BALOZI WA MAREKANI AWATULIZA 'MZUKA' WATANZANIA ZIARA YA OBAMA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/06/balozi-wa-marekani-awatuliza-watanzania.html
![]() |
| Balozi Alfonso Lenhardt. |
Wakati kiongozi wa taifa kubwa duniani, Rais Barack Obama wa Marekani akipanga kuzuru nchini hivi karibuni, Ubalozi wa Marekani umefafanua ziara hiyo haina ajenda yoyote ya siri ya kuchukua rasilimali za Tanzania, bali ni katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt jana alithibitisha ziara hiyo ya Rais Obama.
Alisema "kuna maswali mengi anaulizwa kwa nini Rais Obama amechagua kuzuru Tanzania? Ni kweli Rais wetu anakuja malengo ya ziara yake yatajikita katika mambo ambayo ni malengo ya Marekani kwa Afrika, ambayo ni uhusiano wa kiuchumi, kuimarisha demokrasia na kuwekeza katika kujenga kizazi kijacho cha uongozi".
Tanzania ni nchi pekee kati ya nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo Obama amechagua kufanya ziara yake ya kikazi. Nchi zingine atakazozuru ni Senegal na Afrika Kusini. Ataanza ziara ya kutembelea nchi hizo tatu Juni 26 hadi Julai 2 mwaka huu.
"Ni kweli Obama atakuja Tanzania. Lakini niwahakikishie tu kuwa haji kupora rasilimali za Tanzania, kwani Marekani ina rasilimali nyingi zinazojitosheleza," alisema Lenhardt wakati akijibu moja ya maswali ya waandishi wa habari ambao walitaka kujua kiini cha ziara hiyo.
"Hatuna ajenda ya siri juu ya ziara hiyo. Ila kampuni za Marekani zimekubali kuja nchini kwa ajili ya kuangalia fursa za kuwekeza na lazima zitafuata taratibu zote," alisema.
Alisema lengo kubwa la ziara hiyo ni kupata fursa ya kujadiliana na viongozi wa kiserikali na wadau wengine juu ya masuala ya kuimarisha uchumi, biashara, fursa za uwekezaji na suala la kuimarisha demokrasia nchini.
Lenhardt alisema akiwa nchini, Obama atakutana na viongozi wa Serikali, wafanyabiashara na asasi zisizo kuwa za kiserikali ambazo ni muhimu katika ustawi wa nchi hasa katika maeneo ya demokrasia na uimarishaji wa uchumi.
Pamoja na kutangaza ujio wa Rais wake, Balozi huyo alikiri kuwa hakuwa anajua hasa tarehe ambayo kiongozi huyo atatua Tanzania na kipindi ambacho atakaa nchini.
Katika safari yake, Obama atatua nchini akiwa amefuatana na mkewe, Michele na watoto wake wawili, Sasha na Malia.
"Tunaweza tusitoe taarifa za kina juu ya ziara hii, kwani mambo yote yanaratibiwa na Ikulu ya Marekani, lakini niseme kwamba sisi tunahitaji kuwa na marafiki na Tanzania ni rafiki yetu na sio suala la kuchukua rasilimali zenu ," alisisitiza Balozi huyo.
Katika kusisitiza mtazamo wa Marekani kwa Tanzania, Balozi alisema malengo ya viongozi wa Marekani ni kutaka Wamarekani wafike Tanzania ; na ndio maana wamekuwa wanatoa misaada mbalimbali inayofikia dola za Marekani milioni 750 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.
