MBUNGE WA CCM KUPANDISHWA KORTINI LEO SAKATA LA GESI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/06/mbunge-wa-ccm-kupandishwa-kortini-leo.html
![]() |
| Hasnain Murji. |
Ulinzi umeimarishwa mjini Mtwara wakati Jeshi la Polisi mkoani hapa likitarajiwa kumfikisha mahakamani Mbunge wa Mtwara Mjini Hasnain Murji (CCM).
Mbunge huyo anafikishwa kortini, kujibu tuhuma za kuchochea vurugu za kupinga mradi wa bomba la gesi kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.
Jana magari ya Serikali yalikuwa yakirandaranda yakiwa na watu waliovalia sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yakitangaza kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao na kuwataka wawaumbue wale wote wanaokula njama za kuleta fujo mkoani humo na hasa mjini Mtwara.
Pamoja na kutangaza kwamba ulinzi umeimarishwa na kwamba watu waendelee na shughuli zao, matangazo hayo pia yamekuwa yakibeba onyo kwamba mtu ambaye hatafungua biashara yake ili kuendelea kutoa huduma , basi atambue kwamba ataendelea kuifunga biashara hiyo kwa majuma matatu yajayo.
Ingawa hali ilionekana kuwa angavu, jana watu wengi walionekana kumiminika pia katika masoko kununua mahitaji yao kwa hofu ya hali kutokuwa njema leo, wakiwa na kumbukumbu ya yaliyojiri Mei 22 na 23 mwaka huu.
Aidha katika kile kinachoonekana kuwa ni hofu ya kuwapo kwa ghasia kama mwanzo, mamia ya wananchi wamefurika katika kituo cha mabasi Mjini Mtwara wakitafuta usafiri wa kuwatoa nje.
Mabasi yanayokwenda wilaya za jirani za Newala, Tandahimba Masasi na hata Lindi yalionekana kujaa na kuondoka huku abiria wengi wakihangaika kutafuta usafiri.
Mwandishi wa habari hizi alipohojiana na watoa huduma za usafiri wa mjini (daladala na bodaboda) , wengi wao walisema kwamba wakihakikishiwa ulinzi wataendelea kutoa huduma hizo, lakini wakiona shaka hawatatoa.
Aidha baadhi ya wananchi ambao wanafanya biashara kubwa hasa maduka na migahawa wamesema kwa hofu ya kuonekana wasaliti kesho watafunga biashara zao na kwenda kusikiliza hatima ya mbunge wao.
Mbunge huyo alikamatwa juzi nyumbani kwake maeneo ya Shangani majira ya jioni na kupelekwa kituo kikuu cha Polisi mjini hapa baada ya kupekuliwa nyumbani kwake.
“Ni kweli tunamshikilia Murji na hivi sasa tunamhoji na tukikamilisha tutamfikisha mahakamani…na tunawaomba wananchi na wakazi wa Mtwara wawe watulivu na waendelee na shughuli zao kama kawaida”, alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa.
Wakati mbunge huyo anafikishwa mahakamani leo viongozi wengine wa vyama vya upinzani wanne watafikishwa mahakamani kwa mara ya pili Juni 13.
Viongozi hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Juni 4, mwaka huu kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na mashitaka matatu ikiwamo kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Tanzania.
Viongozi hao ni Katani Ahmed Katani (33) Mwenyekiti wa Vijana Taifa CUF na Saidi Kulaga (45) Katibu wa CUF Wilaya ya Mtwara, Hassan Uledi (35) Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Wilaya ya Mtwara na Hamza Licheta (51) Katibu Mwenezi wa TLP Mkoa wa Mtwara. Wote wakazi wa Mtwara.
“Amekamatwa kwenye saa 11:00 jioni, na hati ya kukamatwa kwake imeeleza kuwa anatuhumiwa kuchochea vurugu za kupinga kusafirisha kwa njia ya bomba gesi inayopatikana mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam,” alisema Katibu wa Mbunge huyo, Meckland Millanzi.
Jana jioni pia kulikuwa na tetesi za kukamatwa kwa Mwenyekiti wa CCM, Mtwara na MNEC wake lakini uchunguzi unaonesha kwamba bado hawajakamatwa.
Mwenyekiti huyo na MNEC wake wanadaiwa kushiriki kikao cha kula njama za kuzuia gesi isisafirishwe kwenda Dar es Salaam.
Vurugu hizo zilizosababisha baadhi ya watu kupoteza maisha huku wengine wakiachwa majeruhi na mali nyingi kuharibiwa.
Mvutano kuhusu mradi wa bomba la gesi ulianza Novemba 16, mwaka jana baada ya Serikali kutuma kamati inayoratibu maoni ya sera ya gesi “The Natural Gas Policy of Tanzania -2013” ambayo ilifika mkoani Mtwara kukusanya maoni ya wananchi.
Katika mikutano yake mjini Mtwara, wananchi wengi hawakukubaliana na wazo la kusafirishwa gesi nje ya Mtwara kwa njia ya bomba madai ambayo yaliungwa mkono na Murji akidai kuwa ndio anaowasemea.
