MPASUKO WAIBUKA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR...

https://roztoday.blogspot.com/2013/06/mpasuko-waibuka-serikali-ya-umoja-wa.html
Moja ya vikao vya Baraza la Wawakilishi Zanzibar. |
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar imeanza kupata ufa kutokana na mawaziri kukosa umoja na kujitenga katika shughuli za Serikali na kushindwa kuwapa mapokezi viongozi wa kitaifa.
Hayo yameelezwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM na CUF wakati wakijadili na kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi, Mohammed Aboud.
Akichangia hotuba ya makadirio ya ofisi hiyo juzi, Mwakilishi wa Viti Maalumu, Asha Bakari (CCM) ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) alisema lengo la kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa limepoteza mwelekeo.
Alisema mawaziri wa CUF wamekuwa wakikwepa shughuli za kitaifa za Serikali na kutoa mfano viongozi wote kushindwa kuhudhuria uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru uliowashwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein, Chokocho, Pemba.
Alisema kitendo cha mawaziri kutohudhuria shughuli hiyo ya kitaifa kinakwenda kinyume na lengo la kuunda Serikali hiyo ikiwamo kudumisha amani na Umoja wa Kitaifa kwa wananchi wake.
“Mawaziri wanafikia kukimbia shughuli za Mwenge wa Uhuru, hali hii ni kwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema.
Mchango wa mwakilishi huyo uliungwa mkono na Mwakilishi wa Kwahani, Ali Salum (CCM) ambaye alisema hofu ya wananchi kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa kushindwa kufikia malengo yake imetimia.
Alisema wananchi wa Zanzibar mapema walionekana kuwa na wasiwasi kubadilishwa kwa Katiba na kukaribisha mfumo mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutokana na kutokuwapo kwa nia njema ya kujenga Zanzibar moja.
“Wananchi wengi wa Zanzibar walikuwa na wasiwasi kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa nikiwamo mimi…leo wanaona wenyewe utendaji kazi wa viongozi wao wakiwemo mawaziri,” alisema.
Hoja hizo zilipingwa na wawakilishi wa CUF akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Hamada Masoud ambaye ni Mwakilishi wa Ole pamoja na Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa ambao waliibua mjadala mkali.
Jussa alisema viongozi wa CCM ndio chimbuko la tatizo akidai wameshindwa kumpa heshima Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad ikiwamo kujitokeza kumpokea wakati anaporudi safari za ndani na nje ya nchi.
“Ukipanda mbigiri utavuna mbigiri, mimi nimekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF wakati mwingine nilikuwa nakwenda kumpokea Makamu wa Kwanza bila kuwapo Mkuu wa Mkoa au mawaziri kutoka CCM,” alisema Jussa.
Hata hivyo, alisema wapo watu hawana nia njema na Serikali hiyo, lakini malengo yao hayatatimia kwa sababu imewekwa kwa mujibu wa Katiba na waamuzi ni wananchi wa Zanzibar wenyewe.
Alisema Katibu Mkuu Kiongozi ndiye alianza kuzorotesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kitendo cha kutupilia mbali ripoti ya muundo wa Serikali hiyo kwa watendaji wa Serikali na kusababisha Serikali kuwa na viongozi wa kisiasa tu bila kuhusisha watendaji wake.
Mwakilishi Hamad Masoud wa CUF alisema ipo hatari Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ikarudisha migogoro ya kisiasa kwa sababu watendaji wake hawataki kubadilika.