NI FURAHA AU KILIO KWA WAFANYAKAZI WIKI HII...
https://roztoday.blogspot.com/2013/06/ni-furaha-au-kilio-kwa-wafanyakazi-wiki.html
![]() |
| Dk William Mgimwa. |
Dhamira ya Serikali ya kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wake itajulikana wiki hii ambapo inatarajiwa kuwasilisha bungeni bajeti yake kwa mwaka ujao wa fedha.
Bajeti ya Serikali ya Sh trilioni 17.7 itasomwa na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa Alhamisi saa kumi alasiri. Siku hiyo asubuhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano) Steven Wasira atawasilisha bungeni hali ya uchumi na mipango ya Taifa.
Hotuba ya Wasira itaweka sura ya bajeti ya Serikali kwa kuainisha vipaumbele vya taifa ambavyo viko kwenye mpango wa Taifa wa miaka mitano pamoja na utekelezaji wake kwa mwaka wa fedha unaomalizika mwezi huu wa Juni.
Wasira kwa sasa ndiye Waziri anayesimamia Tume ya Mipango ambayo utendaji wake unasimamiwa na Ofisi ya Rais. Mtendaji Mkuu wa tume hiyo ni Dk Phillip Mpango.
Kwa kuwa tayari wizara zote zimeshaainisha mapato na matumizi yake, kinachosubiriwa kwa hamu kwa sasa ni kuona mipango ya Serikali ya kumpunguzia ukali wa maisha mwananchi wa kawaida ikiwa ni kupunguza kodi katika bidhaa mbalimbali.
Kuanzia Ijumaa iliyopita mpaka kesho kutwa tayari kumeanza kufanyika kwa vikao vya kushauriana kati ya Serikali na Kamati ya Bajeti ya Bunge na hatimaye kufanya majumuisho kuzingatia hoja zenye maslahi kwa Taifa zilizojitokeza wakati wa kujadili bajeti mbalimbali za Wizara.
Miongoni mwa mambo ambayo wananchi watahitaji kusikia kwenye bajeti hiyo ni ahadi ya Serikali ya kupunguza kodi kwa wafanyakazi kama ambavyo kimekuwa kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi kupitia vyama vya vya wafanyakazi.
Akihutubia Taifa Mei Mosi mwaka huu jijini Mbeya, katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Rais Jakaya Kikwete, alisema Serikali yake imesikiliza kilio cha wafanyakazi na kuwahakikishia kuwa mwaka huu itashusha kiwango cha kodi ya mshahara (PAYE).
Hata hivyo, Rais Kikwete hakutaja kiwango kipya, badala yake alisema Waziri wa Fedha, Dk Wiliam Mgimwa, atatoa ufafanuzi wa suala hilo katika hotuba yake ya bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2013/14.
Mapendekezo ya vyama hivyo ni kutaka kiwango cha kodi wanachokatwa wafanyakazi kinabaki tarakimu moja tofauti na sasa wafanyakazi wamekuwa wanakatwa kiasi kikubwa hadi kufikia tarakimu mbili kulingana na kiasi anachapokea mfanyakazi.
Maeneo mengine ambayo Serikali imeshauriwa ni kuacha kutoa misamaha ya kodi isiyo ya lazima na pia ipunguze posho na kupunguza tofauti ya mshahara wa kima cha chini na mshahara wa juu ili uweze kumudu kulipa mshahara wenye tija kwa wafanyakazi.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi(TUCTA) wakati wa sherehe hizo za Mei Mosi liliishauri Serikali kupunguza misamaha ya kodi hadi asilimia moja ya pato la Taifa, hatua ambayo itaokoa zaidi ya Sh bilioni 600 kila mwaka. Kwa hali hiyo hotuba ya Dk Mgimwa itafafanua suala hilo.
Tucta inaamini kuwa Serikali ikizingatia ushauri huo na kutekeleza, itafanikiwa kuokoa mabilioni ya fedha ambazo zinatumika pasipo na maslahi ya Taifa na zikiingizwa katika bajeti ijayo itaboresha mishahara ya wafanyakazi, kuwapunguzia mzigo wa kodi ya mapato (PAYE) na kuboresha pensheni ya wastaafu.
Licha ya kupunguza kodi hiyo, wananchi pia wanatarajia kusikia wigo mpana wa kodi ukitekelezwa na Serikali ni kutoza kodi huduma za kutuma na kupokea pesa kwa kutumia simu za mkononi.
Huduma hizo ambazo kwa sasa zinatolewa na M pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na Easy Pesa hazitozwi kodi yoyote na tayari Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameainisha eneo hilo kuwa ni muhimu kutozwa kodi.
Katika kupanua kodi hiyo, pia CAG alishauri kumbi za harusi ambazo kwa sasa ni nyingi katika maeneo mengi ya miji kuwa nazo zitozwe kodi kwa vile zinaingiza fedha nyingi lakini wamiliki wa kumbi hizo wamekuwa hawatozwi kodi yoyote.
Mjadala kuhusiana na bajeti hiyo unatarajiwa kuchukua siku saba na utaanza Jumatatu wiki ijayo, ambapo michango mbalimbali inatarajiwa kutolewa na wabunge, ambapo Watanzania watakuwa na hamu na shauku kubwa ya kutaka kujua katika mwaka ujao wa fedha, Serikali imepanga nini katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Sura ya bajeti ya Alhamisi imelenga kutekeleza vipaumbele vya Taifa yenye lengo la kufikia dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2015. Vipaumbele ni nishati ya umeme, kuboresha miundombinu ya bandari na reli, kilimo, utafutaji wa mapato, elimu na maji.
Bajeti ya mwaka 2012/13 ililenga kukabiliana na changamoto zinazokabili uchumi ikiwa ni pamoja na; kuongeza fursa za kukuza uchumi, kushughulikia uhaba wa chakula nchini, kupambana na mfumuko wa bei, kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kusimamia matumizi, kushughulikia suala la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.
Bajeti hiyo pia ililenga kuwekeza katika miundombinu ya nishati ya umeme hususan ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, barabara, bandari na reli ya kati ili kupunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza tija katika uzalishaji; pamoja na kulipa madeni ya ndani na nje.
Kwa kuzingatia sera za uchumi pamoja na misingi na sera za bajeti, Serikali ilitarajia kukusanya Sh trilioni 15.1. Makusanyo yasiyo ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 8.7 (asilimia 18 ya Pato la Taifa). Mapato kutokana na vyanzo vya halmashauri ni Sh bilioni 362.2 (sawa na asilimia 0.7) ya Pato la Taifa.
Washirika wa maendeleo walitoa misaada ya Sh trioni 3.2. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 842.5 ni misaada na mikopo ya kibajeti na Sh trilioni 2.3 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo ilijumuisha Basket Funds na fedha za Millenium Challenge Account (MCA – T).
