MADAKTARI WALIOGOMA WAFUTIWA USAJILI WAO...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/madaktari-waliogoma-wafutiwa-usajili-wao.html
Baadhi ya madaktari na wauguzi wakati wa mgomo. |
Madaktari 20 waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo ambao walishiriki mgomo mwaka jana, wamefutiwa usajili kutokana na agizo la Baraza la Madaktari Tanganyika.
Kutokana na hatua hiyo, madaktari hao waliosomea taaluma yao kwa miaka mitano na kuanza mafunzo kwa vitendo, sasa hawataruhusiwa kufanya kazi ya udaktari popote nchini.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dk Donan Mbando, ilieleza kuwa madaktari hao 20, wamechukuliwa hatua hiyo, baada ya kushindwa kuitika mwito wa kwenda kujibu tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.
Katika taarifa hiyo, Dk Mbando alifafanua, kwamba madaktari hao na wenzao waliokuwa wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali yaliyotokana na mgomo huo, waliitwa kujibu mashitaka yao.
Kabla ya kuitwa kwa mujibu wa Dk Mbando, Desemba 15, mwaka jana Baraza lilikabidhi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, taarifa ya kukamilika kwa uchunguzi dhidi ya madaktari walioshiriki mgomo huo Juni mwaka jana.
Dk Mbando alisema, baada ya kukabidhi taarifa hiyo ya uchunguzi serikalini, waliwaita madaktari mbele ya Baraza mwaka jana, lakini madaktari hao pamoja na wenzao watano hawakufika.
“Baraza lilitoa fursa nyingine kwa madaktari wote 25 ambao hawakusikilizwa katika kikao cha Desemba mwaka jana, kufika katika kikao kilichofanyika Aprili 9 hadi 11 mwaka huu Dar es Salaam.
“Licha ya Msajili, kutoa mwito wa kufika mbele ya Baraza, madaktari 20 hawakutokea kwa mara nyingine kujibu mashitaka yanayowakabili, hivyo Baraza lilimwagiza Msajili kufuta majina yao katika Daftari la Usajili wa muda kuanzia Aprili 12,” ilieleza taarifa hiyo.
Katika ufafanuzi wa utendaji kazi wa Baraza hilo ambalo hukaa kwa kufuata utaratibu wa Mahakama, kwa kawaida masuala yote ya mawasiliano ikiwamo kuwaita washitakiwa na hata kuwafutia usajili, hufanywa na Msajili.
Madaktari waliofutiwa usajili ni Lilian Komba, Emmanuel Luchagula, Nerbert Benjamin, Ahmed Kombo, Moses Karashani, Deo Mwanakulya, Lucy Laurent, Elias Paschal, Ahmed Ahmed na Malaja Ng’wigulu.
Wengine ni Malaba Raphael, Biswaro Malima, Said Ibrahim, Peter Kyabaroti, Mamelita Basike, Veronica Lyandala, Meshack ole Sabaya, Musyangi Tekele, Kasirye Collins na Baraka Yessaya.
Akizungumza na mwandishi jana, Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Primus Saidia, alisema wamesikitishwa kupata taarifa za wenzao kufutiwa usajili kupitia magazeti.
Dk Saidia alisema kwa kawaida Baraza lilitakiwa kutoa taarifa MAT, kwa kuwa hata katika kikao cha kwanza, chama hicho cha madaktari kiliarifiwa na kutumia mtandao wake kuarifu washitakiwa.
Alisema kikao cha pili cha Baraza kilipoitishwa, MAT haikupewa taarifa na kuongeza kuwa huenda habari hazikuwafikia madaktari hao, ndio maana hawakufika.
Akiwatetea waliofutiwa usajili, Dk Saidia alisema baada ya mgomo na kusimamishwa kazi, baadhi yao waliorejea vijijini na wengine walisafiri nje ya nchi.
“Hivyo si haki kutoa hukumu kwa mtu ambaye hujakutana naye na kusikiliza utetezi wake, mimi binafsi nimesikitishwa na uamuzi huo na nitaitisha kikao cha Halmashauri yetu ili kutoa uamuzi,” alisema.
Dk Saidia alishauri Baraza kuepuka uamuzi unaoweza kusababisha migongano baina ya wanataaluma, kwa maelezo kwamba njia waliyotumia si sahihi na wajue kuwa katika migogoro hiyo, wanaoumia ni watu wasio na hatia ambao ni wagonjwa.
Alisema uamuzi kama huo kwa nchi yenye upungufu wa wataalamu, si sahihi na jambo la msingi wangewasiliana nao na kumaliza tatizo.
Rais huyo alisema Baraza lingewafikishia wao taarifa ya kuwaita tena Aprili 9 hadi 11, wangetafuta namna ya mawasiliano, kwani wana mawasiliano ya wanachama wao wote hata kupitia mitandao yao ya kijamii.
Alisema walipowaita awali, hawakupata taarifa ya waliofika na ambao hawakufika na kama wangepata taarifa hizo, wangetafuta njia yoyote kuhakikisha wote wamefika.
Kiini cha mgomo huo, kilikuwa maslahi makubwa waliyoyadai ambayo Serikali ilieleza kuwa haina uwezo wa kuwalipa. Madaktari hao walitaka walipwe mshahara wa Sh milioni 3.5 kwa mwezi kwa daktari anayeanza kazi kutoka chuoni.
Pia walitaka posho za kila mwezi ikiwamo asilimia 10 ya mshahara huo kwa ajili ya posho ya kuitwa kazini ambayo ni Sh 350,000 na asilimia 30 ya mshahara huo iwe posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi, ambayo ni Sh 1,050,000.
Posho nyingine walizodai katika mlolongo huo wa maslahi ni kupewa nyumba daraja A au asilimia 30 ya mshahara iwe posho ya makazi ambayo ni Sh 1,050,000, posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu ambayo ni asilimia 40 ya mshahara huo sawa na Sh milioni 1.4.
Madaktari hao pia walitaka posho ya usafiri asilimia 10 ya mshahara huo sawa na Sh 350,000 ambapo posho na mshahara kwa pamoja kwa mujibu wa madai hayo, daktari katika kima cha chini, alipaswa kulipwa Sh milioni 7.7 kwa mwezi.
Madai mengine ambayo hawakuyaweka katika kiwango cha fedha ni pamoja na kupewa kadi ya kijani ya Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Serikali ilikubali suala la usafiri na kuwataka madaktari watumie fursa ya utaratibu uliopo, ili wakopeshwe magari, pikipiki, samani na matengenezo ya magari.
Pia ilikubalika kwamba utekelezaji utaanza kwa kuwapa madaktari kadi ya kijani ya NHIF na katika hatua za kinidhamu, dhidi ya watendaji wakuu wa Wizara, uongozi wa juu wa Wizara ulibadilishwa na sasa kuna uongozi mpya.
Hata hivyo, pamoja na Serikali kubadilisha uongozi huo, Waziri mpya wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alipowataka madaktari hao waonane kuzungumzia hoja zao, walikataa kumwona kwa madai kuwa hawaoni sababu kwa vile wamezungumza na Kamati yake kwa miezi mitatu bila mafanikio.