IDDI SIMBA NA WENZAKE WAACHIWA HURU KESI YA KUFUJA MABILIONI UDA...

https://roztoday.blogspot.com/2013/06/iddi-simba-na-wenzake-waachiwa-huru.html
![]() |
Iddi Simba. |
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru vigogo wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh bilioni 8.4.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta aliwaachia huru washitakiwa hao jana baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kufuta mashitaka dhidi yao.
Washitakiwa hao wanadaiwa kulisababishia shirika hilo hasara kwa kuuza hisa zake milioni 7.8 kwa Kampuni ya Simon Group, bila kufuata utaratibu wa mchakato wa zabuni.
Awali Wakili wa Serikali Awamu Mbagwa, alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kusikilizwa lakini DPP aliwasilisha hati ya kuondoa shauri hilo mahakamani bila kutaja sababu za kufanya hivyo.
Upande wa utetezi haukuwa na pingamizi na ombi hilo, lakini walitaka kujua sababu za DPP kufuta kesi hiyo kwa kuwa hiyo ni mara ya pili, hivyo waliomba kinga kwa washitakiwa ili wasije wakakamatwa tena na Mahakama iangalie utu wao na kuwalinda.
ÒHatuna pingamizi, lakini ni vema waeleze sababu ya kuondoa shauri hili kwa sababu inawezekana wakakamatwa tena kama walivyowaachia na kuwakamata mara ya kwanza, hivyo hatuwezi kusema mashitaka yameondolewa na wao wako salama,Ó alidai Wakili Mpare Mpoki.
Hata hivyo, Hakimu Mugeta alisema amefuta mashitaka na kuwaachia huru hata kama DPP hajatoa sababu za kuondoa shauri hilo mahakamani.
Washitakiwa walioachiwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo, Iddi Simba ambaye alipata kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mkurugenzi wa Bodi ya Shirika hilo, Salim MwakingÕinda, Meneja Mkuu wa Shirika, Victor Milanzi na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena.
Kisena aliachiwa huru kabla ya kufikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yanayomkabili licha ya Mahakama kutoa hati ya kukamatwa.
Ilidaiwa katika mashitaka yanayowakabili Simba na Milanzi, kuwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010 Dar es Salaam, walipanga njama kwa nia ya kujihusisha na vitendo vya rushwa katika ununuzi, pia walipokea Sh milioni 320 kutoka kwa Kisena, kama kishawishi cha kuiuzia kampuni hiyo hisa za Uda.
Simba, Milanzi na MwakingÕinda, wakiwa katika ofisi za Uda, Kurasini, Temeke, Dar es Salaam, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuuza hisa milioni 7.8 za shirika hilo, zilizokuwa zikimilikiwa na Serikali na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa Kampuni ya Simon Group bila kufuata mchakato wa zabuni.
Aidha, inadaiwa kati ya Septemba 2009 na Februari 2011, washitakiwa hao walitumia madaraka yao vibaya kwa kuuza hisa kwa Sh bilioni 1.1, bila kuhusisha wamiliki wa hisa hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Washitakiwa hao wanadaiwa kulisababisha shirika hilo hasara ya Sh bilioni 8.4 kutokana na kuuza hisa hizo kwa Sh bilioni 1.1, wakati kama wangefuata mchakato wa zabuni, wangeuza hisa hizo kwa Sh bilioni 8.4.
Katika mashitaka yanayomkabili Kisena, ilidaiwa kwamba akiwa Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group ambayo ilikuwa na nia ya kununua hisa kwa UDA, alitoa Sh milioni 320 kwa Simba na Milanzi, kama kishawishi cha kuruhusiwa kununua hisa hizo, kitendo ambacho ni kinyume na sheria za ununuzi wa umma.
Awali Simba na wenzake, walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya kusababishia shirika hilo hasara ya Sh bilioni 2.3, lakini (DPP) alifuta kesi hiyo ya jinai na kufungua kesi ya uhujumu uchumi na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh bilioni 8.4.