NDEGE YA BILIONEA WA ARUSHA YAANGUKA, YAMUUA "BABU SEMBEKE"...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/ndege-ya-bilionea-wa-arusha-yaanguka.html
Hii ndio ajali ya ndege iliyochukua uhai wa "Babu Sembeke". |
Mfanyabiashara mashuhuri mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Peter Joseph (49), maarufu ‘Babu Sembeke’, amefariki dunia katika ajali ya ndege.
Sembeke alikuwa rubani katika ndege hiyo aina ya Cessnar, yenye namba za usajili 5H –QTT na alikuwa peke yake ndani ya ndege. Alipata ajali katika eneo la Kisongo, nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na mwandishi, ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiri 4, iliparamia tawi la mti mkubwa uliopo eneo hilo juzi saa 12.40 jioni.
Mashuhuda hao walidai Babu Sembeke alipata ajali hiyo, wakati akiwa katika harakati za kukata kona ili apate mwelekeo mzuri wa kutua katika uwanja wa ndege wa Arusha uliopo Kisongo jijini Arusha.
Walidai baada ya kuparamia mti huo na kupoteza mwelekeo, ndege hiyo ambayo ilinunuliwa kutoka kwa mfanyabiashara mashuhuri wa Arusha, Nyaga Mawalla (38) ambaye alifariki hivi karibuni jijini Nairobi, ndege hiyo ilianguka papo hapo na kusababisha majeraha sehemu za kichwani za Sembeke.
"Sembeke alikufa njiani akipelekwa hospitalini, alikuwa na majeraha makubwa kichwani,’’ alisema mtoa habari.
Sembeke alikuwa akimiliki ndege mbili pamoja na hiyo iliyopata ajali na nyumba za kifahari Arusha, Dar es Salaam na Moshi.