RAILA ODINGA 'AMVAMIA' RAIS UHURU KENYATTA IKULU...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/raila-odinga-rais-uhuru-kenyatta-ikulu.html
Raila Odinga. |
Katika hali ambayo haikutarajiwa kuonekana katika siku za hivi karibuni, Rais mpya wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto, jana walikutana na viongozi wa muungano wa Cord walioshindwa katika uchaguzi mkuu wa Kenya uliofanyika mapema mwezi uliopita, Raila Odinga na aliyekuwa mgombea mwenza wake, Kalonzo Musyoka.
Mkutano huo umefanyika siku nne tangu kuapishwa kwa Kenyatta na Naibu wake, shughuli ambayo Odinga na mgombea mwenza wake hawakushiriki, kwani walikuwa katika mapumziko Afrika Kusini waliokwenda siku chache baada ya kushindwa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliompa ushindi Kenyatta.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu ya Nairobi, viongozi hao walikubaliana kushirikiana kuwaunganisha Wakenya.
Aidha, walijadili mambo kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na uzinduzi rasmi wa shughuli za Bunge la 11 ambalo wabunge wake walipatikana katika uchaguzi mkuu wa Machi 4 mwaka huu. Odinga na Musyoka wameahidi kushiriki.
Kenyatta na Ruto waliahidi kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa vyama vya upinzani, huku Odinga na Musyoka wakitumia fursa hiyo kuwapongeza vijana hao kwa kupata baraka za kuiongoza Kenya, huku wakiahidi kutoa kila aina ya ushirikiano katika kipindi chote watakachokuwa madarakani. Wakati Uhuru ana umri wa miaka 51, Rutto ana miaka 47. Odinga ana miaka 68, na Musyoka ana miaka 59.