MBUNGE WA CCM ACHEKELEA SERIKALI KUKAMUA WANANCHI...

Ally Keissy Mohamed.
Wakati wabunge mbalimbali pamoja na Kamati ya Bunge ya Bajeti, wakipendekeza baadhi ya kodi kuondolewa,  Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy Mohamed (CCM) ameitaka Serikali iwakamue vilivyo wananchi.
Mbunge huyo alitaka Serikali baada ya kuwakamua wananchi, ijitegemee na kuacha kutafuta wajomba wa kuipa misaada kutoka Ulaya na kuwageukia wabunge na kuwataka waache kuitaka Serikali ipunguze kodi, wakati wao ndio wanaongoza kwa kuleta madai mbalimbali wakitaka Serikali iwatekelezee.
“Watu hapa mnadai barabara na maji, halafu wakati huo huo mnataka VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) ifutwe huku na kule, eleza tukifuta hiyo kodi wapi tupate fedha?
“Uingereza wanakamuana wanatuletea huku misaada, hadi televisheni zinalipiwa, hapa televisheni mnazo tatu tatu mpaka chooni na hamlipi hatuwezi kufuta kodi,”
alisisitiza na kusababisha kicheko.
Akijenga hoja zake huku akipigiwa makofi ya kibunge, Keissy ameitaka Serikali kuhakikisha watendaji watakaotumia vibaya kodi zilizokamuliwa kutoka kwa wananchi, wafilisiwe na baada ya hapo wanyongwe.
“Nashukuru sasa hivi ninaunga mkono na wabunge wengi kuhusu adhabu ya kifo, wengi wanasubiri iletwe hapa bungeni ili tuifanyie kazi…hata Sitta (Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel), alisema wanyongwe.
Mbunge huyo alitaka kila kitu kikatwe kodi bila huruma mpaka katika fedha za harambee na michango ya harusi ambako alipendekeza zikatwe asilimia 30 ya kodi.
“Hata wauzaji wa dawa za kulevya, wakatwe kodi, tusijali wanakozipeleka. Cha muhimu tuache kuombaomba. Nyie (wabunge) watu wa ajabu sana, Serikali ikiomba misaada kelele, ikitoza kodi kelele, nyie mkoje?
“Hivi mtu akioa mke na kuanza kuomba misaada kwa jirani, hivi huyo mke umeoa? Ni wa kwako?” Alihoji na kusababisha kicheko zaidi.
Akizungumzia matumizi ya Serikali katika magari aina ya Land Cruiser VX, Mbunge huyo alisema kauli za Serikali kwamba magari hayo yanauzwa kwa Sh milioni 200 mpaka Sh milioni 300 si za kweli.
“Eti gari Sh milioni 200 au 300, hakuna kitu, mimi nimenunua na risiti nitaleta ni Sh milioni 83, hizo fedha ni mkate wa mtu,” alisema.
Akizungumzia vipaumbele vya Serikali, Mbunge huyo aliuijia juu uamuzi wa Serikali kutenga fedha za kukarabati na kujenga viwanja vya ndege na kutaka fedha hizo zipelekwe katika reli.
“Nenda Tabora, Kigoma na Mwanza, uliza kati ya ndege na reli wanataka nini, kwanza mna ndege nyie? Mliua ATC (Shirika la Ndege la Tanzania) na wengine mpaka wamekufa hawakuchukuliwa hatua, …waleteni hapa hata kama wamekufa tusage mifupa yao.
“Ndege zitapakiwa na Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa na labda Mbunge, mtapakia migebuka huko au madebe ya mawese?” Alihoji na kusababisha kicheko. Alisisitiza umuhimu wa Serikali kutoa kipaumbele katika ujenzi wa reli zaidi ili kukuza uchumi.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item