HATIMAYE MBOWE NA LEMA WAJISALIMISHA POLISI, WATOA MAELEZO...

Freeman Mbowe (kushoto) na Godbless Lema.
Baada ya utata wa siku kadhaa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) wamejisalimisha Polisi na kutoa maelezo yao.
Viongozi hao waliwasili jana saa 3 asubuhi na kuhojiwa  hadi saa 7.45 mchana na walipotoka nje  wakiwa na mawakili wao; Albert Msando na James Millya, Mbowe alisisitiza kuwa hawako tayari kutoa ushahidi Polisi kwa sababu polisi ndio watuhumiwa namba moja ila wako tayari kuutoa kwa Rais Jakaya Kikwete endapo ataunda tume huru ya majaji.
Alisema watatoa ushahidi juu ya tukio zima la ulipuaji wa bomu katika viwanja vya Soweto uliosababisha vifo vya watu wanne.
Alisema ushahidi huo ni wa mikanda ya video, picha za mnato binadamu ambao hakutaja ni wangapi na ni akina nani ambao alisema walishuhudia tukio zima lilivyotokea na mtu/kundi lililofanya tukio  hilo ambalo aliliita la kigaidi.
Alisema pia kitendo cha polisi kudai walifanya mkusanyiko usio halali hakubaliani nacho na hata kwenye maelezo aliyoyatoa Polisi alisema Jeshi hilo ndilo lilitoa kibali cha kufanyika mazishi hayo. 
Mbowe alipomaliza kuzungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi za Polisi aliondoka akifuatana na Lema na viongozi wa chama hicho kwenda kwenye maziko ya Judith Moshi (44) ambaye alikuwa Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) wa Kata ya Sokon One.
Walishiriki ibada ya mazishi ya kiongozi huyo iliyofanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Sokoni mtaa wa Sokon One.
Akiongoza ibada hiyo, Mwinjilisti, Ezekiel Kisiri akiongozwa na Mkuu wa Jimbo, Solomon Masangwa aliiomba Polisi kutotumia nguvu bila sababu na kufanya baadhi ya watu kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu kwenye viungo.
Kisiri pia alisihi viongozi wa vyama vya siasa na Serikali kutatua kero za wananchi na kutoa majibu ya kuridhisha. Alisema amani iliyopo ni vema ikatunzwa na vyombo vya ulinzi na usalama, wananchi na watu wote.  
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema maelezo ya Mbowe na Lema Polisi ni tofauti na maelezo waliyotoa nje wakati wakizungumza na waandishi wa habari.
Sabas alipoulizwa kama Mbowe na Lema wakati walipojisalimisha na kutoa maelezo yao na walikataa kutoa ushahidi wa tukio hilo wanawachukulia hatua gani aliongeza kuwa hivi sasa Polisi inaangalia sheria inasema nini juu ya suala hilo.
Juzi wabunge wanne wa chama hicho, Tundu Lissu,  Mustafa Akunai, Said Arfi na Joyce Nkya na wafuasi wao 67 walikamatwa na Polisi eneo la Soweto kwa kufanya mkutano usio halali lakini hawakufikishwa mahakamani bali walijidhamini wenyewe na baadhi ndugu zao.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item