wamejiajiri katika sekta ya kilimo na wengi wao wanalima mashamba madogo wanayomiliki au ya familia.
Mawaziri waliokuwa ndani ya Bunge wakati huo, ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Wengine ni Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji
Ofisi ya Rais, Dk Mary Nagu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani na Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Christopher Chiza.
Naibu mawaziri ni wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, wa Fedha, Janet Mbene na Saada Salim Mkuya, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele.
Wengine waliokuwa kwenye kikao hicho ni Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima.
Baraza la Mawaziri lina jumla ya mawaziri 55, mawaziri wakiwa 30 na manaibu 25, hivyo idadi ilionesha kuwa mawaziri na naibu mawaziri ambao hawakuwa kwenye kikao hicho ni 45.
Baada ya kuombwa Mwongozo, Ndugai aliahidi kutoa majibu baadaye, na kabla ya kuahirisha kikao hicho, alikiri kuwa mawaziri wengi hawapo kutokana na majukumu waliyonayo.
“Naomba niwahakikishie kuwa pamoja na kwamba mawaziri wengi hawapo humu ndani, lakini wapo Dodoma, kila mmoja anajitahidi kuweka mambo yake sawa na kama mnavyoelewa mkutano wetu huu ni wa bajeti,” alisema Ndugai.
Alisema kutokuwapo kwa mawaziri hao bungeni si ajabu huku akitolea mfano mabadiliko yanayoendelea nchini Kenya ambako kwa sasa kuna mabunge mawili, ambayo ni Bunge la kawaida na Bunge la Seneti.
Alisema katika Bunge la kawaida, hakuna waziri anayehudhuria vikao kwa kuwa mawaziri si wabunge hivyo huishia kwenye Kamati za Bunge tu na kulifanya Bunge la nchi hiyo kutokuwa na kipindi cha maswali na majibu.
“Wenzetu hata muundo wao wa uongozi ndani ya Bunge ni tofauti, wakati sisi Kiongozi wa Serikali ndani ya Bunge ni Waziri Mkuu wao wana kiongozi ambaye anatokana na chama chenye wabunge wengi huku nafasi ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, wao wamempa mtu kiongozi wa kundi lenye wabunge wachache,” alisema.
Pamoja na Ndugai kutoa maelezo kuwa wanahangaikia bajeti zao, baada ya Lugora kuomba Mwongozo huo na kuambiwa atajibiwa baadaye, baadhi ya mawaziri na manaibu waliokuwa nje ya ukumbi wa Bunge, waliingia.
Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka.
Naibu mawaziri walioingia ni pamoja na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene; Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu; Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima na Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge.