MAONESHO YA SABASABA MWAKA HUU KWA TIKETI ZA KIELEKRTONIKI...

https://roztoday.blogspot.com/2013/06/maonesho-ya-sabasaba-mwaka-huu-kwa.html
![]() |
Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wakiwa katika harakati za kuingia kwenye Viwanja vya Sabasaba. |
Kwa mara ya kwanza katika kudhibiti mapato na kuondoa usumbufu kwa wananchi, tiketi za kuingia katika Maonesho ya 37 ya Kibiashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) mwaka huu zitakatwa kwa mfumo wa kielektroniki.
Aidha, katika maonesho hayo yanayoanza Juni 28 hadi Julai 8, maboresho kadhaa yamefanywa, ikiwemo kuwa na mabanda matatu maalumu ya kuonesha na kutangaza bidhaa zinazotengenezwa na kuzalishwa nchini, la watu wenye ulemavu na la kutangaza uzalishaji wa asali.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Jacqueline Maleko aliyasema hayo jana katika hotuba yake, iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Masoko wa Nje wa mamlaka hiyo, Anna Bulondo katika ufunguzi wa semina ya kujua sheria na kanuni za ushiriki kwa washiriki wa maonesho hayo.
Maleko alisema maboresho yaliyofanywa yanalenga kuongeza hamasa na ubora wa bidhaa kwa washiriki ili kupata na kuongeza masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi hasa ikizingatiwa kuwa maonesho hayo yanatambuliwa na Umoja wa Taasisi zinazoandaa Maonesho Ulimwenguni (UFI).
ÒTangu maonesho ya DITF yamekuwa mwanachama wa UFI, viwango vimekuwa vikipanda na kukubalika kimataifa na kusababisha ongezeko la washiriki, ndio maana mwaka huu TanTrade imeboresha mengi, ikiwemo ukatishaji wa tiketi kwa mfumo wa kielektroniki na kuongeza ukubwa wa mabanda ya kisasa ili kuondoa tatizo la ufinyu wa nafasi,Ó alisema Maleko.
Kwa mujibu wa Bulondo, viingilio vitabaki kuwa Sh 2,500 kwa watu wazima na Sh 500 kwa watoto kama mwaka jana lakini tiketi zote zitakatwa kwa mfumo mpya ili zisomeke katika mashine kuzuia kughushi.
Aidha, nchi 32 kutoka 11 za mwaka jana zitashiriki maonesho na kampuni 401 za nje na za ndani 1,600 zitashiriki huku taasisi za Serikali zikiwa 70. Alisema kuwa tofauti na mwaka jana, mwaka huu washiriki wamepangwa kisekta ili kuboresha ushiriki na upatikanaji wa mshiriki bora kupitia mchujo utakaofanywa na kampuni moja badala ya mchanganyiko wa majaji.
Alisema pia wameandaa mabanda maalumu ya kutangaza bidhaa zinazotengenezwa na kuzalishwa nchini, banda la watu wenye ulemavu pamoja na banda la asali ambalo ni matokeo ya maonesho maalumu ya asili yaliofanyika jijini humo Oktoba 4 hadi 7 mwaka jana ili kuongeza kutangaza bidhaa za hapa nchini.