VIGOGO WA CUF KILA MTU NA LAKE RASIMU YA KATIBA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/06/vigogo-wa-cuf-kila-mtu-na-lake-rasimu.html
![]() |
| Maalim Seif Sharif Hamad (kushoto) na Profesa Ibrahim Lipumba. |
Wakati Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiunga mkono Rasimu ya Katiba ya Muundo wa Serikali tatu, Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amepinga, huku akisisitiza kuwa Zanzibar lazima iwe Dola kamili inayojitegemea.
Juzi Profesa Lipumba aliunga mkono Rasimu hiyo katika eneo la Serikali tatu, huku akitaka mchakato mzima wa kujadili Rasimu ya Katiba kutoharakishwa hadi pale itakapopatikana Rasimu ya Katiba ya Tanzania Bara.
Akizungumza na wananchi Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja katika mkutano wa hadhara jana, Maalim Seif alisema suala la Zanzibar kuwa Dola kamili halizuiliki kwa sababu ndiyo maoni ya Wazanzibari wengi.
"Chama cha CUF na Wazanzibari maoni yao katika Rasimu ya Katiba yako wazi ni Dola kamili na kuwa na kiti chake Umoja wa Mataifa Rasimu hii ya Katiba ya Jaji Warioba hatuikubali hata kidogo," alisema.
Akifafanua, Maalim alisema kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa ikipuuzwa katika Muungano, huku ikichukuliwa kama sehemu ya Muungano na si mshiriki kamili wa Muungano huo uliozaliwa mwaka 1964.
Alisema kitendo cha Rasimu kutaka Serikali tatu ni sawa na kiinimacho huku kikiipa nguvu na kuitambua Serikali ya Tanganyika wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiendelea kukandamizwa na kutotambuliwa.
"Wazanzibari nawataka muwe macho na mbinu zinazofanywa na kuikandamiza Zanzibar na kutoitambua kama nchi kamili lakini namwambia Warioba hilo halitafanyika na nguvu ya umma itatumika kama Zanzibar haikutambuliwa kuwa Dola kamili," alisema.
Kwa mfano, Maalim Seif alisema, inasikitisha kuona nafasi za watendaji wakuu wote wa taasisi za ulinzi tangu mwaka 1964 zimekuwa zikishikwa na viongozi wa Tanzania Bara likiwamo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Usalama wa Taifa na Polisi.
ÒZanzibar hairidhishwi na muundo wa tume za uajiri katika vyombo vya ulinzi, ambazo ni za upande mmoja vyeo vyote vinakwenda kwa watendaji kutoka Tanzania Bara," alisema.
Alisema mfumo wa Serikali tatu kwa Zanzibar bado hauna maslahi kwa Wazanzibari ambao kwa muda mrefu wamenyonywa sana katika Muungano ambao unatokana na pande mbili ya nchi zilizo huru.
Mapema Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais alitaka wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao katika Rasimu ya Katiba kupitia mabaraza yao.
Alisema mapambano ya kudai Zanzibar kamili kupitia sehemu ya pili ya mchakato wa Katiba yanaendelea pamoja na safari ya kuelekea kupiga kura ya maoni.
"Nawaomba Wazanzibari mapambano ya kudai Zanzibar huru bado yapo na kwa sasa tutumie fursa hiyo kupitia mabaraza ya Katiba," alisema.
Alitoa onyo kali kwa watendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ikiwamo Sekretarieti na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kuhusu alichosema ni mbinu za kuvuruga Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ikiwamo kunyima wananchi haki zao za msingi.
Alidai zipo mbinu za kunyima fursa wananchi zaidi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kuandikishwa katika Daftari hilo ikiwamo kunyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi kwa malengo ya kuibeba CCM.
"Nakupa onyo kali ewe Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jecha pamoja na Sekretarieti yako... nchi haitakalika kama ukijaribu kuwanyima wana CUF kusajiliwa katika Daftari la Wapiga Kura huwezi kuzuia nguvu ya umma kwa sasa," alisema.
ZEC inatazamiwa Juni 29 kuanza kuandikisha wananchi wenye sifa kwenye Daftari ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Mapema Maalim Seif alipokea wanachama wapya 609 wakiwamo 160 waliohama CCM.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Hamad Masoud alipongeza wanachama hao kwa kuonesha mapenzi ya wazi ya kujiunga na chama hicho kwa hiari.
"Tunawakaribisha wanachama wote wapya waliojiunga na CUF...tunataka kuivunja ngome ya CCM katika Mkoa wa Kaskazini Unguja," alisema.
Katika maoni ya Rasimu ya Katiba, Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba alisema CUF imepokea mapendekezo ya Serikali tatu huku akitaka wananchi wapewe muda zaidi wa kuchangia Rasimu hiyo katika maeneo mbalimbali.
Profesa Lipumba alisema hata hivyo ni vema Rasimu hii isiharakishwe bila kwanza kuangalia jinsi Katiba za Bara na Visiwani zitakavyokuwa bila kuathiri Katiba ya Muungano.
Alipendekeza wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Bara waandae Rasimu ya Katiba ya Bara na wale wa Zanzibar nao waandae Rasimu ya Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoka katika ziara ya wiki moja nchini China mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Dk Ali Mohamed Shein alitaka viongozi wa vyama vya siasa kuacha jazba na badala yake waelekeze wananchi kuchangia Rasimu hiyo kuanzia mabaraza ya Katiba hadi kura ya maoni, huku akisisitiza hakuna sababu ya wananchi kushawishiwa kufanya fujo.
