SAMWELI SITTA AAGWA RASMI KAMA SPIKA...

https://roztoday.blogspot.com/2013/06/samweli-sitta-aagwa-rasmi-kama-spika.html
![]() |
Samweli Sitta. |
Bunge la Jamhuri ya Muungano juzi usiku lilimuaga aliyekuwa Spika, Samweli Sitta na kumsifu kwa kutetea maslahi ya watumishi wa Bunge na kuendesha Bunge la Spidi na Viwango.
Katika hafla hiyo ambayo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikuwa mgeni rasmi, wafanyakazi wa Bunge, wabunge na Waziri Mkuu, walimzawadia Sitta vitu mbalimbali kama ishara ya kumuaga.
Akizungumza baada ya kupewa zawadi hizo, Sitta ambaye kwa sasa ni Waziri wa Afrika Mashariki, alisema hakutarajia kufanyiwa hafla kubwa ya kumuaga na kumshukuru Spika Anne Makinda, kwa heshima aliyompa.
Pia alimshukuru Waziri Mkuu, kwa kukubali kuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo, wakati alikuwa ametoka safari na alikuwa na mkutano wa zaidi ya saa moja muda mfupi kabla ya kuanza kwa shughuli hiyo.
Naye Waziri Mkuu alimshukuru kwa kumlea tangu walipokutaka Ikulu wakati huo Pinda akiwa karani na hata alipokuwa mtumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria, wakati huo Sitta akiwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Spika Makinda naye alikumbusha kwamba Sitta ni Spika mstaafu na Bunge linawajibika kumlea kwa wadhifa huo, pamoja na kwamba ameteuliwa kuwa Waziri.
Baada ya Bunge kama taasisi na watumishi wa Bunge kumpa zawadi zao, wabunge wa CCM, NCCR Mageuzi na CUF walipata nafasi ya kumpa zawadi na mkono wa kwaheri.
Miongoni mwa zawadi alizopewa ni pamoja na Kiwanja mkoani Dodoma chenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 10, ili ajenge makazi yake Dodoma, zaidi ya Sh milioni 10 taslimu zilizochangwa na watumishi kwa kukumbuka alivyotetea maslahi yao.
Wabunge wa CCM wakiongozwa na Katibu wao, Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, walimzawadia mke wa Sitta, Margaret vitenge na khanga, seti ya blangeti sita na Sh milioni moja taslimu, akanunue ng’ombe wa maziwa.
Waziri Mkuu alitoa zawadi binafsi ikiwemo mashine ya jokofu, flat screen ya nchi 46, mashine ya kupoza maji ya kunywa na vingine ambapo mke wa Sitta, Margaret aliwashukuru wote na kusema amejiona kama amefanyiwa 'kitchen party'.